JE HAMASA YA SAMIA KWA TAIFA STARS KUIMALIZA UGANDA KESHO?
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kesho Jumanne watashuka dimbani, katika Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam kuvaana na timu ya taifa ya Uganda katika mchezo wa marudiano, kuwania kufuzu kombe la mataifa Africa.
Katika mchezo wa awali, Taifa Stars ilifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na kiungo mshambuliaji, Simon Msuva, dakika ya 68, akimalizia kazi nzuri ya krosi kutoka kwa Dickson Job, ambaye alipokea pasi nzuri kutoka kwa Mdhamiru Yassin.
Bao hilo limewafanya wachezaji wa TIMU YA TAIFA ya Tanzania, Taifa Stars kupewa Sh Mil 10 kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa motisha kwa wachezaji kwa kununua kila goli moja Sh Mil 10.
Pia mama ametoa ahadi ya Sh Mil 500 kama wakifanikiwa kufuzu na kucheza, kombe la mataifa barani Africa ‘’Afcon’’. Mashindano ambayo yanatarajiwa kufanyika Januari, mwakani nchini Ivory coast.
Kwa namna ambavyo matokeo ya awali yamekuwa wachezaji wa Taifa Stars wanatakiwa kupambana ili waendelee kuogelea mamilioni ya Mama, pamoja na kuliheshimisha taifa.
Katika mchezo huo wa kesho dhidi ya Uganda, wachezaji wanatakiwa kupambana kufa au kupona kwa sababu mbili, moja ni kufuzu kucheza Afcon na nyingine ni kuchukua mamilioni ya Mama.
Stars katika kundi lao, wapo katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 4 huku Algeria wakiongoza kundi wakiwa tayari wameshafikisha jumla ya pointi 9, Niger akiwa na pointiu 2 na Uganda ikiwa na pointi moja pekee.
Katika mchezo huo, Stars wanatakiwa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu, pamoja na tahadhari kubwa ya kushambulia na kulinda goli lao, kwani Uganda hawatakubali kufungwa kwa mara ya pili na Taifa Stars, ndani ya siku 7.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars Adel Amrouche anategemewa kuingia uwanjani na mbinu zile zile ambazo alizitumia katika mchezo uliopita ambao ulimpa ushindi wa bao 1-0 ugenini ambao ulipigwa nchini Misri.
Amrouche anaonekana kupendelea kutumia mfumo wa 3-5-2 akijaza viungo wengi wakabaji walioanza pamoja ambapo Novatus Dismas, Himid Mao, Mudathiri Yahya na Mzamiru Yassin walifanikiwa kuwadhibiti viungo hatari wa Uganda akiwemo Khalid Aucho anayeichezea Yanga ya hapa nchini.
Akizungumzia mchezo wa kesho, Amrouche anasema amewaandaa wachezaji wake kucheza mechi dhidi ya Uganda kwa nidhamu na tahadhari kubwa.
“Haikuwa kazi rahisi kupata matokeo ugenini dhidi ya Uganda, kwani ni timu iliyokuwepo pamoja muda mrefu inayoundwa na wachezaji wengi vijana na wanaocheza katika mataifa yaliyoendelea kisoka kama Uhispania.
“Tuliwaheshimu wapinzani ndani ya uwanja, hiyo ndio sababu ya msingi iliyotupa matokeo mazuri katika mchezo wa kwanza na sasa tuna nafasi nyingine ya kupata matokeo mazuri iwapo kila mchezaji atafuata maelekezo ya kile ambacho ninawaagiza kufanya.
“Nawapongeza wachezaji kwa kupambana na kufanikiwa kupata ushindi wiki iliyopita, ambao unamfanya kila Mtanzania kuwa na furaha.
“Kwa muda mfupi ambao nimekaa na timu, wachezaji wameweza kufuata maelekezo na mfumo wangu ambao ninautumia ili kupata matokeo mazuri ya ushindi.
“Ni matumaini yangu, siku ya kesho, wachezaji wangu watajitahidi kupambana katika mchezo huu wa marudiano dhidi ya Uganda, kwani haitakuwa mechi nyepesi licha ya kuwepo nyumbani,” anasema Amrouche.
Mfungaji wa bao la Taifa Stars Simon Msuva ameahidi kufanya kama ambavyo amefanya kule nchini Misri, kuipatia Tanzania ushindi iwapo atapata nafasi ya kuwemo katika mchezo unaotarajiwa kupigwa siku ya kesho, kwenye dimba la Mkapa.
“Kama mchezaji nipo kwa ajili ya nchi, pia ninahitaji sapoti ya mashabiki kuja uwanjani na kutushangilia, ama kutupa moyo wakati tunacheza dhidi ya Uganda.
“Ninaamini kelele zao za kutushangilia zinasaidia kuwachanganya na kuwatoa mchezoni wachezaji wa timu pinzani na sisi kutuongezea nguvu na kutufanya tuwe wepesi.
“Kama wachezaji kwa pamoja tumekubaliana kupambana kupata matokeo katika michezo iliyobakia katika kundi letu ili tufuzu Fainali ya Afcon,” anasema Msuva.
Kuonyesha ni namna gani kocha wa Taifa Stars amepania kupata ushindi, Amrouche amewaongeza kikosini mabeki wa pembeni wa Simba, Shomari Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chake.
Ni matumaini yetu wachezaji wa timu ya Taifa, wataitoa nchi kimaso maso huku wakichagizwa na hamasa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye tayari ameshatoa tiketi 2000, pamoja na ahadi ya Mil 10 kwa kila goli.
Sisi kama SportPesa tunategemea kuweka mechi hii.