UGANDA VS TANZANIA- Stars kulipa kisasi?
Timu ya taifa ya Uganda inatarajiwa kuikaribisha Taifa Stars kwenye Uwanja wa Suez Canal, Ismailia nchini Tunisia, kuwania nafasi ya kufuzu kombe la Africa.
Mchezo huu wa kuwania kufuzu Fainali za Afcon, mwenyeji ni Uganda na umepelekwa Tunisia kutokana na wenyeji Uganda kutokuwa na uwanja unaokidhi vigezo vya kutumika, katika mashindano ya kimataifa yanayotambuliwa na CAF au FIFA.
Mchezo huu, unachukuliwa kwa umuhimu mkubwa sana,kwa kila timu kutaka kupata ushindi ili ijiweke katika nafasi nzuri ya kufuzu.
Timu hizi mbili, yaani Uganda na Tanzania, mara ya mwisho kukutana, ilikuwa mwaka jana katika mechi za kuwania kufuzu kombe la Chan.Taifa Stars ilifungwa michezo yote miwili, wa nyumbani 1-0 kabla ya kwenda kurudiana Uganda na kufungwa 4-0.
Kuelekea mchezo huu, Taifa Stars itaanza kibarua hicho ikiwa na Kocha Mkuu mpya Adel Amrouche ambaye raia wa Ubelgiji, mwenye asili ya Algeria, aliyechukua mikoba ya ukocha akimrithi Kim Poulsen.
Hichi ni kibarua kigumu kwa Amrouche ambaye ameajiriwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndio inamlipa mshahara.
Katika mchezo huu, Stars itaingia uwanjani kuvaana na Uganda ikiwa na nyota wake wote muhimu walioitwa na kocha Amrouche.
Baadhi ya nyota hao ni pamoja na nahodha Mbwana Samatta anayekipiga klabu ya Genk ya nchini Ubelgiji wengine ni Simon Msuva, Novatus Dismas, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Himid Mao, Mudathiri Yahya na Kelvin John ‘Mbape’.
Katika mchezo huu, Uganda wataingia kwa tahadhari kubwa ya kuwazuia wachezaji wawili ambao ndio hatari kuelekea mchezo huo ambao ni Samatta na Msuva.
Historia ya Samatta inaonyesha, mshambuliaji huyu nguli wa Tanzania, amewahi kuichezea klabu ya Aston Villa ya Uingereza kabla ya kurejea Genk ambako ndiko anapocheza mpaka sasa. Mchezaji huyo pamoja na wachezaji wengine kama Dismas, wataifanya Uganda icheze kwa tahadhari kubwa na kutowapa nafasi ya kumiliki mpira.
Stars wanategemewa kucheza mechi hii kwa kujiamini kutokana na wachezaji wengi muhimu kucheza nje ya Tanzania, huku Uganda nao kama ilivyotanzania wakikosa mashabiki wa kutosha kuwashangilia.
Akizungumzia mchezo huu, Kocha Amrouche anayetumia mfumo wa 4-2-3-1 alisema kuwa maandalizi ya kikosi chake yanakwenda vizuri na ninafuraha kuwa na wachezaji wote wanaocheza soka nje ya nchi ikiwemo Ulaya.
“Ninaamini uwepo wa wachezaji wangu hao wote, utanipa wigo mpana wa kupanga kikosi imara kitakachopata matokeo mazuri katika mchezo huo.
“Katika mchezo huu tutaingia uwanjani tukiwa tunawaheshimu wapinzani wetu Uganda ambao kwa mechi hii wanahesabika kama wapo nyumbani ,” anasema Amrouche.
Akizungumzia mchezo huu, nahodha wat imu ya Taifa Stars, Mbwana Samatta anasema kuwa kihistoria, mechi inazozikutanisha Stars dhidi ya Cranes, siku zote inakuwa mgumu hasa kwa upande wa Taifa Stars.
“Nina amini, licha ya ugumu uliopo baina ya timu hizi mbili zinapokutana, benchi la ufundi, pamoja na wachezaji wote, tutashikamana kwa pamoja na kupata matokeo mazuri ya ugenini.
“Uwepo wa kocha mpya ambaye yeye atakaa katika benchi kwa mara ya kwanza hakutatufanya tupoteze mchezo huu, lakini itakuwa chachu ya kutumia ujuzi, uwezo na maarifa yake katika mechi za kimataifa.
“Kikubwa zaidi ni kwa sisi wachezaji, kuuelewa mfumo na aina ya uchezaji ambao kocha anautaka ili tupate matokeo mazuri ya ushindi. Mimi kama nahodha wat imu, pamoja na wachezaji wenzangu kwa pamoja tunaahidi kumpa ushirikiano wa kutosha kocha wetu mpya,” alisema Samatta.
Kwa upande wa Uganda wenyewe wataingia uwanjani katika mchezo huu wakiwa na kocha wao Mserbia, Milutin Sredojević Micho ambaye analifahamu vizuri soka la Tanzania.
Stars imekuwa ikipata ugumu wa kupata matokeo mazuri mbele ya Micho, kutokana na uzoefu wa kulijua soka la Tanzania alipokuwa akiifundisha Yanga.
Kwa upande wa Micho yeye amesema kuwa timu hizo zinapokutana upinzani unaongezeka kwa kiasi kikubwa, hiyo imetokana na ujirani uliokuwepo kati ya Uganda na Tanzania.
“Maandalizi ya timu yangu yamekamilika na kwa kiasi kikubwa hautakuwa mchezo mwepesi, hivyo tutaingia uwanjani tukiwa tunawaheshimu wapinzani wetu Taifa Stars.
Katika mchezo wa leo, Stars ina kibarua kigumu mbele ya kiungo mkabaji anayekipiga klabu ya Yanga, Khalid Aucho aliyekuwa katika kiwango kizuri.
Ni mchezaji anayeimudu vema nafasi ya kiwango, huyo huenda akawa mchezaji wa kuchungwa kwa upande wa Stars kutokana na kuimudu vema nafasi ya kiungo kwa kupiga pasi zenye madhara katika goli la wapinzani.
Wapo viungo wengine hatari kama kama Bobosi Byaruhanga na Allan Okello ambao wana umiliki mzuri wa kiungo, waliowahi pia kutakiwa na klabu za Simba na Yanga katika misimu hii miwili.
Pia Uganda wana kiungo mshambuliaji, Emmanuel Okwi ambaye yeye ni hatari zaidi kwa mabeki wa Stars wanatakiwa kuongeza makini kumzua nyota huyo aliyeng’ara akiwa anaichezea klabu ya Simba ya Tanzania.