Mastaa Simba- YangaMastaa Simba- Yanga


BAADA ya kumalizika kwa kelele za mchezo wa Dabi ya Kariakoo, mchezo ambao ulipigwa juzi Jumamosi wababe hao Simba na Yanga kesho Jumanne watarudi tena uwanjani kesho Jumanne kuendelea na ratiba za michezo mingine ya ligi Kuu Bara ambapo Simba wanatarajia kuvaana na Tanzania Prisons mkoani jijini Mbeya, huku Yanga ambao wanadhaminiwa na kampuni bora ya michezo ya kubashiri ya SportPesa wao wakiwa na kibarua cha kuvaana na JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

SIMBA
Prince Dube akipambana na Abdalazak Hamza

BAADA YA KIPIGO, SIMBA WAAPA KUTORUDIA MAKOSA

Kuelekea mchezo huo, kocha mkuu wa Simba Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema mchezo wa kesho dhidi ya Tanzania Prisons utakuwa mgumu kutokana na timu kukosa muda mzuri wa kufanya maandalizi, mara baada ya kutoka kucheza mechi kubwa na ngumu ya Dabi na kikosi chake hakijapata muda wa kurejesha utimamu wa mwili na kesho wanatakiwa kushuka dimbani. Hata hivyo kocha huyo ameongeza kuwa amekiandaa kikosi kiakili kuhakikisha kinapata matokeo chanya.

“Utakuwa mchezo mgumu kutokana na kukosa kupata muda wa kufanya mazoezi sababu ya kucheza mechi ngumu iliyopita ya dabi, ila tupo hapa kwa ajili ya kuhakikisha tunapata ushindi,” amesema Kocha Fadlu.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji nahodha wa Simba, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema utakuwa mchezo mgumu lakini wapo tayari kufauata maelekezo kutoka kwa walimu wao. Zimbwe Jr ameongeza kuwa wanajua mashabiki hawajafurahishwa na matokeo ya mchezo uliopita lakini kesho watajitajidi kuwapa furaha.

“Sisi kama wachezaji tupo tayari kufuata maelekezo tutakayopewa na makocha, na kila atakayepata nafasi atahakikisha anapambana ili kuwapa furaha Wanasimba,” amesema Zimbwe Jr.

ALICHOSEMA AHMED

SIMBA
Ahmed Ally

Mara baada ya kupoteza mchezo huo, Meneja wa habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema : “Tunaumia kwa kupoteza mchezo wa derby lakini tunajipongeza kwa kuwa mradi wetu wa kutengeneza timu umeanza kutoa matunda tena kwa haraka sana. Wote ni mashahidi misimu kadhaa nyuma tulifungwa derby na kuzidiwa kwa dakika zote 90.

“Jana tumeona tofauti kubwa, tumefungwa lakini tumeutawala mchezo kwa asilimia kubwa na kama kila kitu kingekua sawa basi tungeshinda mchezo ule. Muhimu kwetu wana Simba kwanza tukubali tumepoteza na wala hakuna haja ya kuanza kuhesabu tumepoteza mara ngapi, Mpira ni maisha ya duara muda wetu utafika na sisi tutatawala derby kwani tumewahi kufanya hivyo.

“Muhimu kwa sasa ni kusahau yaliyotokea na kujipanga upya kwa vita iliyo mbele yetu. Tumebakiwa na michezo 24 nguvu kubwa iwe kushinda michezo hiyo, tumepoteza derby sio ubingwa. Na pia tuwekeze nguvu kwenye mchezo wetu Jumanne dhidi ya Tanzania Prison. Ubaya Ubwela unaendelea.”

YANGA WATAMBA KUENDELEZA VIPIGO

SIMBA
Miguel Gamondi

Akizungumzia mchezo wa kesho Jumanne, kocha wa Yanga Miguel Gamondi amesema: “Tupo tayari tena kujianda na mchezo mwingine. Tunakwenda kucheza na timu ambayo imepoteza mchezo mmoja na kutoka sare michezo minne, kimsingi wanaonekana ni wagumu lakini tunajua nini chakufanya. Nafahamu msimu uliopita tulishinda magoli matano, walikuwa na timu tofauti na mwalimu tofauti.

“Kwangu mimi sitazami yaliyopita. Yaliyopita yamepita natazama yajayo, nimewaona wanavyocheza msimu huu wapo vizuri hivyo nakwenda kucheza nao kwa namna wanavyocheza na sio kutazama awali walikuwaje. Naomba niweke sawa jambo hili kwa mashabiki, mimi mipango yangu sio timu ifunge magoli mengi, mimi napenda timu yangu itengeneze magoli mengi. Yakipatikana magoli mengi sawa lakini lengo kuu ni alama tatu.”

KARIAKOO DABI HALI ILIKUWAJE?

SIMBA
Bacca na Ateba

Huu ulikuwa mchezo wa pili kwa timu hizo kukutana msimu huu, hii ni mara baada ya mchezo wa ngao ya jamii, huku pia ukishuhudia Simba wakipoteza kwa mara ya pili kwa idadi ileile ya mabao kama ambavyo ilitokea katika mchezo wa kwanza. Lakini je, mchezo ulikuwaje?

Simba walianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata nafasi ya wazi dakika za mwanzoni ambayo waliipoteza baada ya mshambuliaji wao, Leonel Ateba kuchelewa kufanya maamuzi kabla ya mlinda mlango wa Yanga, Djigui Diara kuokoa hatari hiyo.

Katika dakika 30 za mwanzo Simba walimiiliki sehemu kubwa ya mchezo huku Yanga wakifanya mashambulizi machache lakini ya nguvu. Yanga walipata bao pekee la mchezo dakika ya 86 baada ya mlinzi wa Simba, Kelvin Kijili kujifunga katika jitihada za kuokoa mpira wa krosi uliopigwa na Maxi Nzengeli.

VIKOSI VILIVYUMANA JUMAMOSI NI;

SIMBA 

Camara, Kapombe (Mukwala 88′), Zimbwe Jr, Che Malone, Hamza (Chamou 68′), Kagoma (Okajepha 45′), Kibu (Kijili 82′), Fernandez, Ateba, Ahoua, Mutale (Balua 68′)

YANGA

Diara, Yao, Boka, Bacca, Job, Aucho, Nzengeli, Mudathir (Mwamnyeto 87′), Dube (Musonda 61′), Aziz Ki (Chama 83′), Pacome (Mzize 61′)

Walioonyeshwa kadi: Boka 36′ Job 47′ Bacca 54′ Aucho 77′ Diara 90+5

 

Share this:

By Joel Thomas

Joel Thomas is a Tanzanian sports writer with a BSc (Education) from Mwenge Catholic University. He spent 4 years at Global Publishers and is in his second year with SportPesa, covering football and betting education for local fans. Anapenda soka na anaandika kwa uwajibikaji.