KARIAKOO Dabi Uwanja wa Mkapa dakika za jasho zimevuja ikiwa huzuni kwa Simba na kicheko kwa Yanga baada ya kushuhudia ubao ukisoma Simba 0-1 Yanga na bao la ushindi likifungwa na Maxi Nzengeli dakika ya 86 akitumia makosa ya mlinda mlango Camara kutema mpira wa faulo iliyopigwa na Clatous Chama mchezaji wa zamani wa Simba.
DAKIKA 45 ZA KARIAKOO DABI

Dakika 45 za mwanzo kwenye Kariakoo Dabi hakuna timu ambayo imeshuhudia lango la mwenzake kutokana na mbinu kukwama kuwapa matokeo. Simba walianza kwa kasi kubwa kuliandama lango la Yanga ndani ya dakika 15 za mwanzo na walipata kona ya mapema na faulo iliyopigwa na Jean Ahoua lakini haikuleta matunda.
Yanga walikuwa wanashambulia kwa kushtukiza huku wakimtumia Aziz Ki na Prince Dube kwenye kushambulia na walifanya shambulizi moja la hatari kupitia kwa Pacome dakika ya 41 likaokolewa na Mussa Camarra huku Ateba wa Simba dakika ya 5 alikosa utulivu akiwa ndani ya 18 na shujaa akwa Diarra.
VIKOSI KAZI HIVI HAPA
Kikosi cha Simba ambacho kilipangwa kuanza kilikuwa namna hii:-
Mussa Camara, Shomari Kapombe, Mohamed Hussen ambaye ni nahodha, Abdulazack Hamza, Che Malone, Yusuph Kagoma, Kibu Dennis, Ferndez Mavambo, Leonel Ateba, Jean Ahoua na Joshua Mutale.
Kwa wachezaji wa akiba ni Ally Salim, Kelvin Kijili, Fabrince Ngoma, Awesu Awesu, Okejapha, Edwin Balua, Steven Mukwala, Shadrack, Benjamin.
KIKOSI CHA YANGA HIKI HAPA

Dijgui Diarra, Yao, Ladack Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Prince Dube, Aziz Ki na Pacome kwa kikosi cha kwanza.
Wachezaji wa akiba ni Khomein, Mshery, Bakari Mwamnyeto, Jonas Mkude, Duke Abuya, Wilson, Ibrahim, Clatous Chama, Musonda, Baleke na Mzize.
MITAMBO YA KAZI KWA MKAPA

Simba wenyeji hawakuwa wanyonge kwa kuwa mitambo yao ya kazi nayo iliwasili mapema uwanjani kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo huo wakiongozwa na nahodha Mohamed Hussen ambaye anavaa jezi namba 15 mgongoni, Shomari Kapombe, Mussa Camara.
Mitambo ya kazi kwa timu zote mbili mapema iliwasili Uwanja wa Mkapa tayari kwa mchezo huo na walipata muda kuukagua uwanja kabla ya kuanza kusaka pointi tatu ndani ya uwanja.

Miongoni mwa mitambo ya kazi kwa upande wa Yanga ni Maxi Nzengeli ambaye ni kiungo mshambuliaji ikumbukwe kwamba kwenye Ngao ya Jamii walipokutana Uwanja wa Mkapa wakati Simba ikifungwa bao 1-0 ni Nzengeli alifunga bao hilo.
Jean Baleke huyu aliwahi kucheza Simba msimu wa 2023/24 kabla ya kukutana na Thank You, Ladak Bocca mzee wa spidi 120 ndani ya uwanja, Khalid Aucho kiungo mkabaji, Kennedy Musonda ambaye ni mshambuliaji.
Aziz Ki mtaalamu wa mapigo huru ambaye mguu wake wenye nguvu ni ule wa kushoto naye alikuwa ndani ya uwanja, Bakari Mwamnyeto ambaye ni nahodha, Prince Dube na Clement Mzize hawa wote ni washambuliaji na kiungo Mudathir Yahya.
2023/24 MNYAMA ALIPATA TABU KARIAKOO DABI
Rekodi zinaonyesha kuwa msimu wa 2023/24 mnyama Simba mbele ya Yanga inayodhaminiwa na SportPesa alipata tabu kwelikweli kwa kufungwa nje ndani kwenye mechi za ligi walipokutana uwanjani kwenye msako wa pointi tatu muhimu.
Katika dakika 180 utawala ulikuwa kwa Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi ambapo kete zake zilikuwa upande wake kila wakati kwenye kusaka pointi tatu ndani ya uwanja.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Kariakoo Dabi baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 1-5 Yanga pointi tatu na mabao matano yalifungwa kwa Yanga na bao moja kwa Simba hali ilikuwa hivyo.
Mzunguko wa pili mnyama akapasuka tena kwa kushuhudia ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Yanga 2-1 Simba ikawa ni mara ya pili mfululizo kupoteza kwenye Kariakoo Dabi ndani ya msimu wa 2023/24 ambapo iligotea nafasi ya tatu na bingwa alikuwa Yanga alipokomba pointi 80 baada ya kucheza mechi 30.
MVUA YATIBUA HALI YA HEWA KWA MKAPA
Saa chache kabla ya mchezo kuanza Uwanja wa Mkapa ilinyesha mvua kubwa ambayo ilitibua mpangilio wa mambo kuelekea kwenye mchezo huo ambao ni mkubwa Bongo na Afrika.
Wakati mvua inaanza kunyesha ilianza taratibu kwa manyunyu kunyesha kisha mvua kubwa ikanyesha zaidi jambo lililovuruga utaratibu wa mashabiki kuendelea kukata tiketi na kuingia uwanjani.
Hali ya tiketi kwa upande wa VIP C na machungwa ilikuwa bado haijawa vizuri kwa kuwa tiketi bado zilikuwa zinauzwa tofauti na VIP A, VIP B na mzuguko asilimia 100 zote zilikuwa mikononi mwa mashabiki ambao walinunua tiketi zao kushuhudia Kariakoo Dabi.

