UONGOZI wa Simba umebainisha kuwa unyonge sasa basi mbele ya watani zao wa jadi Yanga kuelekea kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Oktoba 19 2024 kwa wababe hao kila mmoja kusaka pointi tatu uwanjani.
Ikumbukwe kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii walipokutana Uwanja wa Mkapa, baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 0-1 Yanga na bao la Yanga likifungwa na Maxi Nzengeli.

Mwisho Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi ilitwaa taji la Ngao ya Jamii kwa ushindi mbele ya Azam FC kwenye mchezo wa fainali. Wababe hawa wanatarajiwa kukutana kwa mara nyingine tena Uwanja wa Mkapa kwenye mchezo wa ligi.
SEMAJI HILI LA SIMBA UNYONGE BASI

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amebainisha kuwa kwa sasa unyonge sasa basi wanakwenda kupambana kupata furaha kwenye mchezo huo ambao utakuwa na ushindani mkubwa.

“Unyonge sasa basi unaona kwamba hatujapata matokeo mazuri kwenye mechi zetu zilizopita dhidi ya wale watani zetu sasa tunakwenda kukutana nao Oktoba 19 2024 hakika tutafanya kazi kubwa kutafuta matokeo na inawezekana.
“Kwa namma ambavyo maandalizi yanaendelea kuelekea mchezo wetu hakika tutafanya kweli. Unajua nyuma mwiko tukimfunga hapo tunapata nguvu ya kutamba, mashabiki hilo wanalijua na inaongeza hali ya kujiamini kwa mechi zetu zinazokuja.
“Shabiki wa Simba hawezi kutamba akimfunga Azam FC, shabiki wa Simba hawezi kutamba akimfunga Kagera Sugar ama Fountain Gate hapana atatamba ikiwa atamfunga nyuma mwiko hivyo tunahitaji pointi tatu na nguvu ya kutamba pia hivyo mashabiki wajitokeze kuwapa nguvu wachezaji tunaamini watafanya balaa.”
UNYONGE DAKIKA 180

Ipo wazi kuwa katika mechi mbili ambazo ni dakika 180 Simba ilifungwa mabao 7 na Yanga ilifungwa mabao mawili pekee uwanjani ambapo ilikuwa imara kwenye eneo la ulinzi ikiongozwa na Bakari Nondo, Dickson Job.
Kwa mwendo ambao ulikuwa kwa Simba mbele ya Yanga kwenye eneo la ulinzi ilikuwa ni wastani wa kuruhusu bao moja kila baada ya dakika 25. Zama hizo Henock Inonga alikuwa chaguo la kwanza eneo la ulinzi kwa sasa amebaki Che Malone.
Ni msimu mpya wa 2024/25 Kariakoo Dabi ipo njiani ambapo kila timu ipo kwenye hesabu ya kuvuna pointi tatu muhimu ndani ya uwanja. Wachezaji na benchi la ufundi hesabu ni kuona furaha inakuwa kwao baada ya dakika 90 na mashabiki furaha yao ni ushindi.
Kikosi cha Simba chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids raia wa Afrika Kusini tayari kwenye ligi ni mechi tano kimeshuka uwanjani ndani ya Ligi Kuu Bara ambazo ni dakika 450 katika msako wa pointi 15 uwanjani kwa timu zote mbili.
Baada ya dakika 450 kugota mwisho kwenye msako wa pointi 15 ni pointi 13 zimekusanywa kibindoni na kuyeyusha pointi mbili. Hii ilitokana na kushinda mechi nne na kuambulia sare kwenye mchezo mmoja wakiwa Uwanja wa KMC, Mwenge.
Katika mechi hizo ushindi ulipatikana kwenye mechi nne ambazo ni dakika 360 sare mchezo mmoja ilikuwa Simba 2-2 Coastal Union uliochezwa Uwanja wa KMC, Mwenge hiyo ilikuwa ni Oktoba 4 2024.
MECHI ZA SIMBA KWENYE LIGI
Simba 3-0 Tabora United mchezo huu ulichezwa Uwanja wa KMC, Mwenge ilikuwa Agosti 18 2024 ni mchezo wa kwanza kwa Simba kwenye ligi na mtupiaji bao la kwanza ni Che Malone ilikuwa dakika ya 14 akitumia pasi ya Jean Ahoua ambaye amekuwa kwenye ubora eneo la kiungo mshambuliaji.
Simba 4-0 Fountain Gate, huu ulikuwa ni mchezo wa pili kwa Simba ulichezwa Uwanja wa KMC, Mwenge ilikuwa Agosti 25 2024. Kwenye mchezo huu Ahoua alitoa pasi mbili za mabao na alifunga bao moja akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo.
Azam FC 0-2 Simba huu ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Simba kucheza ugenini ulichezwa Uwanja wa New Amaan Complex Septemba 26 2024. Nyota Leonel Ateba ambaye ni mshambuliaji alifunga bao lake la kwanza akiwa na uzi wa Simba kwenye ligi na Fabrince Ngoma alifungua akaunti yake ya mabao.
Dodoma Jiji 0-1 Simba ilikuwa Septemba 29 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ni Simba walisepa na pointi tatu kwenye mchezo huu.
Safu ya ushambuliaji ya Simba imefunga mabao 12, na ukuta wa Simba umeruhusu kufungwa mabao mawili ndani ya uwanja ilikuwa kwenye mchezo mmoja wakiwa nyumbani ndani ya msimu wa 2024/25.

