Fadlu DavidsFadlu Davids

KINAWAKA leo Uwanja wa Mkapa ambapo kutakuwa na dakika 90 za moto kati ya Simba na Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara mzunguko wa kwanza ikiwa ni Kariakoo Dabi msimu wa 2024/25.

Ipo wazi kwamba timu zote zinapiga hesabu ya pointi tatu wenyeji ni Simba wataikaribisha Yanga inayodhaminiwa na SportPesa.

MATOKEO YA SIMBA KWENYE LIGI

Fadlu
Fadlu Davids, Kocha Mkuu wa Simba 2024/25. Source: Simba.

Simba 3-0 Tabora United mchezo huu ulichezwa Uwanja wa KMC, Mwenge Agosti 18 2024, Simba 4-0 Fountain Gate, huu ulikuwa ni mchezo wa pili kwa Simba ulichezwa Uwanja wa KMC, Mwenge ilikuwa Agosti 25 2024.

Azam FC 0-2 Simba huu ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Simba kucheza ugenini ulichezwa Uwanja wa New Amaan Complex Septemba 26 2024. Dodoma Jiji 0-1 Simba ilikuwa Septemba 29 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma walisepa na pointi tatu kwenye mchezo huu.

Mchezo wao uliopita ilikuwa Oktoba 4 2024 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa KMC, Mwenge ulisoma Simba 2-2 Coastal Union wakigawana pointi mojamoja.

WAKALI WA PASI ZA MWISHO

JEAN Ahoua
Jean Ahoua kiungo wa Simba mwenye jezi namba 10 mkali wa pasi za mwisho akiwa nazo nne: Source: Simba.

Kwenye kutoa pasi za mwisho ndani ya Simba ni kiungo Jean Ahoua ambaye katoa pasi nne za mabao na kufunga mabao mawili kwenye mechi za ligi ambazo alipata nafasi ya kucheza. Amekomba dakika 381 ndani ya ligi akicheza mechi tano ni nguzo katika eneo la kiungo mshambuliaji.

Ahoua amesema kuwa anatambua mchezo wa Kariakoo Dabi sio mwepesi kulingana na ushindani ulivyo lakini malengo yao ni kuona kwamba wanapata ushindi katika mchezo baada ya dakika 90 kwa kuwa pointi tatu ni muhimu.

“Sio mchezo mwepesi ukizingatia ni Kariakoo Dabi ambacho tunahitaji ni kuona kwamba kwa ushirikiano wetu wachezaji na benchi la ufundi tunapata ushindi ili kupata pointi tatu muhimu. Tunaamini inawezekana na tupo tayari.”

Simba baada ya kucheza mechi tano ni ushindi kwenye mechi nne na sare mchezo mmoja. Safu ya ushambuliaji imefunga jumla ya mabao 12 na kukusanya jumla ya pointi 13 kibindoni.

AZIZ KI

Aziz KI
Aziz Ki kiungo wa Yanga menye pasi tatu za mabao ndani ya ligi 2024/25. Source: Yanga.

Kutoka Jangwani Aziz Ki ni namba moja katika watengeneza pasi za mwisho kwa wachezaji wa Yanga akiwa katoa pasi tatu na kufunga bao moja. Ni dakika 322 amecheza na kuhusika katika mabao manne yaliyofungwa na Yanga.

Yanga baada ya kucheza mechi nne ni mabao 8 safu ya ushambuliaji imefunga na kukusanya pointi 12 kibindoni baada ya kushinda mechi zake zote ilizocheza kwa msimu wa 2024/25.

NENO LA FADLU

Fadlu Davids, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa ugumu upo kwenye Kariakoo Dabi lakini wanatambua namna bora itakayowapa matokeo licha ya kuwa wachezaji wengi ni wageni kwenye Kariakoo Dabi.

“Mchezo muhimu kwetu kupata matokeo na ukizingatia tunakutana na timu kubwa, tunahitaji kutawala mchezo ili kupata matokeo wachezaji wapo tayari licha ya kwamba wengi ni wageni.”

MECHI ZA YANGA

Gamondi
MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga 2024/25. Source: Yanga.

Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi baada ya kucheza mechi nne ambazo ni dakika 360 imekomba ushindi mechi zote nne za Ligi Kuu Bara. Pointi 12 zipo kibindoni. Safu ya ushambuliaji ya Yanga imefunga mabao 8 na ukuta haujaruhusu kufungwa ndani ya uwanja katika mechi za ushindani.
Kinara wa utupiaji ni kiungo Maxi Nzengeli ambaye yeye katupia jumla ya mabao matatu kwenye mechi nne ambazo Yanga imecheza ndani ya uwanja kwenye msako wa ushindi.

HAYA HAPA MATOKEO YA YANGA
Kagera Sugar 0-2 Yanga mchezo huu ulichezwa Uwanja wa Kaitaba, Agosti 29 2024 na mtupiaji wa bao la kwanza ni Maxi Nzengeli ndani ya Yanga kwenye ligi.

Ken Gold 0-1 Yanga huu ulikuwa mchezo wa pili kwa Yanga ugenini ilikuwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya mtupiaji alikuwa ni Ibrahim Bacca ambaye alitumia pasi ya Aziz Ki Septemba 25 2024.

Yanga 1-0 KMC, mchezo wa kwanza wakiwa Uwanja wa Azam Complex msimu wa 2024/25 ilikuwa Septemba 29 2024. Yanga 4-0 Pamba Jiji ushindi mkubwa kwa Yanga ndani ya 2024/25 walikuwa Azam Complex  ilikuwa Oktoba 3 2024.

NENO LA GAMONDI

Miguel Gamondi, kocha wa Yanga amesema kuwa wanatambua umuhimu wa mchezo wa leo huku historia ikifutwa kwa kuwa yaliyopita hayawezi kujirudia kwa wakati mwingine ndani ya uwanja.

“Tunatambua utakuwa mchezo wenye ushindani mkubwa ukizingatia kwamba ni Kariakoo Dabi, wapo wachezaji muhimu ambao tutawakosa lakini hilo siwezi kulisema kwa sasa tutafahamu namna tutakavyowakabili wapinzani wetu.

“Matokeo yaliyopita huwezi kubadili hatuchezi kwa historia tunaangalia yaliyopo mbele yetu kila mchezaji anatambua umuhimu wa mchezo hivyo tutaingia uwanjani kwa tahadhari ili kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wetu.”

Share this: