Usiku wa deni haukawii kukucha ndivyo unavyoweza kusema, ambapo leo Jumatano saa moja usiku kikosi cha Simba kinatarajiwa kushuka katika Uwanja wa Suez nchini Misri kuikabili Al Masry katika mchezo wa robo fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku Simba wakitamba wanataka kulipa Kisasi.
Kumbuka unaweza kujishindia mamilioni kwa kubashiri matokeo ya mchezo huu na mingine kwa kuweka ubashiri wako kupitia kampuni bora ya michezo ya kubashiri ya SportPesa. Tembelea sasa www.sportpesa.co.tz

Huu unatarajiwa kuwa moja ya mechi ngumu ambayo inatarajia kuchezwa usiku wa leo hasa kutokana na historia ya timu zote mbili, ambapo kwa upande wa Al Masry wamekuwa na wakati mzuri wa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani, huku Simba wao wakitamba kujipanga kuhakikisha wanapata matokeo chanya dhidi yao.
Kocha wa Simba, Fadlu Davis ameweka wazi kuwa wataingia katika mchezo wa leo kwa nidhamu kubwa hasa katika ulinzi huku wachezaji wakisisitizwa kutumia vema nafasi zinazopatikana ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu nusu fainali.
ALICHOSEMA KOCHA SIMBA

Kocha, Fadlu ameweka wazi kuwa wachezaji wake wameandaliwa kimwili na kiakili kuhakikisha wanacheza bila presha ili kufanikisha malengo waliyojiwekea, licha ya kukiri kuwa utakuwa mchezo mgumu lakini wamejiandaa kufanya vizuri.
Fadlu ameongeza kuwa anajua mechi ya pili itakayopigwa jijini Dar es Salaam ndio itaamua nani wa kufuzu nusu fainali, lakini mipango yao ni kuhakikisha wanafanya vizuri leo ili kuweka mazingira rafiki kwa mchezo ujao.
“Itakuwa mechi ngumu, lakini tumejiandaa vizuri. Kikosi chetu kimepata muda mzuri wa maandalizi na tumefanya mazoezi hapa Misri kwa siku nne na tupo tayari kwa mchezo.
“Maandalizi yote yamekamilika na kikosi kipo kwenye hali nzuri. Tunatarajia mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa uzoefu wa wapinzani, lakini tumewaandaa wachezaji vyakutosha kuhakikisha tunapata matokeo chanya.
“Al Masry wana kocha mpya na wana kikosi imara ambacho kinaweza kuleta ushindani mkubwa dhidi ya timu yoyote.”
MUKWALA NAYE ACHIMBA MKWARA

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mshambuliaji wa Simba, Steven Mukwala amesema wapo tayari kuhakikisha wanapigania nembo ya klabu yao na kurejea nchini kifua mbele .
“Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari kuhakikisha tunapambana kwa dakika zote 90 ili kuwapa furaha Wanasimba wote ambao tunaamini watakuwa nyuma yetu, kama ambavyo kocha amesema utakuwa mchezo mgumu lakini tunaamini katika kile ambacho makocha wetu wametuelekeza na tupo tayari kwa ajili ya vita hii.”
SIMBA: “TUMEDHAMIRIA KUVUKA NUSU FAINALI MSIMU HUU.”
Kuelekea mchezo huo Simba wameweka wazi kuwa mara baada ya kushindwa kuvuka hatua ya Robo Fainali tano katika misimu iliyopita, msimu huu wamedhamiria kufuzu Nusu Fainali.
“Hii ni robo fainali ya sita kwetu kwenye michuano ya Afrika (Klabu Bingwa na Kombe la Shirikisho), katika kipindi cha miaka saba iliyopita lakini hatukuweza kuvuka, lakini kutokana na ubora na aina ya wachezaji tulionao sasa tunaamini safari hii tunavuka na kutinga nusu fainali.
NI MECHI YA KISASI

Hii sio mara ya kwanza kwa Simba na Al masry kukutana katika mashindano ya kimataifa kwani Machi 7/2018 walikutana na katika mchezo wa hatua ya awali uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao uliisha kwa sare ya kufungana mabao 2-2, huku katika mchezo wa marudiano uliopigwa Machi 17/2018 ulimalizika kwa matokeo ya suluhu na Simba kutupwa nje ya mashindano.
MIPANGO IMEKAMILIKA
Katika kuhakikisha timu inakuwa kwenye mazingira mazuri ya kutimiza malengo yao, Simba ilitanguliza baadhi ya viongozi muhimu kwa ajili ya kuandaa mazingira mazuri kwa timu kufikia ikiongozwa na Mratibu wa timu, Abbas Ally ambaye pia amesema maandalizi ya timu nchini Misri kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry yamekamilika.
Abbas amesema aliandaa mazingira ya timu kufanya mazoezi katika mji wa Ismailia kabla ya kuondoka siku moja kabla ya mchezo kuelekea Suez ambapo kutapigwa mechi yenyewe.
Simba ilikuwa ikifanya mazoezi usiku huko Ismailia ambapo kikosi chao kilikuwa kimefikia katika viwanja vya Hoteli waliyokuwa wamefikia ya Tolip Hotel Resort ambapo wachezaji wote walishiriki.
Ikumbukwe nyota sita waliokuwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania waliocheza dhidi ya Morocco siku ya Jumatano ndio wwalikuwa wakwanza kufika Misri na wameshiriki mazoezi hayo kikamilifu.
Simba ililazimika kufanya mazoezi muda huo kwa ajili ya kuhakikisha wanaendelea kuzoea mazingira ya hali ya hewa.

