Mastaa wa Simba kambiniMastaa wa Simba kambini

SIMBA WARUDI KAMBINI RASMI KUIWINDA YANGA

Zikiwa zimesalia siku 11 tu, kuuelekea mchezo mkubwa wa Kariakoo Dabi ambao unatarajiwa kupigwa siku ya Jumamosi ya Taerehe 19 mwaka huu, wenyeji wa mchezo huo Simba rasmi wamerejea kambini kuanza maandalizi ya kikosi chao.

Tayari sehemu kubwa ya wachezaji wa Simba ambao hawajaitwa kujiunga na timu zao za Taifa kwa ajili ya maandalizi ya michezo iliyo kwenye ratiba ya michuano ya kufuzu mashindano ya AFCON wameripoti kambini Jumanne wiki hii.

Simba wanauendea mchezo huo wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kuangusha pointi mbili kwenye mchezo wao uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union, mara baada ya matokeo ya mwisho ya sare ya mabao 2-2.

Sare hiyo na Wagosi wa Kaya ambayo pia ilishuhudia mlinda mlango wa Simba, Moussa Camara akiruhusu nyavu zake zitikiswe kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu imewafanya Simba kufikisha pointi 13 baada ya kucheza mechi 5.

SIMBA
Baadhi ya mastaa wa wakiendelea na mazoezi

HALI YA MSIMAMO

Mpaka sasa Simba wanakamatia nafasi ya pili wakiwa wamekusanya pointi 13 baada ya michezo mitano, huku watani zao wa jadi Yanga wao wakiwa wanakamatia nafasi ya nne baada ya kukusanya pointi 12 katika michezo yao minne ambayo wamecheza mpaka sasa.

Licha ya tofauti ya mchezo mmoja ambao timu hizo zimepishana kwa msimu huu namba za Simba zimeonekana kuwa bora kuliko watani zao wa Jadi ambapo licha ya tofauti ya pointi mojqa kati yao lakini pia Simba wana faida ya mabao 2 kwenye utofauti wa mabao yakufunga na kufungwa kulinganisha na mpinzani wao.

SIMBA
Msimamo wa ligi

YANGA WABABE REKODI DABI MSIMU WA 2023/24

Ikumbukwe msimu wa 2023/24 Yanga wanaodhaminiwa na Kampuni bora ya michezo ya kubashiri ya SportPesa walifanikiwa  kubeba pointi zote sita.

Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Novemba 5, 2023 baada ya dakika 90 ubao wa matokeo uwanjani ulisoma Yanga wakiwakanda Wanasimba 5-1 Yanga, huku mchezo wa mzunguko wa pili uliopigwa Aprili 20, 2024 Yanga wakifanikiwa kushinda 2-1.

SIMBA
Baadhi ya matukio ya Kariakoo Dabi

MSIMU HUU UMEANZAJE?

Yanga imeendelea kuendeleza utemi wa Kariakoo Dabi kwa msimu huu wa 2024/25 ambapo kwenye mchezo wa mashindano ya Ngao ya Jamii ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa, Benjamin Mkapa Yanga  walifanikiwa kushinda bao 1-0.

Matokeo hayo yamewafanya Simba kupoteza michezo mitatu mfululizo dhidi ya Yanga katika siku za hivi karibuni hali ambayo inaongeza joto la mchezo huu kwani Simba wanautaka mchezo na Yanga wameweka wazi mipango ya kufanya makubwa.

NYENDO ZAO KWENYE LIGI

Kikosi cha Simba chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids raia wa Afrika Kusini wakishuka uwanjani kwao huu unakuwa mchezo wa tano kumeshuka uwanjani ndani ya Ligi Kuu Bara ambazo ni sawa na dakika 450, na katika vita ya kusaka pointi 15 uwanjani wamefanikiwa kuvuna pointi 13 na kupoteza pointi mbili huku wapinzani wao Yanga wakiwa na asilimia 100 ya ushindi katika michezo yao minne ya kwanza.

Mechi walizoshinda Wanasimba mpaka sasa  ni kama ifuatavyo;

Simba 3-0 Tabora United ambapo mchezo huu ulichezwa Uwanja wa KMC, Mwenge Agosti 18, mwaka huu ukiwa ndio mchezo wa kwanza kwao kwenye ligi Kuu Bara ambapo wafungaji walikuwa Che Malone dakika ya 14 ya mchezo ambapo alitumia pasi ya Jean Charles Ahoua.

Kwenye mchezo dhidi ya Fountain Gate, wenyeji wakaibuka na ushindi wa mabao 4-0 huu ulikuwa ni mchezo wa pili kwao uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge siku ya Agosti 25, 2024.

Azam FC 0-2 Simba huu ulikuwa mchezo wa kwanza kwao kucheza ugenini ambapo ulichezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar Septemba 26, 2024, kabla ya kuwaua Dodoma Jiji 1-0 ugenini Septemba 29, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma walisepa na pointi tatu kwenye mchezo huu.

 

ATEBA, AHOUA WAITEKA SHOO NAMBA ZA MABAO

SIMBA
Jean Charles Ahoua

Safu ya ushambuliaji ya Wanasimba imeanza kwa kasi ambapo mpaka sasa imefanikiwa kufunga mabao 12, huku mastaa straika, Leonel Ateba na kiungo Jean Ahoua, Valentino Mashaka wakitamba ambapo wote wametupia mabao mawili, huku ukuta wao ukiwa umeruhusu mabao 2 tu, hivyo kuashiria mwanzo bora wa msimu.

MPANZU NAYE YUMO NDANI YA NYUMBA

Mara baada ya kutangazwa kukamilika kwa usajili wake kiungo mshambuliaji, Elie Mpanzu ni miongoni mwa wale ambao wameshiriki mazoezi hayo ili kujiweka sawa kwenye utimamu wa mwiuli kwa ajili ya majukumu yake mapya.

 

 

 

Share this:

By Joel Thomas

Joel Thomas is a Tanzanian sports writer with a BSc (Education) from Mwenge Catholic University. He spent 4 years at Global Publishers and is in his second year with SportPesa, covering football and betting education for local fans. Anapenda soka na anaandika kwa uwajibikaji.