SEPTEMBA to remember wanasema hivyo na kuna mengi ambayo yalitokea kwenye ulimwengu wa mpira kitaifa na kimataifa huku wakiwepo waliocheka kwa kukomba mkwanja mrefu kutoka SportPesa. Asante Septemba na karibu Oktoba ambapo kuna dakika 270 moto vigongo vikali vinatarajiwa kuchezwa na Kariakoo Dabi ndani.
Ipo wazi kwamba ndani ya Septemba mechi kali zilichezwa huku Simba na Yanga inayodhaminiwa na SportPesa katika anga la kimataifa wakitinga hatua ya makundi kwenye mashindano ambayo wanashiriki.

Simba ni kwenye Kombe la Shirikisho ilipata ushindi wa jumla ya mabao 3-1 Al Ahli Tripoli ilikuwa ni Septemba 22 ambapo mabao ya Simba yalifungwa na Leonal Ateba, Edwin Balua na Kibu Dennis ilikuwa Uwanja wa Mkapa.
Baada ya Simba kupata ushindi kimataifa walicheza mchezo wa Mzizima Dabi ilikuwa Uwanja wa New Amaan Complex baada ya dakika 90 ubao ulisoma Azam FC 0-2 Simba mabao yakifungwa ya Leonal Ateba, Fabrince Ngoma wakakomba pointi tatu mazima.
Katika mechi 11 za hivi karibuni kwenye Mzizima Dabi rekodi zinaonyesha kuwa Simba umepata ushindi mara 5, sare mara 5 huku Azam FC wakipata ushindi mara moja katika mechi za ligi.
Funga kazi ya Septemba ilikuwa dhidi ya Dodoma Jiji walipokomba pointi tatu na sasa wana kazi kubwa kupambania pointi tatu ambazo wapinzani wao nao wanazitaka ndani ya Oktoba kukiwa na mechi tatu ambazo ni dakika 270.
Yanga wao walicheza mchezo wao wa kuwania kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa dhidi ya CBE FA walipopata ushindi wa mabao 6-0 na kutinga hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla mabao 7-0.
HIZI HAPA KETE ZA YANGA OKTOBA

Kete za Oktoba kwa Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi wakiwa ni mabingwa watetezi mbili watakuwa nyumbani na moja watakuwa ugenini itakuwa ni Kariakoo Dabi, Uwanja wa Mkapa dhidi ya Simba.
Oktoba 3 2024: Yanga v Pamba Jiji, saa 12:30 jioni, Uwanja wa Azam Complex ikumbukwe kwamba Pamba imepanda ligi ikitokea Championship.
Oktoba 19 2024: Simba v Yanga saa 11:00 jioni huu utakuwa mchezo wa Kariakoo Dabi mzunguko wa kwanza kwa wababe hawa kukutana uwanjani.
Yanga v JKT Tanzania, saa 1:00 usiku, Uwanja wa Azam Complex. Msimu wa 2023/24 JKT Tanzania ilipokutana na Yanga Uwanja wa Azam Complex ilipoteza kwa kufungwa mabao 5-0.
OKTOBA KWA MNYAMA SIMBA

Funga kazi yao kwenye ligi ilikuwa dhidi ya Dodoma Jiji kwenye mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa na mwisho Simba iliambulia ushindi katika mchezo huo wakiwa ugenini.
Katika mchezo huo baada ya dakika 90 ubao ulisoma Dodoma Jiji 0-1 Simba na bao la ushindi likifungwa na Jean Ahoua kwa mkwaju wa penalti baada ya Zimbwe Jr kufanyiwa faulo ndani ya 18.
Simba ndani ya Oktoba mechi mbili itakuwa nyumbani na mechi moja itakwea pipa na kuibukia Mbeya kwenye msako wa point tatu muhimu.
Simba v Coastal Union inatarajiwa kuchezwa Oktoba 4 2024, Uwanja wa KMC, Mwenge saa 10:15 jioni.
Simba v Yanga itakuwa Oktoba 19 2024, Uwanja wa Mkapa saa 11:00 jioni, Kariakoo Dabi ambapo Simba itakuwa nyumbani kwenye mchezo huu inakumbuka kwamba msimu wa 2023/24 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza ilipoteza kwa kufungwa mabao 5-1.
Tanzania Prisons v Simba, Oktoba 22 2024, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
MATAJIRI AZAM FC

Matajiri Azam FC watakuwa kazini ndani ya Oktoba kwenye mechi tatu kusaka ushindi ndani ya dakika 270 za kazikazi kwa kila mchezaji kutimiza majukumu yake uwanjani.
Ikumbukwe kwamba Mzizima Dabi ya Azam FC v Simba mzunguko wa kwanza ulikamilika kwa ubao wa Uwanja wa New Amaan Complex kusoma Azam FC 0-2 Simba.
Oktoba 3 2024 : Namungo v Azam FC itachezwa saa 3:00 usiku, Uwanja wa Majaliwa. Oktoba 18 2024: Prisons v Azam FC, Uwanja wa Sokoine, saa 10:00 jioni. Azam FC v Ken Gold, saa 1:00 usiku itakuwa Oktoba 29 2024, Azam Complex.
Matajiri Azam FC mechi mbili ambazo ni dakika 180 watakuwa ugenini na mchezo mmoja watakuwa kwenye ngome yao kongwe pale Uwanja wa Azam Complex.

