KIMATAIFA baada ya wawakilishi wa Tanzania kutambua wapinzani wao katika hatua za makundi kwenye mashindano hayo makubwa 2024/25 tambo zimetawala kwa timu zote mbili zikibainisha kwamba zipo tayari kufanya kweli nje ndani kwenye mechi zao ambazo zipo kwenye ratiba.
Ipo wazi kwamba Oktoba 7 2024 ilichezwa droo ya kupanga makundi kwa timu shiriki katika mashindano ya kimataifa yalifanyika nchini Misri na dunia nzima ilikuwa ikifuatilia droo hiyo ambayo ilirushwa mubashara kupitia YouTube ya CAF.

Yanga inayodhaminiwa na kampuni ya SportPesa katika anga la kimataifa ipo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na imetinga hatua ya makundi huku ikiwa na kikosi kilichofanyiwa maboresho zaidi.
Timu mbili zilikuwa kwenye anga la kimataifa katika Ligi ya Mabingwa Afrika Yanga na Azam FC. Bahati haikuwa nzuri kwa Azam FC iligotea kwenye hatua za awali hivyo mpaka wakati ujao tena ikiwa itapata nafasi kwa mara nyingine.
SEMAJI LA YANGA KUHUSU KIMATAIFA
Yanga ambayo imepangwa Kundi A kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika imebainisha kuwa mpango mkubwa ni kupata matokeo mazuri kwenye mechi zote watakazocheza nyumbani na ugenini kutokana na ubora wa kikosi walichonacho.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa wanatambua umuhimu wa mechi zote ambazo watacheza kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika jambo ambalo linawafanya wawe kwenye maandalizi mazuri hasa baada ya droo kupangwa.
“Tunaanza na Al Hilal hawa wameingia kwenye mfumo hivyo ambacho tunakwenda kufanya ni kusaka pointi tatu muhimu tukiwa nyumbani, mashabiki jambo letu ni moja kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Mkapa.
“Kikubwa mchezo wa nyumbani ambao ni wa ufunguzi ni muhimu kwetu kupata matokeo, tuliona walicheza hivi karibuni hapa wakapata sare sasa sisi tunawakaribisha waje Uwanja wa Mkapa tucheze nao watajua kwamba hii ni Yanga.
“Benchi la ufundi linatambua umuhimu wa mchezo wetu na maandalizi yake yatafanyika kwa umakini mkubwa, tunawachezaji wazuri na wenye uwezo hilo lipo wazi wanazimudu hizi mechi kubwa na za ushindani kikubwa ni utayari na mashabiki kuwa bega kwa bega nasi.”
HII HAPA RATIBA YA YANGA KIMATAIFA
26/11/2024: Yanga vs Al Hilal
06/12/2024: MC Alger vs Yanga
13/12/2024: TP Mazembe vs Yanga
03/01/2025: Yanga vs TP Mazembe
10/01/2025: Al Hilal vs Yanga
17/01/2025: Yanga vs MC Alger
HAWA HAPA SIMBA

Timu ya Simba chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids ina kibarua kwenye anga la kimataifa katika Kombe la Shirikisho kiwa imepangwa Kundi A kwenye kusaka ushindi ndani ya uwanja ili kufikia malengo ya kutinga hatua ya robo fainali.
Ipo wazi kwamba msimu wa 2023/24 Simba ilikuwa inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na iligotea hatua ya robo fainali msimu wa 2024/25 ipo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa imetinga hatua ya makundi.
Sababu ya Simba kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika ni nafasi ya tatu iliyogotea katika msimu uliopita na Azam FC ikawa nafasi ya pili hivyo ilipeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
SEMAJI LA SIMBA HILI HAPA

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema uimara walionao unawapa nguvu ya kuamini kwamba watapata matokeo mazuri kwenye mechi za kimataifa na pointi za nyumbani ni muhimu kuzibeba zote baada ya dakika 90.
“Wale wapinzani wetu ambao tunaanzia nao nyumbani tunaamini wapo imara lakini wanapaswa kukutana na ule ubaya ubwela wenyewe ili kupeleka salamu kwa wengine kwamba hii timu haina utani kwenye mashindano ya kimataifa.
“Wachezaji wetu wanatambua umuhimu wa kupata ushindi kwenye mechi za kimataifa hilo lipo wazi hivyo ni suala la muda kufika na kutimiza majukumu yao uwanjani. Mashabiki ni muda wa kujitokeza kwa wingi uwanjani kushangilia timu yao pendwa.
“Kwenye suala la pointi tisa hizi katika mechi tatu za nyumbani halina mjadala tunazitaka na tunazichukua kisha huko ugenini tunakwenda kupambana kuona kipi ambacho tutavuna lakini lazima tushinde mechi zetu.”
RATIBA YA SIMBA HII HAPA
28/11/2024: Simba vs Bravos.
08/12/2024: Costantine vs Simba.
15/12/2024: Simba vs Sfaxien.
05/01/2025: Sfaxien vs Simba.
12/01/2025: Bravos vs Simba.
19/01/2025: Simba vs Costantine.

