BAADA ya Simba kuangusha pointi mbili kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union kigongo kinachofuata kwa Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids ni Oktoba 19 2024 Kariakoo Dabi mchezo unaosubiriwa kwa shauku kubwa na wapenda mpira duniani.
Ikumbukwe kwamba kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union uliochezwa Uwanja wa KMC, Mwenge Complex Oktoba 4 2024 ubao ulisoma Simba 2-2 Coastal Union huku Mussa Camara akionja joto yakutunguliwa kwa mara ya kwanza akiwa langoni walipogawana pointi mojamoja. Simba inafikisha pointi 13 baada ya kucheza mechi 5.

HAWA HAPA WATUPIAJI
Kwa Simba Mohamed Hussen ambaye ni nahodha alianza kutupia bao la kuongoza dakika ya 26 akiwa ndani ya 18 likiwa ni bao la kwanza kwa nahodha na bao la pili lilifungwa na Leonel Ateba kwa mkwaju wa penalti.
Ateba mshambuliaji wa Simba anafikisha mabao mawili kwenye ligi alianza kufunga kwenye Mzizima Dabi mchezo uliochezwa Uwanja wa New Amaan Complex na bao la pili kawatungua Coastal Union ya Tanga.
Coastal Union walijibu mapigo kipindi cha pili kwa kufunga kupitia kwa Hassan Abdallah ilikuwa dakika ya 48 na Hernest Malongo dakika ya 71 na watupiaji wote walifunga wakiwa nje ya 18 wakimpa tabu kipa wa Simba Camara kwa mara ya kwanza ndani ya ligi.
DABI YA 2023/24 MBABE HUYU

Ikumbukwe kwamba msimu wa 2023/24 haukuwa bora kwa Simba nje ndani katika msako wa pointi sita ilipoteza pointi zote na Yanga ilikuwa imara kwenye hili kwa kukomba pointi zote sita mazima ndani ya uwanja. Ipo wazi kwamba Yanga inadhaminiwa na SportPesa.
Kumbuka kwamba kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza ilikuwa Novemba 5 2023 baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 1-5 Yanga na mchezo wa mzunguko wa pili Aprili 20 2024 ilikuwa Yanga 2-1 Simba.
Mchezo wa kwanza bao pekee la Simba lilifungwa na Kibu Dennis mkandaji ambaye kwenye mchezo huo alitumia pasi ya Saido Ntibanzokiza na alikwama kusepa na dakika 90 mkandaji baada ya kupata maumvu na mchezo wa pili bao la Simba lilifungwa na Michael Fred, fungafunga ambaye amepewa mkono wa Thank You ndani ya Simba.
Kwenye mechi mbili ambazo ni dakika 180 Simba ilifungwa mabao 7 na Yanga ilifungwa mabao mawili. Ni wastani wa bao moja kila baada ya dakika 25 Simba ilikuwa ikifungwa ndani ya uwanja.
2024/25 IMEANZA

Ni msimu mwingine tena wa 2024/25 Kariakoo Dabi inanukia ambapo kila timu ipo kwenye hesabu ya kuvuna pointi tatu muhimu ndani ya uwanja huku wapanga ramani wakisoma mchezo mzima na tayari kuna kete ambazo wamezicheza ndani ya ligi.
Kikosi cha Simba chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids raia wa Afrika Kusini ni mechi tano kimeshuka uwanjani ndani ya Ligi Kuu Bara ambazo ni dakika 450 kwenye msako wa pointi 15 uwanjani kikisepa na pointi 13 na kuyeyusha pointi mbili.
Katika mechi hizo ushindi ulipatikana kwenye mechi nne ambazo ni dakika 360 sare mchezo mmoja ilikuwa Simba 2-2 Coastal Union uliochezwa Uwanja wa KMC, Mwenge ilikuwa ni Oktoba 4 2024.
HIZI HAPA ZA USHINDI

Simba 3-0 Tabora United mchezo huu ulichezwa Uwanja wa KMC, Mwenge ilikuwa Agosti 18 2024 ni mchezo wa kwanza kwa Simba kwenye ligi na mtupiaji bao la kwanza ni Che Malone ilikuwa dakika ya 14 akitumia pasi ya Jean Ahoua.
Simba 4-0 Fountain Gate, huu ulikuwa ni mchezo wa pili kwa Simba ulichezwa Uwanja wa KMC, Mwenge ilikuwa Agosti 25 2024. Azam FC 0-2 Simba huu ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Simba kucheza ugenini ulichezwa Uwanja wa New Amaan Complex Septemba 26 2024.
Dodoma Jiji 0-1 Simba ilikuwa Septemba 29 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma walisepa na pointi tatu kwenye mchezo huu.
SAFU YA UTUPIAJI SIMBA
Safu ya ushambuliaji ya Simba imefunga mabao 12, Leonel Ateba, Jean Ahoua, Valentino Mashaka hawa wote wametupia mabao mawilimawili na ukuta umeruhusu mabao 2.
Katika mechi nne ukuta wa Simba hakuruhusu mabao ya kufungwa mpaka mchezo wan ne uliochezwa Uwanja wa KMC Mwenge walipogawana pointi mojamoja na Wagosi wa Kaya.

