Bacca SalutiBacca Saluti

MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa waliamua kubadilisha mbinu mbele ya wapinzani wao Pamba Jiji kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara malengo ikiwa ni kupata pointi tatu muhimu katika mchezo wao baada ya dakika 90.

Kweye mechi tatu ambazo ni dakika 270 safu ya ushambuliaji ya Yanga inayodhaminiwa na SportPesa  ilifunga mabao manne na ukuta wa timu hiyo chini ya Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Dickson Job haujaruhusu bao la kufungwa. Yanga wamevunja rekodi ya ushindi wa mabao mawili 2024/25 na kushinda mabao 4 huku kituo kinachofuata ikiwa ni Kariakoo Dabi dhidi ya Simba, Oktoba 19 2024.

Aziz Ki
Aziz Ki kiungo wa Yanga dhidi ya Pamba Jiji. Source: Yanga.

Ipo wazi kuwa kwa msimu wa 2023/24 Yanga ilikuwa ni namba moja kwa timu ambazo zilifungwa mabao machache ambayo ni 14 baada ya timu hiyo kucheza mechi 30 na ilikamilisha msimu ikiwa na pointi 80 kibindoni.

Baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Pamba Jiji kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Gamondi ameweka wazi kuwa haikuwa rahisi kupata ushindi kwenye mchezo huo kutokana na mfumo uliotumika na mwisho wakapata ushindi.

“Haikuwa rahisi kupata ushindi mbele ya wapinzani wetu Pamba Jiji kwani tulibadilisha mfumo tofauti na ule ambao ulikuwa umezoeleka kwenye mechi zilizopita. Kuanza na washambuliaji wawili unaona imeongeza presha kwa wapinzani wetu.

“Jean Baleke alipata nafasi ya kuanza kwenye eneo la ushambuliaji na Clement Mzize hii ilikuwa ni muhimu kwetu kupata ushindi na pongezi kwa wachezaji namna ambavyo walipambana kutafuta ushindi na mwisho matokeo yamepatikana.”

HIKI HAPA KIKOSI KAZI CHA GAMONDI

Diarra
Diarra Djigui mechi nne ameanza langoni kwenye ligi 2024/25. Source: Yanga.

Djigui Diarra ambaye ni kipa yeye mechi zote nne ameanza langoni na hajafungwa bao msimu wa 2024/25, Ladack Bocca, Dickson Job, Bacca, Bakari Mwamnyeto, Sure Boy, Abuya Duke, Jean Baleke, Aziz Ki, Clement Mzize.

WAVUNJA REKODI

Maxi Nzengeli
Kiungo wa Yanga Maxi Nzengeli ametupia mabao 3 ndani ya ligi 2024/25. Source: Yanga.

Kwenye mechi za mwanzo tatu Yanga ilikuwa na rekodi ya kugotea kufunga mabao mawili ila mbele ya Pamba Jiji wamevunja rekodi hiyo na kuandika rekodi mpya ya ushindi wa mabao zaidi ya matatu ndani ya ligi. Baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Azam Complex ni Yanga 4-0 Pamba Jiji na ushindi wa kwanza Yanga ilipata mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Mabao kwa Yanga yamefungwa na Bacca dk 4, Aziz Ki dk 45 penalti, Maxi Nzengeli dk 54, Kennedy Musonda dk 84. Kwenye mchezo huo Pamba Jiji mchezaji wao mmoja alionyeshwa kadi nyekundu ni Saleh Masoud ni baada ya kuonyesha kadi mbili za njano.

Ikumbukwe kwamba msimu wa 2023/24 chini ya Gamondi ilisepa na pointi sita mazima kwenye mechi mbili za mwanzo huku safu ya ushambuliaji ikifunga jumla ya mabao 10 ikiandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza kwenye msimu kufunga mabao mengi uwanjani kwenye mechi za ligi.

WANAFUKUZIA REKODI ZA 2023/24

Dickson Job
Mfungaji wa bao la kwanza Yanga 2023/24 Dickson Job. Source: Yanga.

Mabingwa hao watetezi wanafukuzia rekodi yao ya msimu wa 2023/24 ambapo kwenye mechi za mwanzo ilikuwa:- Yanga 5-0 KMC mchezo huu ulichezwa Uwanja wa Azam Complex ulikuwa wa kwanza kwa Yanga ndani ya msimu ambapo mfungaji wa bao la kwanza alikuwa beki Dickson Job.

Kwenye mchezo huu Yanga ilifungua pazia la safari kuufuata ubingwa na iliendelea na mwendo huo kwa kuhitimisha msimu ikiwa na jumla ya pointi 80 kibindoni baada ya kucheza jumla ya mechi 30. Huu ulichezwa Agosti 23 2023.

Kete ya pili ilikuwa Yanga 5-0 JKT palepale Uwanja wa Azam Complex Yanga ilikomba pointi tatu mazima na kichapo cha 5G kiliendelea kwa wapinzani wao. Ndani ya dakika 180 safu ya ushambuliaji ya Yanga ilifunga mabao 10 na safu ya ulinzi haikuruhusu kufungwa kwenye mechi zake zote mbili ambazo ilianzia ikiwa nyumbani.

NENO LA SEMAJI ALI KAMWE

Kamwe
Kamwe Ally, Ofisa Habari wa Yanga. Source: Yanga.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe ameweka wazi kuwa wanatambua kwamba mashabiki wa Yanga wanapenda kuona timu hiyo inafunga mabao  mengi hilo wachezaji wanalitambua na wanalifanyia kazi kwa ukaribu kabisa.

“Unajua mashabiki wa Yanga wanatambua namna ambavyo timu yao inacheza na uwezo wake wa kufunga mabao mengi uwanjani hivyo pale wanapofunga mabao machache huwa wanaamini kwamba hapo sio kwenye hatua ya Yanga.

“Kazi inaendelea na benchi la ufundi linafanyia kazi makosa ambayo yamepita kwenye mechi zetu tunaamini kwamba furaha inakuja na watafurahi sana mashabiki kupata burudani bado kikosi kinasukwa.”

Share this: