Jean Charles AhouaJean Charles Ahoua

 

Wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Kikosi cha Simba kimewasili salama jijini Dar es Salaam kutokea Tunisia walipokuwa na majukumu ya mchezo wa mkondo wa nne wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi dhidi ya CS Sfaxien ambao Simba walifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

SIMBA
Mastaa Simba wakishangilia ushindi Tunisia

Katika mchezo huo ambao ulipigwa juzi siku ya Jumapili, Simba wakiwa ugenini walifanikiwa kuichapa Sfaxien bao 1-0 lililofungwa na kiungo wao wa kimataifa wa Ivory Coast, Jean Charles Ahoua. Kikosi hicho kiliondoka nchini Tunisia jana asubuhi  kupitia Uturuki kilipounganisha ndege hadi jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuwasili uongozi wa Simba umetangaza kuwa timu itaanza mara moja maandalizi ya mchezo unaofuata wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos Do Marquis ya Angola unaotarajiwa kupigwa Januari 12. Ikumbukwe mchezo dhidi ya Bravos utapigwa katika Uwanja wa Novemba 11 nchini Angola saa moja usiku kwa saa za Tanzania.

MCHEZO ULIKUWAJE TUNISIA?

SIMBA
Lionel Ateba akipambana na mlinzi wa Sfaxien

Katika mchezo huo wa ushindi wa bao moja dhidi ya CS Sfaxien ambao ulipigwa Uwanja wa Hammadi Agrebi nchini Tunisia, wenyeji Sfaxien walianza kwa kasi dakika 20 za mwanzo kwa kufanya mashambulizi ya haraka lakini Simba walikuwa imara kuwadhibiti.

Jean Charles Ahoua aliipatia bao hilo pekee dakika ya 34 kwa shuti kali akiwa ndani ya 18 baada ya kumalizia pasi ya straika wao, Leonel Ateba kufuatia mpira mrefu uliopigwa na mlinzi, Che Fondoh Malone.

Kipindi cha pili Simba iliongeza kasi ya kutafuta bao la pili huku wakiwa makini zaidi kwenye kuzuia ili wasiruhusu bao na kufanikisha ushindi huo ambao umewafanya kufikisha alama tisa ambazo ziliwafanya kuwa vinara wa kundi kwa muda kabla ya kushushwa nafasi ya pili baada ya kucheza mechi nne.

VIKOSI VYA MCHEZO HUO VILIKUWAJE?

CS Sfaxien

X1: Dahmen, Baccar, Traore (Willy 58′), Harabi, Layouni, Conte, Zaidi (Hmid 58′) Sekkouhi, Becha (Ben Ali 81′), Cristo (Habbesi 68′), Haj Hsan (Habboub 81′)

Simba

X1: Camara, Kapombe Zimbwe Jr, Che Malone, Hamza, Kagoma, Kibu (Chamou 86′), Ngoma, Ateba (Mukwala 90′), Mpanzu (Fernandez 76′), Ahoua

AHMED ATAMBA SIMBA KUTINGA ROBO FAINALI KIBABE

SIMBA
Ahmed Ally

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema kuwa wanashangilia ushindi waliopata ugenini dhidi ya Sfaxien, lakini amekiri kuwa licha ya kuwa karibu kufanikisha malengo yao bado wana kazi kubwa ya kufanya kutokana na ugumu wa mechi zilizo mbele yao.

“Tunajivunia kikosi chetu na kazi kubwa tuliyoifanya kwenye mchezo uliopita nchini Tunisia, tumeshinda ugenini hii ni furaha kwetu lakini bado hatujamaliza tuna kazi nyingine yakufanya kwenye mechi zinazofuata ili kupata ushindi na malengo ni kutinga hatua ya robo fainali hivyo mashabiki wanapaswa watambue hilo lipo wazi kabisa.

“Baada ya kumaliza mchezo wetu ugenini na kupata pointi tatu muhimu tunapaswa kufurahi lakini kwa kiwango kwa kuwa bado tuna kazi nyingine ya kufanya. Tutakuwa na mchezo Januari 12, Angola baada ya kumaliza mchezo huo tutakuwa na mchezo wa mwisho nyumbani.

“Kama mmefuatilia mtagundua kuwa mechi yetu dhidi ya Bravos mashabiki walikuja wachache, mechi yetu ya pili dhidi ya SC Sfaxine pia haikuwa na mashabiki wengi, sasa kwenye mechi yetu ya mwisho funga kazi dhidi ya Costantine tunahitaji mashabiki waujaze Uwanja wa Mkapa.”

AHOUA NI HABARI NYINGINE AWATULIZA WAARABU

SIMBA
Jean Charles Ahoua

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua amekuwa moto wa kuotea mbali hii ni baada ya kuendeleza takwimu nzuri kwenye michuano ya ndani ya kimataifa ambapo sasa kimataifa amefanikiwa kuhusika katika mabao manne akifunga mabao mawili na kuasisti mara mbili.

Ahoua kiungo wa Simba alifunga bao pekee katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya SC Sfaxine dakika ya 34 akitumia pasi ya Leonel Ateba likitosha kuwatuliza Waarabu wa Tunisia kwenye mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Ahoua alitumia pasi ya Ateba ambaye alipokea pasi ndefu ya maelekezo kutoka kwa beki wa Simba, Che Malone aliyeanza kikosi cha kwanza katika mchezo huo wa kimataifa akiongoza safu ya ulinzi iliyokuwa kwenye majukumu mazito ugenini.

 

Share this:

By Joel Thomas

Joel Thomas is a Tanzanian sports writer with a BSc (Education) from Mwenge Catholic University. He spent 4 years at Global Publishers and is in his second year with SportPesa, covering football and betting education for local fans. Anapenda soka na anaandika kwa uwajibikaji.