Jean SimbaJean Simba

SIMBA inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids kwenye anga la kimataifa imeandika rekodi yake katika Kombe la Shirikisho Afrika kwa ushindi nje ndani dhidi ya SC Sfaxine ndani ya dakika 180 na kete ya kwanza walianza Uwanja wa Mkapa dakika 90 wakishinda na mchezo wa pili ugenini kukamilisha dakika 180 wakashinda ugenini mchezo uliochezwa nchini Tunisia.

Kwenye mchezo wa ugenini uliochezwa Januri 5 2025 Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 ambalo lilidumu mpaka mwisho wa mchezo mtupiaji akiwa ni kiungo mshambuliaji Jean Ahoua akitumia pasi ya mshambuliaji Leonel Ateba.

KIPA Kazini
Kipa wa CS Sfaxine jitihada zake kuokoa pigo la Jean wa Simba ziligotea kwenye nyavu kimataifa. Source: Simba.

Ikumbukwe kwamba wawakilishi wote kimataifa walipata ushindi kwenye mechi zao ikiwa ni Yanga inayodhaminiwa na SportPesa hawa waliilaza TP Mazembe mabao 3-1 Uwanja wa Mkapa kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika mabao mawili yakifungwa na Clement Mzize na bao moja likifungwa Aziz Ki.

SEMAJI LA SIMBA LAUNGURUMA

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa wanashangilia ushindi waliopata ugenini lakini kwa kiwango kwa kuwa bado kazi haijaisha kutokana na kuwa na mechi nyingine mbele ngumu zaidi na kinachohitajika ni matokeo chanya.

“Tumeshinda ugenini hii ni furaha kwetu lakini bado hatujamaliza tuna kazi nyingine yakufanya kwenye mechi zinazofuata ili kupata ushindi na malengo ni kutinga hatua ya robo fainali hivyo mashabiki wanapaswa watambue hilo lipo wazi kabisa.

“Baada ya kumaliza mchezo wetu ugenini na kupata pointi tatu muhimu tunapaswa kufurahi lakini kwa kiwango kwa kuwa bado tuna kazi nyingine ya kufanya. Tutakuwa na mchezo Januari 9 Angola baada ya kumaliza mchezo huo tutakuwa na mchezo nyumbani.

“Mechi yetu dhidi ya Bravos mashabiki walikuja wachache, mechi yetu ya pili dhidi ya SC Sfaxine mashabiki walikuja wachache sasa kwenye mechi yetu ya mwisho funga kazi dhidi ya Costantine tunahitaji mashabiki waujaze Uwanja wa Mkapa.”

Ikumbukwe kwamba Januari 9 Simba itakuwa ugenini kusaka pointi tatu dhidi ya Bravos na walipokutana Uwanja wa Mkapa ubao ulisoma Simba 1-0 Bravos kwa bao la Ahoua ambaye alifunga kwa mkwaju wa penalti.

AHOUA ALIVYOWATULIZA WAARABU

JEAN
KIUNGO wa Simba Jean ambaye alifunga bao la ushindi kimataifa ugenini. Source: Simba.

Ni Jean Ahoua kiungo wa Simba alifunga bao pekee katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya SC Sfaxine dakika ya 34 akitumia pasi ya Leonel Ateba likitosha kuwatuliza Waarabu wa Tunisia kwenye mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Ahoua alitumia pasi ya Ateba ambaye alipokea pasi ndefu ya maelekezo kutoka kwa beki wa Simba, Che Malone aliyeanza kikosi cha kwanza katika mchezo huo wa kimataifa akiongoza safu ya ulinzi iliyokuwa kwenye majukumu mazito ugenini.

Bao la Ahoua linakuwa ni bao lake la pili kwenye anga la kimataifa katika Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuwa alianza kufunga kwenye mchezo dhid ya Bravos uliochezwa Uwanja wa Mkapa ilikuwa kwa mkwaju wa penalti Simba iliposepa na pointi tatu mazima ikiwa nyumbani.

Kipindi cha kwanza kilitosha kwa Simba kumaliza kazi huku kipindi cha pili wakiingia kwa mbinu kubwa ya kujilinda na kufanya mashambulizi ya kushtukiza ambayo hayakuleta matokeo chanya kwa upande wao na ulinzi uliimarika licha ya makosa kutokea katika dakika za lala salama ambapo Simba waliruhusu kona na faulo eneo la hatari.

KADI ZA NJANO ZILITEMBEA

Ateba na Jean
Ateba na Jean kwenye mchezo wa kimataifa ugenini wakati Simba ikisepa na pointi tatu. Source: Simba.

Kwenye mchezo huo kutokana na matumizi makubwa ya nguvu na kusaka ushindi kwa namna yoyote zilitembezwa kadi za njano kwa baadhi ya mastaa wa Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids.

Mshambuliaji Ateba alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 45 akiungana na Ellie Mpanzu ambaye alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 27. Ikumbukwe kwamba ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa Mpanzu kwenye anga la kimataifa alikwama kumaliza dakika zote 90 nafasi yake ilichukuliwa na Mavambo.

KUNDI A HALISHIKIKI

SIMBA SHANGILIA
WACHEZAJI wa Simba na benchi la ufundi wakishangilia baada ya ushindi kwenye mchezo wa kimataifa ugenini. Source: Simba.

Kwenye Kundi A Simba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 9 baada ya kucheza mechi 4 vinara ni Costantine wakiwa na pointi 9 hawa waliifunga Simba bado kazi inaendelea kwa timu tatu kusaka nafasi ya kutinga robo fainali kwa kuwa Bravos iliyopo nafasi ya tatu ina pointi 6.

Timu tatu zina nafasi ya kutinga robo fainali kutokana na matokeo ambayo wanayo kwenye anga la kimataifa huku CS Sfaxine mwendo wao wakiwa wameumaliza baada ya mechi nne zote wamepoteza kwenye msako wa pointi 12 wakipoteza nje ndani mbele ya Simba.

Katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 huku mtupiaji kwa Simba akiwa ni Kibu Dennis mkandaji na alianza kikosi cha kwanza ugenini ambapo hakukuwa na mashabiki uwanjani kutokana na timu hiyo kuwa na adhabu ya kucheza bila mashabiki.

Costantine wakiwa nyumbani walishinda mabao 4-0 dhidi ya Bravos mabao yakifungwa na Miloud Rebia dakika ya 41, Omoyele dakika ya 45, Belhocini dakika ya 87 na Mouaki dakika ya 89 hivyo pointi tatu Bravos walizpoteza kituo kinachofuata watakutana na Simba.

 

Share this: