YANGA ikiwa kwenye maandalizi ya mchezo ujao wa kimataifa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kiungo wa kazi Clatous Chama amerejea na kuanza mazoezi na wachezaji wengine kwa ajili ya dakika 90 za kazi kusaka pointi tatu muhimu uwanjani ndani ya 2025.
Yanga inayodhaminiwa na SportPesa imerejea katika ubora wake hivi karibuni kwa kupata matokeo chanya ndani ya uwanja katika mechi za ligi na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ikumbukwe kwamba Chama alipata maumivu ya mkono katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe uliochezwa Desemba 14 2024 na ubao ukasoma TP Mazembe 1-1 Yanga.

Kwenye mchezo bao la Yanga lilifungwa na Prince Dube dakika ya 90 baada ya hapo akawa nje kwa muda mpaka 2024 inagota mwisho hakuonekana uwanjani katika mechi za ushindani.
Kwa sasa amerejea na kuanza mazoezi ikiwa ni tayari kwa majukumu ya mechi zijazo ndani ya kikosi cha Yanga. Rekodi zinaonyesha kuwa kwenye Ligi Kuu Bara ambayo ni namba 6 kwa ubora Afrika, Chama amecheza mechi 11 akikomba dakika 486 kafunga bao moja na kutoa pasi mbili za mabao.
Kwa mujibu wa Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa Chama yupo tayari kwa ajili ya mechi zijazo na atakuwa sehemu ya msafara wa kikosi cha Yanga utakaosafiri kuwafuata wapinzani wao Al Hilal kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Clatous Chama amerejea na ameanza mazoezi na wachezaji wengine tayari kwa ajili ya mechi zetu zinazofuata. Tunatarajia kuwa atakuwa kwenye msafara wa kikosi kinachotarajiwa kuondoka Dar Alhamisi kwa ajili ya maandalizi ya mwisho dhidi ya Al Hilal.
HAWA HAPA MAMBO BADO

Kamwe ameogeza kuwa licha ya Chama kurejea uwanjani bado kuna wachezaji ambao hao watakosekana kwenye mchezo ujao wa kimataifa kutokana na kutokuwa fiti.
“Aziz Andambwile, Yao na Maxi hawa kwa mujibu wa madaktari wameshauri kwamba wanapaswa kuendelea kupata matibabu, bado hawajawa imara kurejea uwanjani kwa ajili ya mechi za ushindani na hawatakuwa kwenye mpango wa safari.”
RATIBA YA YANGA KIMATAIFA
Ratiba inaonyesha kuwa Januari 15 2025 itakuwa ni Al Hilal v Yanga ambapo Yanga watakuwa ugenini nchini Mauritania ngoma inatarajiwa kupigwa saa 4:00 usiku na kete ya mwisho katika hatua ya makundi itakuwa ni Yanga v MC Alger hii itapigwa Uwanja wa Mkapa Januari 18 2025 saa 10:00 jioni.
GUSA ACHIA YAJIBU

Mpango kazi wa gusa achia twende kwao Januari 4 2025 ulijibu Uwanja wa Mkapa baada ya dakika 90 ubao kusoma Yanga 3-1 TP Mazembe ulikuwa ni mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao ulikuwa na ushindani mkubwa huku Yanga ikivuna pointi tatu kwa mara ya kwanza katika hatua ya makundi.
Ikumbukwe kwamba mabao ya Yanga mawili yalifungwa na Clement Mzize alitupia dakika ya 33 na 60 na bao moja lilifungwa na Stephan Azizi Ki dakika ya 56. Bao pekee la TP Mazembe lilifungwa na Alioune Faty dakika ya 16 kwa mkwaju wa penalti iliyomshinda Djigui Diarra.
Ikumbukwe kwamba Diarra hakuwa kwenye mechi za ushindani baada ya kupata maumivu kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe ugenini hivyo hakuwa kwenye mechi za ushindani ndani ya ligi ni Khomein na Aboutwalib Mshery walikuwa kwenye majukumu kwenye kulinda lango.
KUNDI LINA MOTO

Yanga inafikisha pointi nne katika hatua ya makundi baada ya kucheza mechi nne ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo na TP Mazembe inabaki na pointi mbili nafasi ya nne. Vinara wa kundi A ni Al Hilal ambao wamekusanya jumla ya pointi 10 kibindoni baada ya kucheza mechi nne, MC Alger ni nafasi ya pili wakiwa na pointi 5 hivyo timu moja imekata tiketi ya kutinga hatua ya robo fainali ambayo ni Al Hilal.
Yanga, MC Alger na TP Mazembe hawa wote wanapambania malengo yao kutinga hatua ya robo fainali kwa kuwa kila timu ina mechi mbili ambazo ni dakika 180 za kusaka ushindi katika pointi sita yule atakayechanga karata yake kwa umakini ana nafasi ya kugotea nafasi ya pili kisha kutinga hatua ya robo fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

