GAMONDI AKALIA KUTI KAVU YANGA, DAKIKA 180 ZATAJWA

ByLunyamadizo Mlyuka

November 11, 2024
Miguel GamondiMiguel GamondiMiguel Gamondi

BAADA ya Yanga kupoteza mechi mbili mfululizo ndani ya uwanja msimu wa 2024/25 giza limetanda huku tetesi zikieleza kuwa huenda benchi la ufundi la timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi likafutwa na kuletwa kocha mpya kuendelea kuinoa timu hiyo ambapo kocha huyo anatajwa kukalia kuti kavu.

Ipo wazi kwamba Yanga inadhaminiwa na SportPesa hawa ni mabingwa watetezi wa ligi baada ya kucheza mechi 10 ni pointi 24 kibindoni wamekusanya walipoteza mechi mbili wakiwa nyumbani, Uwanja wa Azam Complex.

Mchezo wa kwanza ubao wa Uwanja wa Azam Complex ulisoma Yanga 0-1 Azam FC na mchezo wa pili ilikuwa Yanga 1-3 Tabora United, kwenye msako wa pointi sita iliyeyusha zote mazima ndani ya dakika 180.

GAMONDI NENO LAKE

Gamondi
Gamondi Miguel, Kocha Mkuu wa Yanga 2024/25. Source: Yanga.

Baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Tabora United, Gamondi alibainisha kuwa hakuna wa kumlaumu kwa kuwa walipata nafasi kwenye mchezo huo wakashindwa kuzitumia ndani ya uwanja.

“Tulipata nafasi tukashindwa kuzitumia unaona Aziz Ki alikosa penati hapo wao wakapata nafasi wakaitumia na kuna nafasi nyingine Kennedy Musonda alikosa hivyo ni matokeo na huwezi kumlaumu mtu makosa tutayafanyia kazi.”

JEMEDARI KUHUSU GAMONDI

Mchambuzi wa masuala ya michezo Bongo, Jemedari Said kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika kuwa kocha Gamondi amekamilia kuti kavu ambapo kuna kocha mpya anatarajiwa kuja kubeba mikoba yake.

Said ameandika: ”Kocha kutoka Algeria Kheireddine Madoui anatajwa kuwa mrithi wa Miguel Gamondi kwenye Klabu ya Yanga.

“Gamondi anatajwa kuondoshwa kutokana na vitu vingi lakini mwenendo mbaya wa timu yake kwenye mechi 2 za mwisho umetajwa kuwa sehemu tu (Kamba hukatikia pabovu).

“Jeuri, kiburi, kutoshaurika, ubishi, kupoteza ushawishi kwenye timu na wachezaji (dressing room) kutoelewana na wasaidizi wake vinatajwa kuwa vitu vinavyomuondoa Gamondi Yanga.

“Inasemekana mpaka sasa Gamondi ana elewana na msaidizi wake mmoja tu ambaye ni Msenegal Moussa Ndaw lakini wengine haelewani nao. Taarifa zinasema Ndaw huenda naye akaondoka na bosi wake Gamondi ili kupisha utawala mpya. Kuna habari za Gamondi na kocha wa makipa kurushiana maneno makali katika hoja ya kutoelewana na wasaidizi wake.

“Katika kuonyesha hali ya kukung’uta debe inasemekana mpaka Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu Andre Ntine kutoka Zambia pia nafasi yake imehojiwa klabuni hapo, ameongeza nini tangu amefika? Naye kuna orodha ya madudu mengi yanatajwa kumhusu hivyo akiondoka haitokuwa ajabu kipindi hichi mabingwa wa nchi wamedhamiria kusafisha ghala kuirejesha timu mstarini.”

 

WAHAMA UWANJA NA KUKAGUA KMC COMPLEX

Pacome
NYOTA wa Yanga, Pacome akiwa kwenye majukumu yake dhidi ya Yacouba wa Tabora United, Uwanja wa Azam Complex. Source: Yanga.

Msimu wa 2024/25 Yanga ilikuwa inatumia Uwanja wa Azam Complex kwa mechi za nyumbani baada ya kupoteza kwenye mechi mbili sasa imetangaza kuwa itautumia Uwanja wa KMC, Complex kwenye mechi za nyumbani za Ligi Kuu Bara na CRDB.

Mechi mbili mfululizo ndani ya dakika 180, Yanga ilipoteza kwa kuanza kushuhudia ubao ukisoma Yanga 0-1 Azam FC na mchezo wa pili ilikuwa Yanga 1-3 Tabora United, kwenye msako wa pointi sita iliyeyusha zote mazima ikiwa nyumbani.

MSIKIE ALI KAMWE

Kamwe
Kamwe Ali, Ofisa Habari wa Yanga 2024/25. Source: Yanga.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema kuwa kwa sasa watakuwa na furaha zaidi baada ya kuwa karibu na watani zao wa jadi Simba kwani awali walikuwa mbali na pia Uwanja wa KMC una nafasi kubwa ya kupumzika ikiwa shabiki atakuwa amepata tabu kidogo kwenye kushangilia.

“Unaona hapa KMC Complex viti vyake ni vizuri vinakupa nafasi ya kulala ikiwa utakuwa umepata tabu kidogo hakika uwanja ni mzuri na tumekuja kuendeleza burudani kwa kuwa wachezaji wapo tayari na mashabiki wanaipenda timu yao.

“Mpaka tumeamua kuja hapa tumejipanga na tumedhamiria kufanya kweli.Unajua kulikuwa na mambo mengi lakini kwa sasa tupo hap ana burudani itakuwa kubwa zaidi, mashabiki wazidi kujitokeza kwa wingi kwenye mechi zetu za nyumbani tukiwa hapa ni pazuri kwelikweli.”

AZAM FC YAWAKARIBISHA TENA CHAMAZI

Ibwee
Ibwee Hasheem, Ofisa Habari wa Azam FC 2024/25. Source: Azam FC.

Uongozi wa Azam FC umebainisha kuwa hauna tatizo lolote na wanaohitaji kutumia Uwanja wa Azam Complex kwa kuwa kila mtu ana haki yake kwenye matumizi na hakuna ambaye atazuiliwa kuutumia uwanja huo ikiwa atauhitaji.

Hasheem Ibwe, Ofisa Habari wa Azam FC amesema: “Kama wanaondoka sasa hakuna tatizo ni maamuzi unajua ukipanga unaruhusiwa kuhama na hakuna ambaye anakuzuia. Mengi yanasemwa sijui ukweli uko wapi kwa kuwa walikuwa wanauhuru mkubwa hasa kwenye matumizi ya uwanja hapa wakiwa nyumbani.

“Sisi hatuna tatizo, wameondoka ni saw ana wakirudi tunawakaribisha kikubwa sisi tunachukua mzigo wetu wao wanakuwa na kazi uwanjani kuendelea na kazi yao hakuna ubaya na hakuna tatizo lolote huu ni mpira na Maisha lazima yaendelee.”

Share this: