- Jean Ahoua kiungo mshambuliaji wa Simba SC anaongoza kwenye mkeka wa mastaa waliohusika kwenye mabao mengi ndani ya Ligi Kuu Bara 2024/25.
- Prince Dube wa Yanga SC ni mchezaji wa kwanza kuandika rekodi ya kufunga hat trick mbele ya Mashujaa, Uwanja wa KMC Complex.
- Feisal Salum maarufu kwa jina la Fei Toto amepenya kwenye mkeka wenye majina mengi ya nyota kutoka Simba SC na Yanga SC.
Yanga SC vs Simba SC majina yao yametawala ufungaji bora ndani ya Ligi Kuu Bara 2024/25 kutokana na kuhusika katika mchango wa mabao mengi katika mechi ambazo walishuka uwanjani kusaka pointi tatu ndani ya dakika 90.

Ipo wazi kuwa Yanga SC ni namba moja kwenye msimamo ikiwa na pointi 73, Simba SC ni namba mbili ikiwa na pointi 72 tofauti yao ni pointi moja na wote wamecheza jumla ya mechi 27 na timu nyingine ambazo zimebaki ni mechi 28 zimecheza.
Hapa tunakuletea orodha ya wachezaji waliohusika kwenye mabao mengi ndani ya ligi ikiwa ni vita ya ufungaji bora inazidi kupamba moto namna hii:-
Jean Ahoua wa Simba SC-23
Kwa mitambo ya mabao ndani ya Ligi Kuu Bara ambayo ni namba nne kwa ubora Afrika, kiungo mshambuliaji wa Simba SC anashikilia chati kwenye eneo hili. Ni mkali kwenye kufunga na kutengeneza pasi za mabao.
Jean Ahoua wa Simba katengeneza jumla ya pasi 8 za mabao na kafunga mabao 13. Kahusika kwenye mabao 23 kati ya 63 yaliyofungwa na timu hiyo iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi. Simba SC ni namba mbili kwa timu ambazo zimefunga mabao mengi ndani ya ligi. Ahoua ujanja wake ni kwenye mguu wa kulia akiwa kafunga mabao mengi kwa kutumia mguu huo ambayo ni mabao 14.
Soma na hii:Ukizubaa ndani ya ligi unaachwa mazima 2024/25
Prince Dube wa Yanga SC-21

Prince Dube wa Yanga katengeneza jumla ya pasi 8 za mabao katika kikosi hicho akiwa katupia mabao 13. Amehusika kwenye mabao 21 kati ya 71 yaliyofungwa na Yanga ndani ya ligi msimu wa 2024/25 wenye ushindani mkubwa.
Ipo wazi kwamba Dube ni nyota wa kwanza kufunga hat trick msimu wa 2024/25 ilikuwa dhidi ya Mashujaa kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC, Complex. Kwenye mchezo huo Dube alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo.
Pacome Zouzoua wa Yanga SC-18
Kiungo mshambuliaji wa Yanga SC Pacome Zouzoua anaingia kwenye orodha ya wakali kwenye kutengeneza pasi za mwisho akiwa nazo pasi 9. Ni miongoni mwa nyota ambao wanafanya kazi kubwa akiwa ndani ya Yanga SC

Sio kwenye kutoa pasi za mabao tu bali hata kufunga kiungo huyu mshambuliaji uwezo huo anao akiwa na mabao zaidi ya matano kibindoni ndani ya ligi. Pacome kibindoni ana mabao 9 hivyo kahusika kwenye mabao 18 kati ya 71 yaliyofungwa na timu hiyo inayoongoza ligi kwa msimu wa 2024/25 akiwa ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Miloud Hamdi.
Feisal Salum wa Azam FC-17
Mzawa ambaye ni namba moja kwenye eneo la kutengeneza pasi za mwisho yupo ndani ya kikosi cha Azam FC. Jina lake anaitwa Feisal Salum akiwa ni miongoni mwa wachezaji ambao wanavuja jasho ndani ya matajiri wa Dar.

Feisal katengeneza jumla ya pasi 13 za mabao na pasi yake ya kwanza alitoa kwenye mchezo dhidi ya KMC uliochezwa Uwanja wa KMC Complex ilikuwa dakika ya 19. Ni Idd Nado huyu ni mfungaji wa bao la kwanza ndani ya kikosi cha Azam FC kwenye ligi msimu wa 2024/25.
Weka mbali kutengeneza pasi za mwisho, Feisal anajua kufunga na mguu wake wenye nguvu ni ule wa kulia akiwa kafunga jumla ya mabao manne ndani ya ligi. Kahusika kwenye mabao 17 ndani ya Azam FC inayotumia Uwanja wa Azam Complex.
Clement Mzize wa Yanga SC-16
Mshambuliaji namba moja kwa wazawa ni Clement Mzize akiwa kafunga jumla ya mabao 13. Mzize ambaye ni chaguo la kwanza la Miloud kwenye mchezo dhidi ya Fountain Gate alichaguliwa kuwa mchezaji bora.
Yanga SC ikiwa imefunga mabao 71, mshambuliaji Mzize Clement kafunga mabao 13 na kutoa pasi tatu za mabao ambazo zinamfanya ahusike kwenye jumla ya mabao 16 kutoka kwa timu hiyo ambayo inaongoza ligi.
Soma na hii:Ufungaji bora 2024/25 orodha ya waliopo kwenye vita
Aziz Ki wa Yanga SC-16
Kiungo mshambuliaji wa Yanga SC, Aziz Ki kwa msimu wa 2024/25 kabla yakupata changamoto mpya alikuwa amehusika kwenye mabao 16 ndani ya kikosi hicho ambacho kimefunga jumla ya mabao 71 kwenye ligi namba nne kwa ubora.
Steven Mukwala wa Simba SC-15
Mshambuliaji wa Simba SC, Steven Mukwala anaingia kwenye orodha ya nyota waliohusika kwenye mabao mengi ndani ya ligi ikiwa ni msimu wake wa kwanza akiwa na uzi wa Simba. Ana tuzo ya mchezaji bora ndani ya Mei.
Mukwala raia wa Uganda kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Singida Black Stars uliochezwa Uwanja wa KMC Complex alifunga bao pekee la ushindi kwa Simba SC akifikisha mabao 12 na ametoa jumla ya pasi tatu akihusika kwenye mabao 15.
Vita ya ufungaji bora ndani ya ligi kwa msimu wa 2024/25 inakaribia kufika ukingoni huku nyota kutoka Yanga SC vs Simba SC wakiwa wameshika chati kwenye kuhusika katika mabao mengi. Mechi tatu kwa Yanga SC na Simba SC zimesalia huku Azam FC, Ken Gold, Kagera Sugar zikiwa ni miongoni mwa timu ambazo zina mechi mbili kukamilisha mzunguko wa pili.

