- Mzawa anayekimbiza kwenye eneo la kucheka na nyavu ni Mzize anayekipiga Yanga akiwa katupia mabao 13.
- Aziz Ki alisepa na tuzo ya ufungaji bora 2023/24 alikuwa kwenye vita kali na Feisal Salum wa Azam FC.
- Kiungo mshambuliaji Jean Ahoua mabao yake yote katupia kwa mguu wa kulia ambayo ni 12.
VITA ya ufungaji bora ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara inazidi kushika kasi na kwa sasa ni mzunguko wa pili unakaribia kugota mwisho 2024/25.

2023/24 vita kali ilikuwa kwa nyota wawili ambao walikuwa wakiipambania kati ya Aziz Ki wa Yanga na Feisal Salum wa Azam FC na ngoma tuzo ikachukuliwa na Aziz wa Yanga.
Hawa hapa kwenye vita ya ufungaji bora
Clement Mzize

Mshambuliaji namba moja kwenye eneo la utupiaji ndani ya ligi ni Clement Mzize mali ya kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi. Mzize katupia jumla ya mabao 13 katika mchezo dhidi ya Fountain Gate alipachika mabao mawili nakufikisha mabao 13.
Yanga SC imetupia jumla ya mabao 68 ndani ya ligi ikiwa ni timu namba moja yenye mabao mengi kibindoni kwa msimu wa 2024/25. Huyu ni mzawa namba moja kwa utupiaji.
Prince Dube
Prince Dube mshambuliaji wa Yanga katupia mabao 12 yeye ni raia wa Zimbabwe. Ukiweka kando kufunga Dube nim kali kweye kutengeneza pasi za mwisho akiwa na rekodi ya kutengeneza jumla ya pasi 8 za mabao katika kikosi.

Jumla Dube kahusika kwenye mabao 20 kati ya 68 yaliyofungwa na Yanga ndani ya ligi. Huyu anaingia kwenye rekodi ya kuwa nyota wa kwanza kufunga hat trick kwenye ligi ilikuwa kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC, Complex.
Jean Ahoua
Jean Ahoua kiungo wa Simba ana mabao 12 yeye ni raia wa Ivory Coast. Mguu wenye nguvu kwenye utupiaji kwa Ahoua ni ule wa kulia akiwa katupia mabao yote hayo kwa mguu wa kulia. Katengeneza pasi 7 za mabao Ahoua akihusika kwenye 19 kati ya 52 yaliyofungwa na Simba SC.
Jonathan Sowah
Mshambuliaji wa Singida Black Stars ni ingizo jipya ndani ya timu hiyo kwenye dirisha dogo akiwa katupia jumla ya mabao 11. Huyu ni raia wa Ghana timu ya Singida Black Stars ikiwa nafasi ya nne na pointi 53 na safu ya ushambuliaji imetupia mabao 40.
Elvis Rupia
Mshambuliaji mwili jumba wa Singida Black Stars Elvis Rupia anaingia kwenye orodha ya wakali wakucheka na nyavu akiwa katupia mabao 10. Huyu ni raia wa Kenya ambaye ana zali lakucheza na nyavu.
Steven Mukwala

Mshambuliaji wa Simba SC Steven Mukwala katupia jumla ya mabao 9 huyu ni raia wa Uganda. Katika mchezo dhidi ya Mashujaa FC ugenini nyota huyo alipachika bao la jioni dakika ya 90 akitumia pasi ya Awesu Awesu.
Pacome Zouzoua
Kiungo mshambuliaji wa Pacome Zouzoua anaingia kwenye orodha ya wakali kwenye kutengeneza pasi za mwisho akiwa nazo pasi 9. Sio kwenye kutoa pasi za mabao tu bali hata kufunga ni mkali. Kibindoni ana mabao 9 hivyo kahusika kwenye mabao 18 kati ya 68 yaliyofungwa na Yanga.
Walikimbiza 2023/24 hawa
Aziz Ki alihusika kwenye mabao 29 kati ya 71 yaliyofungwa na Yanga iliyotwaa ubingwa. Yanga ilikuwa ni namba moja kwa timu ambazo zilizofunga mabao mengi msimu uliopita na sasa inaongoza kwenye eneo la utupiaji.
Kiungo Feisal alihusika kwenye mabao 26 kati ya 63 yaliyofungwa na Azam FC timu hiyo ikiwa ni namba mbili kwa timu zilizofunga mabao mengi. Kwa msimu wa 2024/25 Azam FC ni namba tatu kwa timu iliyofunga mabao mengi ambayo ni 43 baada ya kucheza mechi 27.
Kwa msimu wa 2024/25 kiungo Feisal ni namba moja kwenye eneo la kutengeneza pasi za mwisho huku eneo la utupiaji akiwa hajaonyesha ubora wake kwa ukubwa katika kuifikia rekodi yake mwenyewe akiwa kafunga mabao manne.

Feisal Salum katengeneza jumla ya pasi 13 za mabao na pasi yake ya kwanza alitoa kwenye mchezo dhidi ya KMC uliochezwa Uwanja wa KMC Complex ilikuwa dakika ya 19 alimpa mshikaji wake Idd Nado ambaye ni mfungaji wa bao la kwanza ndani ya kikosi cha Azam FC kwenye ligi msimu wa 2024/25.

