- JKT Tanzania FC Vs Simba SC 5/5/2025 ngoma inapigwa Uwanja wa Jenerali Isamuyo Mbeni, DSM
- Mara ya mwisho timu hizo kukutana Simba walishinda bao 1-0 ambapo ulipigwa Desemba 24, mwaka jana
- Mchezo huu utafuatiliwa na mamilioni ya mashabiki kufuatia matukio ya mchezo uliopita wa Simba dhidi ya mashujaa
JKT Tanzania FC Vs Simba SC 5/5/2025 ni vita ya kupasha viporo kwa Simba wakisaka pointi tatu muhimu ugenini dhidi ya JKT Tanzania, huku mabosi wa Simba wakifanya kikao kizito cha kupanga mikakati ya ubaya ubwela ili kumaliza msimu kwa kishindo.
Huu unakuwa mchezo wa pili wa kiporo kwa Simba kucheza mara baada ya mchezo uliopita kuvaana na Mashujaa FC na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 siku ya Ijumaa mchezo ukipigwa kwenye dimba la KMC.
JKT waichimba mkwara mzito Simba!

Mara baada ya kufanikiwa kupata matokeo mazuri dhidi ya timu kubwa za Yanga na Azam katika Uwanja wao wa nyumbani, JKT Tanzania wametamba kuwa Simba wajiandae kukutana na mchezo mgumu.
Kutokana na ubora ambao wameonyesha kwenye mashindano mbalimbali msimu huu, JKT wametamba kuwa wataingia uwanjani kwa tahadhari kubwa na lengo kupata ushindi ili kujiweka katika nafsi nzuri kwenye msimamo wa ligi.
JKT Tanzania FC Vs Simba SC 5/5/2025: Namba zinaibeba Simba

Tangu kuanza msimu huu Simba SC wameonyesha kuwa na ubora mkubwa hasa kwenye eneo la ulinzi, ambapo ni timu namba moja kufungwa mabao machache msimu wa 2024/25 ambayo ni 9 baada ya kucheza mechi 23, huku pia wakionyesha kuwa hatari wakiwa ndani ya 18.
Ni mabao 54 ya jumla ambayo Simba SC imefunga na katika hayo mabao 50 yamefungwa na wachezaji wao wakiwa ndani ya 18 huku 12 ikiwa ni penati na ndiyo timu ambayo imefaidika zaidi na mapigo ya penalty.
JKT wagumu kupoteza kwenye Uwanja wao
Miongoni mwa ubora mkubwa wa rekodi ambao JKT wamekuwa nao msimu huu ni kupata matokeo mazuri dhidi ya timu nyingine wanapocheza kwenye Uwanja wao wa nyumbani Mbweni. JKT ni miongoni mwa timu imara kwenye kucheza kwa kujilinda.
Ubora huo kwenye ulinzi umeifanya JKT kuwa miongoni mwa timu zilizokusanya sare nyingi zaidi.
Waliokosekana Vs Mashujaa, warejea Simba

Kuelekea mchezo huu, Simba wanatarajia kurejea kwenye makali yao kutokana na kurejea kwa baadhi ya mastaa wao muhimu waliokosa mchezo uliopita dhidi ya Mashujaa wakiwemo kiungo, Jean Charles Ahoua.
Kuhusu mlinzi, Che Malone ambaye alikuwa nje kwa muda akiuguza majeraha aliyoyapata kwenye mchezo dhidi ya Azam, baada ya kuwa nje kwa muda akipambania hali yake amerejea kuwa ya kikosi cha Simba SC.
Che Malone alipata nafasi ya kurejea tena uwanjani kupitia mchezo wa kimataifa wa nusu fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch FC uliochezwa nchini Afrika Kusini ambapo aliingia dakika ya 86 akichukua nafasi ya Ellie Mpanzu.
Matola aahidi ushindi mbele ya JKT
Seleman Matola, kocha msaidizi wa Simba SC ameweka wazi ubora wa wapinzani wao JKT Tanzania na wanatarajia mchezo mgumu, lakini ametamba kikosi chao kimejiandaa vya kutosha kukabiliana na hali hiyo.
“Tunatambua ubora na ugumu wa wapinzani wetu JKT Tanzania, hivyo ni wazi tunatarajia mchezo mgumu na wapinzani wetu wameonyesha hilo mara kadhaa, lakini tutaingia kwa umakini na kucheza kama fainali kufikia malengo yetu ya kupata pointi tatu muhimu.”
Mabosi Simba wafanya kikao kizito

Kuelekea kufungwa kwa msimu wa 2024/25 huku kikosi chao kikiwa na mafanikio makubwa katika mashindano matatu wanayoshiriki, mabosi wa Simba jana Jumapili walikutana chini ya Rais wa heshima wa timu hiyo, Mohammed Dewji.
Bodi ya wakurugenzi ya Simba ilikutana kwa maelezo kuwa na mpango mkakati wa kufanya tathimin ya kikosi chao mpaka hapa walipofika na kujua ni namna gani wanaweza kumaliza msimamo wa ligi na mashindano mengine wanayoshiriki kwa kishindoikiwemo mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

