- Real Madrid 3-2 Celta Vigo ni ushindi muhimu ambao umeirudisha Madrid katika mbio za ubingwa
- Kylian Mbappe aongoza Oparesheni ya kusaka pointi tatu nyumbani, mara baada ya kuibuka shujaa kwa kufunga mabao mawili.
- Kituo kinachofuata ni dabi ya El Classico wikiendi ijayo: Barcelona Vs Real Madrid.
Real Madrid 3-2 Celta Vigo ni ushindi muhimu ambao umeirudisha Madrid katika mbio za ubingwa kwa kupunguza pengo la pointi kati yao na vinara Barcelona.
Ni straika wa kimataifa wa Ufaransa, Kylian Mbappe ndiye ambaye aliongoza Oparesheni ya kusaka pointi tatu nyumbani, mara baada ya kuibuka shujaa kwa kufunga mabao mawili katika ushindi huo.
Katika mchezo huo wa kusisimua nusura Madrid waangushe pointi na walilazimika kujikaza kuzuia ‘Come back’ ya wapinzani wao Celta Vigo.
Ikumbukwe kabla ya mchezo wa leo Jumapili pengo la pointi kati ya Madrid na vinara wa msimamo wa ligi Barcelona lilikuwa pointi 7, lakini kwa ushindi ambao wameipata Madrid umeshusha pengo hilo mpaka kuwa pointi nne.
Real Madrid 3-2 Celta Vigo, mchezo ulikuwaje?

Kylian Mbappe alifunga mara mbili huku Madrid wakipambana na upinzani mkali wa mwisho kutoka kwa Celta ambao walikuwa karibu kupindua meza.
Mabingwa watetezi Madrid, walio katika nafasi ya pili, walijikuta wakilazimika kujilinda kwa nguvu katika uwanja wa Santiago Bernabeu dhidi ya Celta.
Celta walioko nafasi ya saba ambao nao wanapambana na wapo na matumaini ya kumaliza nafasi za juu ili kufuzu kwa mashindano ya Ulaya msimu ujao.
Kikosi cha Carlo Ancelotti kilikuwa na mapungufu kutokana na majeruhi upande wa ulinzi huku baadhi ya wachezaji wakitumika adhabu, Celta wakitaka kutumia faida hiyo walifanyamashambulizi ya hatari mwanzoni mwa mchezo.
Lakini baada ya kustahimili mashambulizi ya awali ya Celta, Madrid walichukua udhibiti wa mchezo, huku kinda wa Kituruki mwenye umri wa miaka 20, Arda Guler, akiongoza mashambulizi kwa kuwa Rodrygo alikuwa nje kwa matatizo ya afya.
Guler alijaribu majaribio kadhaa ikiwemo shambulizi la tik-tak, ingawa mpira ulipita pembeni mwa goli, akionyesha kuwa hana hofu ya kujaribu mambo makubwa.
Celta Vigo nao walifanya majaribio kadhaa ikiwemo lile la beki wa zamani wa Barcelona, Marcos Alonso aliyepiga kichwa nje kidogo na baadaye Courtois akaokoa shuti lake kwa ustadi, huku Celta wakitishia.
Aurelien Tchouameni alipiga kichwa juu akiwa kwenye nafasi nzuri upande wa Madrid, huku wenyeji wakizuia wageni. Madrid walifungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Guler dakika ya 33, alipofanikiwa kupata nafasi ndani ya boksi na kupiga mpira wa kupinda kwa ustadi ambao ulizama golini pembeni mwa Guaita.
Mbappe aliongeza bao la pili dakika ya 39 baada ya shambulizi la kasi. Courtois aliokoa mpira wa Borja Iglesias, kisha Madrid wakafanya shambulizi la haraka ambapo Bellingham alimpa Mbappe pasi safi pembeni ya kulia.
Nyota huyo wa Ufaransa alipiga shuti kali lililompita Guaita kutoka ndani ya eneo la hatari. Mbappe alipachika bao lake la pili dakika ya 48, baada ya kukimbia kupokea pasi murua ya Guler na kupiga kwa mguu wa kushoto hadi kona ya chini.
Celta wacharuka, wakaribia kupindua meza

Hata hivyo, Celta hawakukata tamaa na Javi Rodriguez alipunguza pengo kwa bao dakika 20 kabla ya mchezo kumalizika, akifunga kutoka karibu baada ya Madrid kushindwa kuondoa kona ipasavyo.
Ushindi ambao ulionekana kuwa rahisi kwa Madrid ulianza kuwa mgumu baada ya, Iago Aspas kutoa pasi nzuri kwa mchezaji wa akiba Williot Swedberg aliyefunga bao la pili dakika ya 76.
Pablo Duran alikaribia kusawazisha dakika mbili baadaye baada ya kuachwa wazi kwa pasi nyingine nzuri kutoka kwa Aspas, lakini Courtois alifanikiwa kuokoa baada ya mpira kupenya chini ya mwili wake.
Kwa kuwa wageni walikuwa wakisukuma kwa kusaka bao la kusawazisha, nafasi zilipatikana kwa pande zote mbili katika dakika za mwisho za msisimko, lakini Los Blancos walidumu hadi mwisho kupata alama tatu muhimu.
Real Madrid 3-2 Celta Vigo, kituo kinachofuata ni Barcelona

Baada ya kufufua matumaini ya kutwaa ubingwa wa La Liga kwa ushindi dhidi ya Celta Vigo, Madrid sasa kituo kinachofuata ni dhidi ya Barcelona wikiendi ijayo.
Madrid watahitaji kushinda mchezo huo dhidi ya Barcelona ili kujiweka katika nafasi ya kushinda ubingwa wa La Liga, ambapo zitakuwa zimesalia mechi tatu tu, kabla ya kumaliza msimu.
Ikiwa Madrid watashinda mchezo huo, watakuwa wanajiweka katika nafasi ya kushinda ubingwa kwani pengo la pointi kati yao na Barcelona itakuwa moja.
La Liga tumaini pekee la Madrid
Baada ya kampeni yao ya kutetea taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kuanguka, na pia kushindwa kwenye fainali ya Copa del Rey dhidi ya Barcelona wiki iliyopita, Los Blancos sasa bado wana matumaini ya kuwashinda vijana wa Hansi Flick kwenye LaLiga.
Ushindi huu unamaanisha kuwa mabingwa watetezi Real Madrid wataelekea Barcelona Jumapili ijayo wakiwa na matumaini kuwa ushindi wao wa tano mfululizo unaweza kuwaweka pointi moja tu nyuma ya mahasimu wao wakuu, huku zikiwa zimesalia mechi tatu.

