- Simba SC iliwazimia kitufe cha kicheko mzunguko wa kwanza dakika ya 90 mazima ugenini.
- Mashujaa FC yagomea unyonge kuwakabili Simba SC kwa namna watakavyokuja.
- Milioni 100 zatolewa macho na Mashujaa FC wakimuua mnyama Simba SC jumlajumla.
Simba SC vs Mashujaa FC ni vita ya msako wa pointi tatu ndani ya uwanja huku makocha wa timu zote mbili wakibainisha kuwa hesabu kubwa ni kupata matokeo chanya kwenye mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Mei 2 2025.

Ipo wazi kwamba huu ni mchezo wa mzunguko wa pili baada ya ule wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma baada ya dakika 90 ubao kusoma Mashujaa 0-1 Simba SC. Mzunguko wa pili unapigwa KMC Complex.
Mashujaa FC wamebainisha kuwa hawajasahau bao ambalo walifungwa dakika ya 90+7 na mshambuliaji Steven Mukwala akitumia pasi ya Awesu Awesu hivyo wataingia uwanjani kwa tahadhari kubwa na lengo kupata ushindi. Inaelezwa kuwa kuna ahadi ya milioni 100 kwa wachezaji wa Mashujaa FC ikiwa watamuua mnyama Simba SC.
Uimara wa Simba SC
Simba SC ni imara kwenye eneo la ulinzi, ikiwa ni timu namba moja kufungwa mabao machache msimu wa 2024/25 ambayo ni 8 baada ya kucheza mechi 22. Ukiweka kando eneo la ulinzi wachezaji wake wanahatari zaidi kufunga wakiwa ndani ya 18.

Ni mabao 52 jumla Simba SC imefunga na katika hayo 48 yalifungwa na wachezaji wakiwa ndani ya 18 huku 9 ikiwa ni penati. Simba SC ni timu namba moja kwa kupata penati nyingi ambazo ni 10, kwenye hizo 10 tano alipiga Jean Ahoua alifunga zote, tano alipiga Leonel Ateba huyu alifunga nne na kukosa moja dhidi ya Namungo.
Uimara wa Mashujaa FC
Mashujaa FC ni imara kwenye kucheza kwa kujilinda hasa jambo linalofanya iingie kwenye orodha ya timu tatu ambazo zimepata sare nyingi ndani ya uwanja kwenye msako wa pointi tatu muhimu.
Mashujaa ni namba tatu ikiwa imekusanya jumla ya sare 9 vinara ni JKT Tanzania ambao wamekusanya sare 11 huku Coastal Union ikiwa ni namba mbili ni sare 10 ilikusanya ndani ya uwanja.
Katika eneo la ushambuliaji Mashujaa FC safu yake ilitupia mabao 26 na ukuta ukiruhusu mabao 30 baada yakucheza jumla ya mechi 26 ikiwa nafasi ya 10 kwenye msimamo.
Beki Simba SC arejea
Che Malone beki wa Simba SC huenda akawa sehemu ya wachezaji watakaokuwa kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa FC unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC Complex.

Beki huyo alikuwa nje kwa muda mrefu baada ya kupata maumivu kwenye mchezo wa Mzizima Dabi uliochezwa Uwanja wa Mkapa mzunguko wa pili.
Ilikuwa ni Februari 24 2025 Che Malone alikwama kuendelea katika mchezo huo ambao baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 2-2 Azam FC wababe hao wakigawana pointi mojamoja.
Baada ya kuwa nje kwa muda akipambania hali yake amerejea sehemu ya mazoezi ya kikosi cha Simba SC ikumbukwe kwamba Che Malone alipata nafasi ya kucheza mchezo wa kimataifa dhidi ya Stellenbosch FC uliochezwa nchini Afrika Kusini ikiwa ni mkondo wa pili hatua ya nusu fainali alianzia benchi akiingia dakika ya 86 akichukua nafasi ya Ellie Mpanzu.
Seleman Matola kocha msaidizi wa Simba SC neno
Seleman Matola, kocha msaidizi wa Simba SC amesema kuwa wanatambua mpinzani wao Mashujaa FC yupo imara wataingia kucheza kama fainali ili kufikia malengo yakupata pointi tatu.
Mzunguko wa kwanza Uwanja wa Lake Tanganyika, Novemba Mosi 2024 baada ya dakika 90 ubao ulisoma Mashujaa FC 0-1 Simba SC bao la ushindi likifungwa na Steven Mukwala dakika ya 90 akitumia pasi ya Awesu Awesu.
Nyota hao wote wa Simba SC ambao walihusika kwenye bao la ushindi mchezo uliopita wote walianzia benchi na walipoingia walitimiza majukumu waliyopewa kwenye msako wa pointi tatu muhimu.
Matola amesema: “Tunatambua mchezo wetu utakuwa mgumu kwa kuwa wapinzani wetu wapo imara ila tutaingia kwa umakini na kucheza kama fainali kufikia malengo yetu ya kupata pointi tatu muhimu.”
Huyu hapa kocha wa Mashujaa FC

Charlse Fred, kocha msaidizi wa Mashujaa FC iliyo nafasi ya 10 kwenye msimamo na pointi zake 30 baada ya mechi 26 ameweka wazi kuwa watapambana kwa kila namna kuwakabili wapinzani wao Simba SC.
“Timu nzima na wachezaji wote tupo tayari kila idara kuanzia safu ya ulinzi hadi washambuliaji, hivyo tutapambana na kila hali ambayo timu ya Simba watakuja nayo. Tunatambua uimara wao na ulipo nasi tumefanya maandalizi mazuri.”

