
Mara baada ya kushushwa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa muda kikosi cha Simba wamerejea tena kibabe kileleni baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Fountain Gate FC.
Mchezo huo unakuwa mchezo wa pili kwa Simba ambao wamewahi kuwa na udhamini mnono wa Kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Tabora United walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Simba wamekuwa na mwanzo mzuri wa msimu huu wa 2024/25 wakicheza michezo yote miwili katika Uwanja wa KMC Complex unaopatikana Mwenge, Dar es Salaam.
MCHEZO ULIKUWAJE?

Simba wakiuanza mchezo huo kwa kujiamini walifanikiwa kuandika bao la kwanza mapema tu, kipindi cha kwanza kupitia kwa kiungo wao mshambuliaji, Edwin Balua ambaye aliifungia Simba kwa kichwa akiunganisha pasi safi ya kiungo, Jean Charles Ahoua.
alitupatia bao la kwanza kwa kichwa dakika ya 13 baada ya kumalizia mpira krosi uliopigwa na Jean Charles Ahoua.
Baada ya bao hilo la kuongoza, Simba waliendelea kulisakama lango la Fountain Gate na kufanikiwa kuifungua safu ya ulinzi ya Fountain Gate ambapo straika, Steven Mukwala aliifungia bao la pili dakika ya 44 ya mchezo akimalizia pasi safi kutoka kwa Shomari Kapombe.
Timu hizo zilienda mapumziko huku Simba wakiwa mbele kwa mabao 2-0. Kipindi cha pili wenyeji walianza kwa kasi wakiendeleza kutengeneza nafasi za kufunga ambapo jitihada hizo zilizaa matunda kwa, Ahoua kuifungia bao la tatu dakika ya 59 kwa shuti kali la kuzungusha mpira ‘curve’ 18 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Balua.
Wakionekana kuumaliza mchezo, Valentino Mashaka aliwapatia wenyeji bao la nne dakika ya 81 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Ahoua.
SIMBA KILELENI MWA MSIMAMO WA LIGI MPAKA SASA
Ushindi huu unaifanya kufikisha pointi sita baada ya kucheza mechi mbili, ambapo pia wamefanikiwa kufunga mabao saba, huku wakiwa hawajaruhusu bao lolote.

HIVI HAPA VIKOSI VYA TIMU ZOTE MBILI
SIMBA
X1: Camara, Kapombe (Kijili 65′), Zimbwe Jr, Hamza, Che Malone, Mzamiru (Kagoma 55′), Balua (Karabaka 81′), Fernandes, Mukwala (Mashaka 55′), Ahoua, Awesu (Kibu 65′).
FOUNTAIN GATE
X1: Fikirini, Lulambo Kadikilo, Hebrone, Makame, Kulandana, Ambundo (Mwampangama 48′), Kassim, Kilemile (Zamfuko 83′), Sadick (Mwalimu 48′), Kihimbwa
Walioonyeshwa kadi: Laurian Makame 74′ Erick Nkosi 86′
KOCHA SIMBA ATOA TAMKO LA UBINGWA
Mara baada ya mchezo huo uongozi wa Wanamsimbazi umeweka wazi kuwa wameanza taratibu kujipata na malengo yao ni kuhakikisha wanashinda michezo iliyo mbele yao na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kushinda ubingwa msimu huu.
Akizungumzia kikosi chake kocha mkuu wa Wekundu wa Msimbazi, Fadlu Davids amesema: “Ni jambo zuri kwetu kupata matokeo ya ushindi katika mchezo wetu huu wa pili.
“Taratibu baada ya kikosi chetu kupata wiki sita za mazoezi pamoja na kucheza mechi kadhaa za kirafiki, zile za Ngao ya Jamii na hizi za ligi, tunaendelea kuongezeka utayari wetu kwa michezo ya Ligi Kuu.
“Malengo yetu ilikuwa kuhakikisha tunaanza vizuri ligi kwa kupata matokeo ya ushindi na tunashukuru kufanikisha hilo. Kikosi chetu kipo kwenye umbo bora la kiushindani na mawasiliano ndani ya uwanjani yameendelea kuimarika, malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda kila mechi ili kujiweka sawa kwenye harakati za kupigania taji la ubingwa,” amesema Kocha Fadlu.
MUTALE AENDELEA KUKOSEKANA

Licha ya ushindi huo pigo kwa Simba ni kuwa walilazimika kuingia katika mchezo huo wakiwa wanaendelkea kukosa huduma ya kiungo wao wa kimataifa wa Zambia, Joshua Mutale.
Mutale alipata majeraha katika mchezo wa kwanza pale Simba walipoikaribisha Tabora United katika mchezo wa ufunguzi na kushuhudia mchezaji huyo akishindwa kuendelea na mchezo na kutolewa dakika ya 31 baada ya kupata maumivu ya mguu.
Mutale ambaye baadaye alifanyiwa vipimo na anatarajiwa kukosekana kwa kipindi cha wiki mbili ambapo mpaka sasa bado taarifa rasmi haijatolewa kuhusu ukubwa wa jeraha lake.

