WAWAKILISHI wa Tanzania Ligi ya Mabingwa Afrika wamebainisha kuwa watapambana kufanya vema katika mechi za marudiano ili kupeperusha vema bendera ya Tanzania kimataifa. Ni Yanga na Azam FC hizi zote zipo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika huku Coastal Union na Simba zipo katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Mchezo ujao wa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’O ambapo wameweka wazi kuwa wataongeza dozi ya mabao ili kutuma salamu kwa wapinzani wao kimataifa 2024/25 ndani ya uwanja. Azam FC mchezo wao ujao ni dhidi ya APR, Coastal Union itakuwa dhidi ya Bravos.

Ikumbukwe kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ilikuwa na kibarua cha kusaka ushindi mchezo wa awali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’O mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex na kuibuka kwa ushindi wa mabao 4-0.
Agosti 24 ambayo itakuwa Jumamosi, Yanga itashuka Uwanja wa Mkapa kusaka ushindi dhidi ya wapinzani wao hao kwenye ngwe itakayoamua nani atasonga mbele katika anga la kimataifa.
WATUPIAJI KIMATAIFA KWA YANGA
Katika mchezo uliopita mabao ya Yanga anga la kimataifa yalifungwa na Prince Dube dakika ya 6, Clatous Chama ambaye ni ingizo jipya akitokea Simba ilikuwa dakika ya 67, Clement Mzize dakika ya 74 na chuma cha nne ni mali ya Aziz Ki dakika ya 90 kwa mkwaju wa penalti.
Ushindi huo unaipa Yanga zawadi ya milioni 20 ikiwa ni goli la mama ambapo kila bao lina thamani ya milioni 5 kwenye hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika kila timu inapopata ushindi.
SEMAJI KAMWE KUHUSU MCHEZO UJAO

“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mpaka sasa hivi hatuna majeruhi katika kikosi chetu, wachezaji wako fiti na wanaendelea na maandalizi ya Mchezo wetu wa Jumamosi dhidi ya Vital’O pale Benjamin Mkapa.
“Ambacho tunahitaji ni kupata ushindi mkubwa ukizingatia tunakwenda kucheza Uwanja wa Mkapa, mashabiki wajitokeze kwa wingi kuujaza uwanja na kuwaongezea nguvu wachezaji kwa kuwa hili linawezekana na kila kitu kinakwenda vizuri.
“Niwaambie ndugu zangu Wanahabari, Yanga ni kisima cha ubunifu, sisi tuna watu wanafikiria zaidi, tunayo project nyingine nzuri zaidi na tutaweka Historia nyingine kama ilivyokuwa ile ya Max Day Pacome Day, Muda Day na nyinginezo. Mechi hii ya Vital O tumeiacha pekee kwakuwa ni ufunguzi wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
“Msimu huu tunayo kazi kubwa sana ya kufanya. Kazi ya kwanza sisi kufanya vizuri lakini nimegundua pia tuna kazi kubwa ya kuwaombea wenzetu dua nao wafanye vizuri. Tuna wasiwasi mkubwa sana na mwenendo wa wenzetu kwani matokeo yao hayaridhishi.
KWA MKAPA HAPATOSHI

“Matarajio yetu ni kuujaza Uwanja wa Benjamini Mkapa kwenye mechi dhidi ya Vital O. Lakini vile vile tunayo hamasa kubwa ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo ni goli la mama hamasa ya Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan msimu huu imeanza hatua ya mwanzo kabisa.
“Sasa hivi tupo kwenye mahesabu ya kuangalia inabidi tufunge magoli mangapi ili tupate hela nyingi. Tunaweza kutafuta mshahara wa wafanyakazi kwenye goli la mama pekee.
“Kupitia mashindano ya CAF, hatua hizi za awali, kuna ujumbe tunataka kuupeleka kwa wale ambao wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa AFRIKA. Tutatuma ujumbe ndani ya Uwanja na nje ya Uwanja. Nje ya Uwanja tulituma ujumbe msimu uliopita kwa kujaza Uwanja wa ugenini.”
BEI YA TIKETI
Mzunguko ni 5,000, VIP C 10,000, VIP B 20,000, VIP A 30,000. Kamwe amebainisha kuwa mashabiki waanze kununua tiketi mapema ili kupunguza presha siku ya mchezo na kuwa na uhakika kuutazama mchezo huo wakiwa Uwanja wa Mkapa
AZAM FC HESABU ZAO HIZI HAPA

Matajiri wa Dar, Azam FC hesabu zao ni kuelekea mchezo wa marudio katika Ligi ya Mabingwa ambao unatarajiwa kuchezwa Rwanda Jumamosi, Aprili 24 2024.
Ipo wazi kuwa Katika mchezo wa awali uliochezwa Uwanja wa Azam Complex Agosti 18 2024 baada ya dakika 90 ubao ulisoma Azam FC 1-0 APR hivyo Azam FC ilikomba milioni tano kwenye anga la kimataifa goli la mama. Ni dakika ya 55 nyota Jhonier Blanco alipachika bao pekee la ushindi akifungua code kwa mguu wa kulia likadumu mpaka mwisho wa mchezo. Penalti hiyo ilisababishwa na kiungo Feisal Salum ambaye alichezewa faulo akiwa ndanj ya 18.
Yusuph Dabo, Kocha Mkuu wa Azam FC ameweka wazi kuwa wanakwenda kufanya kazi kubwa kwenye mchezo wa marudio kwa kuwa wanatambua uimara wa wapinzani wao ulipo.
“Kupata ushindi kwenye mchezo wa kwanza ni furaha kwetu lakini bado kazi haijaisha, tunakwenda ugenini kutafuta ushindi na tunatambua kwamba utakuwa mchezo wenye ushindani tupo tayari.”

