
Huku wakiendelea kusherehekea mwanzo bora wa msimu kufuatia kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United, pigo zito limeikumba kambi ya Simba, hii ni baada ya taarifa za ndani za kitabibu kuthibitisha kuwa watakosa huduma ya nyota wao Mzambia, Joshua Mutale kwa kipindi kinachokadiriwa kuwa ni wiki mbili.
Mutale alipata majeraha hayo baada ya kuchezewa madhambi na mlinzi wa Tabora United hali iliyopelekea kushindwa kuendelea na mchezo na kutolewa dakika ya 31 baada ya kupata maumivu ya mguu.
Kufuatia majera hayo, Mutale amefanyiwa vipimo na imebainika kuwa majeraha yake si makubwa, hivyo anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki mbili, kabla ya kurejea tena kujiunga na wenzake kwa ajili ya kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu Bara na mashindano mengine.
MWANZO BORA WA MSIMO

Baada ya kuwa na ukame wa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu mfululizo, Simba ambao wamewahi kuwa na udhamini mnono wa Kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa msimu huu wanaonekaa kudhamiria kurudisha ubingwa huo hasa baada ya kuanza kwa kishindo msimu mpya wakifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United. Mchezo huo wa ufunguzi kwa Simba kwenye Ligi Kuu Bara 2024/25 uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo wa kipindi cha kwanza timu zote zilicheza kwa tahadhari kubwa kuhakikisha hazifanyi makosa, huku Simba wakiwa na utawala mkubwa katika kipindi kirefu cha mchezo huo. Utawala huo wa mchezo ukawapa bao la kuongoza kupitia kwa mlinzi wa kati wa timu hiyo raia wa Cameroon, Che Fondoh Malone ambaye alifunga bao kwa kichwa dakika ya 13 baada ya kumalizia mpira wqa kona uliopigwa na kiungo Jean Charles Ahoua.
Kipindi cha Simba walirudi kwa kasi wakifanikiwa kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Tabora United na straika mpya, Valentino Mashaka aliipa Simba bao la pili dakika ya 68 akiunganisha kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ kabla ya bao la tatu la Simba kuwekwa kambani na kiungo wao mpya Awesu Awesu dakika ya 92.
Katika mchezo huo kikosi cha Simba kilichoanza ni; Camara, Kapombe (Kijili 71′), Zimbwe Jr, Che Malone, Hamza, Mzamiru (Okajepha 71′), Balua, Fernandes, Mukwala (Mashaka 57′), Ahoua (Kibu 57′), Mutale (Awesu 31′)
SIMBA KILELENI MWA MSIMAMO

Kufuatia matokeo hayo, Simba wamefanikiwa kushika usukani wa msimamo wa ligi mpaka sasa licha ya kwamba sehemu kubwa ya timu shiriki bado hazijacheza mechi zao wakiwemo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga.
Simba wanaongoza msimamo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, hii ni baada ya kuandikisha mabao matatu, bila kuruhusu bao lolote langoni mwao, hivyo kuandikisha ‘Clean Sheet’ ya kwanza msimu huu.
KOCHA FADLU ANAUTAKA UBINGWA SIMBA

Mara baada ya matokeo hayo ya ushindi katika mchezo wa ufunguzi, Simba wameanza tambo kuwa safari ndiyo imeanza na wamejipanga kuhakikisha wanashinda michezo iliyo mbele yao na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kushinda ubingwa msimu huu.
Akizungumzia kikosi chake kocha mkuu wa Wekundu wa Msimbazi, Fadlu Davids amesema: “Tumepata wiki sita za mazoezi pamoja na kucheza mechi kadhaa za kirafiki pamoja na zile za mashindano ya Ngao ya Jamii, hivyo ni wazi tupo tayari kwa Ligi Kuu.
“Malengo yetu kuelekea mchezo wa kwanza dhidi ya Tabora ilikuwa kuhakikisha tunaanza vizuri ligi kwa ushindi na tunashukuru kufanikisha hilo, tumekitazama kikosi chetu na kuridhishwa kuwa tupo kwenye umbo bora la kiushindani na mawasiliano ndani ya uwanjani yameendelea kuimarika, dhidi ya Tabora mchezo tuliupa umuhimu mkubwa na malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda kila mechi ili kujiweka sawa kwenye harakati za kupigania taji la ubingwa,” amesema Kocha Fadlu.
Kocha, Fadlu pia alimzungumzia straika wake mpya, Lionel Ateba ambapo ameweka wazi kuwa nyota huyo anaendelea na uangalizi maalum wa programu za utimamu wa mwili kutokana na kuchelewa kujiunga na wenzake na atakapokuwa tayari basi Wanasimba wataanza kumuona akiuwasha moto uwanjani.

