Aucho v FeiAucho v Fei

MABINGWA wa Ligi Kuu Bara mara 30 wakiwa na rekodi ya kucheza jumla ya mechi 49 bila kufungwa na kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho 2022/23 Yanga wameendeleza balaa lao.

Yanga inadhaminiwa na kampuni ya SportPesa imeanza msimu wa 2024/25 ikitwaa taji la kwanza Bongo na ikumbukwe kwamba kuna moja ilitwaa ugenini ilipoalikwa kwenye Toyota Cup.

Mabingwa Ngao
MABINGWA Ngao ya Jamii 2024/25 Yanga. Source: Yanga.

Kwenye Toyota Cup, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambayo inafundishwa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi ambaye aliwahi kuifundisha Yanga na ni yeye alikuwa benchi wakati timu hiyo ikitinga hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika.

MABINGWA WA NGAO 2024/25

Kwenye fainali ya Agosti 11 2024 Uwanja wa Mkapa Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Azam FC matajiri wa Dar. Mabao matano yamefungwa kwenye fainali huku kila bao likitoka kwa mfungaji mmojammoja kwenye fainali iliyokuwa na ushindani mkubwa.

Bao pekee la Azam FC lilifungwa na Feisal Salum alianza kufunga dakika ya 13 lilikuwa ni bao pekee kwa Azam FC lilidumu mpaka mwisho wa mchezo huo.

MABINGWA NA MABAO YAO

Ki na Nzengeli
MABINGWA Ngao ya Jamii 2024/25 Yanga wakishangilia moja ya bao lililofungwa na Aziz Ki. Source: Yanga.

Mabingwa Yanga chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi walianza kuweka usawa kupitia kwa Prince Dube nyota wa zamani wa Azam FC ambaye huyu aliweka usawa dakika ya 18, Chadrack Boka dakika ya 27, Aziz Ki dakika ya 30 na msumari wa mwisho ni kazi ya Clement Mzize dakika ya 90.

Prince Dube amesema ni furaha kubwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii kwa kuwa walishirikiana kufanya kazi kubwa uwanjani na mwisho wakatwaa taji hilo.

“Ilikuwa ni kazi kubwa na tumefurahi kuona hili linatokea kwa kuwa tumeshirikiana kila mchezaji kuona tunapata ushindi. Pasi ambayo ilitoka kwa Mudathir, (Yahya) ilikuwa nzuri na anajua namna ambavyo ninapaswa kupewa kwa kuwa tuliwahi kucheza naye.”

AZAM FC WAZUNGUMZIA KUKOSA UBINGWA

 

Fei
KIUNGO wa Azam FC Feisal Salum akishangilia moja ya bao dhidi ya Yanga. Source: Azam.

Hasheem Ibwe, Ofisa Habari wa Azam FC ameweka wazi kuwa wamepoteza mchezo lakini walikuwa bora hivyo wapinzani wao wasifikiri timu hiyo inafungika kirahisi hilo wasahau.

“Tumepoteza mbele ya mpinzani wetu hilo ni matokeo lakini kwenye ubora sisi tulikuwa bora. Timu bora imepoteza mbele ya mpinzani ambaye ametumia makosa yetu kipindi cha kwanza hilo lipo wazi.”

SIMBA WASHINDI WA TATU, USHAMBULIAJI KUGUMU

SIMBA
MABINGWA wa Ngao ni Yanga, Azam FC nafasi ya pili, Simba nafasi ya tatu na Coastal Union nafasi ya nne. Source: Simba.

Chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids Simba imegotea nafasi ya tatu Ngao ya Jamii huku nafasi ya kwanza ni Yanga, pili Azam FC, Simba tatu na nne ipo mikononi mwa Coastal Union ya Tanga.

Kwenye mchezo wa kusaka mshindi wa tatu bao pekee la ushindi lilifungwa na Saleh Karabaka ilikuwa  dakika ya 10 Uwanja wa Mkapa na lilidumu mpaka mwisho wa mchezo.

Uongozi wa Simba umebainisha kuwa kuna tatizo kubwa kwenye eneo la ushambuliaji jambo ambalo linafanyiwa kazi kwa ukaribu na uongozi wa timu hiyo ili kuwa imara kwenye eneo hilo katika mechi za ushindani.

Wakati safu ya ushambuliaji ikifunga jumla ya bao moja ndani ya dakika 180 kwenye mechi mbili za ushindani ukuta umeruhusu bao moja pia ilikuwa Kariakoo Dabi katika hatua ya nusu fainali na mfungaji alikuwa ni Maxi Nzengeli dakika ya 44.

Ligi Kuu Bara inarejea baada ya msimu wa 2023/24 kugota mwisho na bingwa kuwa Yanga. Ni pointi 80 ilifikisha Yanga baada ya mechi 30 kukamilika.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika ujumbe huu: “Nimewatazama wapinzani wote msimu huu naiona Simba yetu ikifanya maajabu ya dunia.

“Mpaka sasa Simba ndio timu yenye wachezaji bora wenye viwango vikubwa mno, kilichobaki ni mwalimu kutengeneza timu yenye mtiririko, muunganiko na maelewano ya pamoja. Eneo pekee linalohotaji nguvu mpya ya nje ni eneo la ushambuliaji nalo viongozi wetu wanakamilisha mpango hivi punde.

“Wanasimba tuwe na subira tumpe nafasi mwalimu wa kufanya kazi yake tutakapoanza kula matunda ya furaha kila mtu atapata tunda lake. Ubaya Ubwela unaenda kukamilika.”

Share this: