
KUELEKEA maadhimisho ya kilele cha wiki ya Mwananchi ambacho kinatarajiwa kuadhimishwa rasmi Jumapili ya Agosti 4, mwaka huu, uongozi wa Yanga kwa kushirikiana na Kampuni ya SportPesa ambao ni wadhamini wao wakuu wametangaza tukio kubwa la Supu day siku ya Jumamosi ya Agosti 3, mwaka huu.
Yanga Jumapili hii wanatarajiwa kuwa na tukio kubwa la kilele cha wiki ya Mwananchi ambapo kupitia tukio hilo wanatarajia kutangaza rasmi kikosi chao kwa msimu ujao ambapo pia kunatarajiwa kuwa na burudani mbalimbali pamoja na kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki ambapo kwa mwaka huu wanatarajia kuvaana na Red Arrows.
HAJI MANARA ALICHOSEMA KUHUSU WIKI YA MWANANCHI

Klabu ya Yanga kupitia kwa Msemaji wake, Haji Manara imetangaza kuwa katika kilele cha wiki ya mwananchi wanatarajia kucheza dhidi ya Mabingwa wa Michuano ya KAGAME Cup kutokea Zambia, Red Arrows kutoka Zambia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
“Niwape habari njema kwa mashabiki wa Yanga ni kuwa, Mshindi wa Kagame Cup Red Arrows ndio tutakaocheza nao kwenye mchezo wa siku ya Mwananchi Pale Benjamini Mkapa. Wote mnafahamu ukubwa wa Red Arrows ya Zambia, wamesema watakuja na Ndege yao ya kijeshi kama ilivyo kawaida yao.” Amesema Haji Manara.
SPORPESA WATANGAZA SUPU DAY
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumanne kwenye hoteli ya Serena, Dar es Salaam, wadhamini wakuu wa Yanga SportPesa kupitia kwa Mkurugenzi wa Mahusiano wa TZ Sportpesa, Sabrina Msuya umesema “Sisi kama wadhamini wakuu tutakuwa pamoja kwenye supu day siku ya jumamosi, Kampuni ya SportPesa imeandaa supu kwa wananchi wakiwa wanajiandaa kupata burudani kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi.”
Naye Meneja Masoko wa TZ Sportpesa, Tracy Humplick amesema “Tumeandaa Kampeni maalumu kwa mashabiki wote wa Yanga Sc, tutakuwa tunagawa jezi mpya za msimu huu kama zawadi kwa mashabiki wa Yanga Sc kuelekea kilele cha wiki ya Mwananchi”
WADHAMINI WA WIKI YA MWANANCHI WATANGAZWA
Kuelekea tukio hilo kubwa na kihistoria uongozi wa timu hiyo tayari umewaweka wazi wadhamini wao wa tukio hilo ambapo kupitia kwa Mkurugenzi wa Sheria wa timu hiyo, Simon Patrick amesema “Tumekuja hapa kuwatangazia wadhamini wetu kuelekea kilele cha wiki ya Mwananchi, ambapo mdhamini mkuu wa wiki ya mwananchi ataendelea kuwa benki ya CRDB, lakini pia tumeongeza tumeongeza washirika wengine ambao ni Benki ya Equity pamoja na GSM Beverage.
“Tunashukuru sana Uongozi wa GSM Group kwa kutambua umuhimu wa kuongeza nguvu ya udhamini kwa klabu yetu, Kampuni hii ya vinywaji visivyo na kileo kama juisi, soda na maji itakuwa sehemu ya wadhamini wetu kwa kipindi hicho cha miaka mitano.”
GSM BEVERAGES WANASEMAJE?
Kupitia kwa Mtendaji Mkuu wa GSM Group, Benson Mahenya uongozi wa Kmpuni hiyo umesema “Kwa niaba ya GSM Group tunayo furaha ya kutangaza rasmi kuwa tumepanua wigo wa mahusiano yetu na klabu ya Yanga SC, tunatangaza rasmi kuwa kampuni mpya ya vinywaji ya GSM imeingia mkataba wa miaka mitano na klabu ya Yanga SC, na mkataba huu una thamani ya Tsh bilion 1.”
Nao wadhamini wakuuu benki ya CRDB kupitia kwa Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam, Muhumuliza Buberwa umesema “Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama nitashindwa kuwapongeza Yanga kwa jitihada kubwa ambayo wameifanya kwenye maendeleo ya soka, tunayo furaha kuwatangazia kuwa tutakuwa pamoja kama mdhamini mkuu wa wiki ya Mwananchi, jambo la muhimu sana katika wiki hii kuna shughuli mbalimbali ambazo zimetangazwa jana. Katika hayo maeneo yote tutatoa huduma zote za kibenki ikiwemo kupata kadi yako ya uanachama”
KIKOSI CHAREJEA KUTOKA AFRIKA KUSINI

Kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga Jumanne hii wamerejea rasmi Tanzania kutokea Afrika Kusini ambapo walikuwa kwenye ziara fupi ya maandalizi ya kabla ya msimu yaani pre-season ambapo wakiwa huko walicheza michezo mitatu wakishinda mechi mbili na kupoteza mchezo mmoja.
Yanga pia wamefanikiwa kurejea nchini wakiwa na ubingwa wa Kombe la Toyota ambalo walilitwaa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs.

