
Kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga Jumapili hii wametangazwa rasmi kuwa mabingwa wa mashindano maalum ya Kombe Toyota yaliyofanyika huko nchini Afrika Kusini.
Yanga wamefanikiwa kuibuka na ubingwa huo baada ya kuishushia kipigo cha mabao 4-0 wenyeji wao Kaizer Chiefs mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa TOYOTA Free State.
Katika mchezo huo magoli ya Yanga yalifungwa na Stephanie Aziz Ki aliyefunga mabao mawili, Clement Mzize na Prince Dube.
YANGA MECHI 3, USHINDI 2 KIPIGO 1

Baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Aughsburg katika mchezo wao wa kwanza wa maandalizi ya kabla ya msimu, Wananchi hawakutaka kuwa wanyonge katika michezo yao miwili iliyofuata ambapo walianza kwa kuvaana na TX Galaxy ya Afrika ya Kusini na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Wananchi waliibuka na ushindi katika mchezo huo ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Kanyamazane nchini Afrika Kusini ukiwa ni mchezo wa pili kwao kwenye ziara yao ya wiki mbili nchini Afrika Kusini.
Bao pekee la Yanga lilifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Prince Dube.
Wakiwa nchini Afrika Kusini, Yanga wamefanikiwa kucheza mechi tatu za kirafiki ambapo wamemaliza ratiba yao leo Jumapili kwa kushiriki mashindano ya Kombe la Toyota wakivaana na Kaizer Chiefs katika mchezo wao wa mwisho wa kirafiki.
Kikosi cha Yanga ambacho kinadhaminiwa na Kampuni ya michezo ya Kubashiri ya SportPesa kililazimika kukatisha kambi yake ya maandalizi ya kabla ya msimu ‘Pre-season’ ambayo ilikuwa ikiendelea Avic Town, Kigamboni Dar es Salaam.
Mwaliko huu ni kutoka ndani ya kikosi cha timu ya Kaizer Chiefs ambao wamekuwa na mahusiano nao ya ukaribu katika masuala ya kiuongozi na uendeshaji wa klabu ambapo ikumbukwe msimu uliopita Kaizer Chiefs walialikwa na Yanga kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kuadhimisha kilele cha wiki ya Wananchi, mchezo ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
KOCHA YANGA ATUMA SALAMU SIMBA

Katika kile ambacho kinaweza kuelezewa kuwa ni kama anawatumia salamu watan zao wa jadi Simba, alipozungumzia maandalizi ya kikosi chao Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi amesema: “Ukubwa wa timu yetu ndio umeifanya leo hii tumepata mialiko mikubwa nje ya Tanzania ambapo tunacheza michezo ya kirafiki.
“Kwa jinsi ambavyo tumecheza mechi zetu tatu dhidi ya FC AUGSBURG, TX Galaxy na Kaizer Chiefs nadhani tumeonyesha kiwango bora na tunaweza kujua tupo wapi na wapi tunaelekea. “Michezo hii kwetu ni sehemu ya maandalizi ya Kampeni yetu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ambapo malengo yetu makubwa ni kuhakikisha tunaandika rekodi ya kufika mbali katika mashindano hayo na ikiwezekana kushinda ubingwa.
“Kikosi chote kilikuwa na ari kubwa ya kuandika historia katika ziara hii na najivunia maingizo ya wachezaji wetu wapya ambao ni sehemu ya maboresho ya kikosi chetu kuelekea msimu ujao wa 2024/25.”
YAWAJIBU SIMBA UZINDUZI WA JEZI MPYA 2024/25
Baada ya Jumatano ya wiki iliyopita uongozi wa Simba kuteka mitandao ya kijamii kwa kufanya uzinduzi mkubwa wa jezi zao mpya kwa msimu ujao, ni kama uongozi wa watani zao wa jadi Yanga umekuja juu na moto wa hatari baada ya kufanya uzinduzi wa aina yake wa jezi zao za msimu ujao.
Ikumbukwe Simba wao walifanya uzinduzi wa jezi zao katika hifadhi ya Wanyamapori ya Mikumi mkoani Morogoro ambapo jezi hizo zimekuja katika rangi tatu ambazo ni bluu, nyeupe na nyekundu.
Katika jezi hizo jezi ya rangi nyekundu inatarajiwa kuwa jezo ya nyumbani, jezi ya rangi nyeupe itakuwa jezi ya ugenini na jezi ya bluu ikiwa ni jezi ya tatu ‘third kit’.
Uzinduzi wa jezi hizo za Simba ulifanywa na Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Imani Kajula, mwenyekiti wao wa zamani Mzee Hassan Dalali na Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally.
Tukio hilo lilienda sambamba na uzinduzi wa Wiki ya Simba ambao ulifanyika katika Stendi ya Mabasi Morogoro, huku Wanasimba kutokana maeneo mbalimbali ndani ya nje ya mkoa huo wakihudhuria.
JEZI YANGA ZAFUNIKA
Kabla ya uzinduzi wa jezi hizo Ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe aliponukuliwa akisema: “Somo Lingine kubwa Tutalitoa Msimu huu ambalo ni, tofauti ya Uzinduzi wa Kisasa wa Jezi na kuzururisha Vijora Mitaani, pia tofauti ya Jezi za Football na Vitambaa vya Sanda Itaonekana.”
SPORTPESA KUTAWALA KIFUANI

Kampuni bora kabisa ya michezo ya kubashiri ya SportPesa ambao ndio wadhamini wakuu wa Yanga wanatarajiwa kuendelea kutawala eneo la kifuani kwenye jezi hizo mpya.

