
Baada ya Jumatano ya wiki hii uongozi wa Simba kuteka mitandao ya kijamii kwa kufanya uzinduzi mkubwa wa jezi zao mpya kwa msimu ujao, uongozi wa watani zao wa jadi Yanga umekuja juu na kutangaza kufanya tukio kubwa la uzinduzi wa jezi zao.
Simba ambao walifanya uzinduzi wa jezi zao katika hifadhi ya Wanyamapori ya Mikumi mkoani Morogoro tayari wamefanya uzinduzi wa jezi zao za msimu ujao ambapo jezi hizo zimekuja katika rangi tatu ambazo ni bluu, nyeupe na nyekundu.
Katika jezi hizo jezi ya rangi nyekundu inatarajiwa kuwa jezo ya nyumbani, jezi ya rangi nyeupe itakuwa jezi ya ugenini na jezi ya bluu ikiwa ni jezi ya tatu ‘third kit’.
Uzinduzi wa jezi hizo za Simba ulifanywa na Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Imani Kajula, mwenyekiti wao wa zamani Mzee Hassan Dalali na Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally.
Uongozi wa Simba umeweka wazi kuwa baada ya uzinduzi jezi hizo tayari zimeanza kuuzwa kwenye maduka yote ya mdhamini wao katika utengenezaji wa jezi Sandaland The Only One nchi nzima.
Msafara wa Simba kwenda Morogoro uliongozwa na Mtendaji wao Mkuu, Imani Kajula ambaye aliongozana na Viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na Viongozi kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC).
Tukio hilo lilienda sambamba na uzinduzi wa Wiki ya Simba ambao ulifanyika katika Stendi ya Mabasi Morogoro, huku Wanasimba kutokana maeneo mbalimbali ndani ya nje ya mkoa huo wakihudhuria, huku safari ya Wanasimba ikianzia Kituo cha Treni ya Mwendokasi (SGR) hadi Morogoro.
YANGA WANASEMAJE?

Kufuatia shughuli hiyo ya Watani wao Simba uongozi wa Yanga kupitia kwa Ofisa habari wa timu yao, Ally Kamwe amesema: “Somo Lingine kubwa Tutalitoa Msimu huu ambalo ni; Tofauti ya Uzinduzi wa Kisasa wa Jezi na kuzururisha Vijora Mitaani, pia tofauti ya Jezi za Football na Vitambaa vya Sanda Itaonekana.”
“Weka oda yako mapema Mwananchi huu Uzi wa msimu huu ukichelewa kuuvaa utajilaumu sana, siku zimebaki chache sana.”
SPORTPESA KUTAWALA KIFUANI

Kampuni bora kabisa ya michezo ya kubashiri ya SportPesa ambao ndio wadhamini wakuu wa Yanga wanatarajiwa kuendelea kutawala eneo la kifuani kwenye jezi hizo mpya.
KIKOSI KINAENDELEA KUWASHA MOTO SAUZI
Baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Aughsburg katika mchezo wao wa kwanza wa maandalizi ya kabla ya msimu, Wananchi hawakutaka kuwa wanyonge katika mchezo wao wa pili ambapo walivaana na TX Galaxy ya Afrika ya Kusini na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Wananchi waliibuka na ushindi katika mchezo huo ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Kanyamazane nchini Afrika Kusini ukiwa ni mchezo wa pili kwao kwenye ziara yao ya wiki mbili nchini Afrika Kusini.
Bao pekee la Yanga lilifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Prince Dube.
Wakiwa nchini Afrika Kusini, Yanga wanatarajiwa kucheza mechi tatu za kirafiki ambapo pia watashiriki mashindano ya Kombe la Toyota wakivaana na Kaizer Chiefs katika mchezo wao wa mwisho wa kirafiki.
Kikosi cha Yanga ambacho kinadhaminiwa na Kampuni ya michezo ya Kubashiri ya SportPesa kimelazimika kukatisha kambi yake ya maandalizi ya kabla ya msimu ‘Pre-season’ ambayo ilikuwa ikiendelea Avic Town, Kigamboni Dar es Salaam.
Mwaliko huu ni kutoka ndani ya kikosi cha timu ya Kaizer Chiefs ambao wamekuwa na mahusiano nao ya ukaribu katika masuala ya kiuongozi na uendeshaji wa klabu ambapo ikumbukwe msimu uliopita Kaizer Chiefs walialikwa na Yanga kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kuadhimisha kilele cha wiki ya Wananchi, mchezo ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
KOCHA YANGA ATAMBA NA UBORA WA KIKOSI
Akizungumzia maandalizi ya kikosi chao Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi amesema: “Ukubwa wa timu yetu ndio umeifanya leo hii tumepata mialiko mikubwa nje ya Tanzania ambapo tunacheza michezo ya kirafiki.
“Kwa jinsi ambavyo tulicheza na FC AUGSBURG na TX Galaxy nadhani tulionyesha kiwango bora na tunaweza kujua tupo wapi na wapi tunaelekea.
“Michezo hii kwetu ni sehemu ya maandalizi ya Kampeni yetu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ambapo malengo yetu makubwa ni kuhakikisha tunaandika rekodi ya kufika mbali katika mashindano hayo na ikiwezekana kushinda ubingwa.
“Kikosi chote kina ari kubwa ya kuandika historia katika ziara hii na najivunia maingizo ya wachezaji wetu wapya ambao ni sehemu ya maboresho ya kikosi chetu kuelekea msimu ujao wa 2024/25.”

