
NGOMA ni nzito kuelekea msimu wa 2024/25 ambapo kila timu kwa sasa ipo chimbo kusuka mitambo ya kazi itakayoendeleza balaa uwanjani kwenye mashindano ya kitaifa na kimataifa sio Simba, Yanga, Azam FC bali kila kona timu zinaendelea kujipanga vema.
Yote yakitokea ipo wazi kwamba kwa 2023/24 ni Yanga walitwaa CRDB, NBC chini ya Kocha Mkuu Miguel Gamondi ambaye bado yupo ndani ya timu hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya SportPesa.
Mbali na kutwaa taji la ligi iligotea hatua ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Kuelekea msimu mpya ilikuwa Afrika Kusini huko ilicheza mechi tatu za kirafiki, ilipoteza mchezo mmoja na ushindi kwenye mechi mbili mfululizo.
NGOMA MPYA ZIMEANZA KUJIBU

Ngoma mpya ambazo zimetambulishwa ndani ya Yanga kuelekea msimu mpya unaotarajiwa kuanza Agosti 16 zimeanza kujibu kwa kufunga mabao kwenye mechi ambazo Yanga ilicheza ndani ya uwanja nchini Afrika Kusini.
Prince Dube ingizo jipya ndani ya Yanga kafunga mabao mawili kwenye mechi mbili mfululizo akifunga bao mojamoja. Ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya TS Galaxy na Kaizer Chiefs Dube alifungua ukurasa kwa kufunga bao mojamoja katika mechi hizo.
Ingizo jipya Jean Baleke ambaye aliwahi kucheza Simba kwenye mchezo dhidi ya FC Ausburg yeye alifunga bao moja wakati Yanga ikipoteza kwa kufungwa mabao 2-1.
NGOMA YA AZAM INASUKWA HUKO
Azam FC sio kinyonge nao pia wanaendelea kusuka mitambo ya kazi kuelekea msimu mpya huku wakiwa na maingizo mapya, wale waliokuwa ndani ya kikosi kwa msimu wa 2023/24 miongoni mwao ni Feisal Salum, Mohamed Mustafa ambaye ni kipa aliyekuwa kwa mkopo na sasa ni mali ya Azam FC kwa kuwa wameshamalizana naye.
Julai 16 2024 Azam FC walimtangaza nyota mpya ambaye ni kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Mali, Cheickna Diakite kuwa ni ingizo jipya baada ya matajiri hao kumnunua kutoka miamba ya Real Bamako. Nyota huyo chipukizi, 19, aliyepachikwa jina la staa wa Real Madrid Mbappe, kutokana na kasi na uwezo wake wa kuipenya safu ya ulinzi ya timu pinzani, amesaini mkataba wa miaka mitatu utakaomfanya kudumu ndani viunga vya Azam Complex hadi mwaka 2027.
NGOMA ZA KIRAFIKI ZINAPIGWA

Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Bruno Ferry bado wapo Morocco na kuna mechi za kirafiki ambazo walicheza ikiwa ni maalumu kwa ajili ya kutambua uwezo wao ili kuwa bora zaidi uwanjani katika mechi za ushindani.
Ikumbukwe kwamba Azam FC watapeperusha bendera ya Tanzania katika anga la kimataifa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kugotea nafasi ya pili na pointi zao 69.
Julai 29 2024 wanatarajia kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Wydad AC unaotarajiwa kuwa saa 2:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na kati.
Julai 27 2024 Azam FC ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Touarga ulikamilika kwa kutoshana nguvu ya bao 1-1. Julai 20 2024 Azam FC walicheza mchezo wa kirafiki ambapo mwisho ubao ulisoma Azam FC 3-0 US Mansour. Huu ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa Azam FC kucheza mchezo wa kirafiki baada ya kuweka kambi nchini Morocco ikiwa ni maandalizi ya msimu wa 2024/25 unaotarajiwa kuanza Agosti 16 2024.
Bruno amebainisha kuwa kila mchezo ambao wanacheza ni muhimu kutazama maendeleo ya wachezaji huku akiridhishwa na mwendo wa wachezaji katika mechi ambazo wamecheza.
“Mechi ambazo tunacheza ni muhimu kuendelea kuwa imara. Ninafurahishwa na uwezo wa wachezaji na matumaini ni kuendelea kuwa bora zaidi kwa mechi zinazofuata.”
FOUNTAIN GATE WAMO

Wakati Simba wakija na Simba Day Agosti 3 2024. Yanga wakiwa na Mwananchi Day Agosti 4 2024 matamasha haya yote yanatarajiwa kwa Uwanja wa Mkapa. Fountain Gate inayodhaminiwa na SportPesa Agosti 9 wanajambo lao.
Kupitia kwa Ofisa Habari Issa Liponda maarufu kama Issa Mbuzi amesema: “Tukutane Agosti 9 2024 Tanzanite Kwaraa Stadium, ishakuwa Mbwai acha iwe mbwai tu.
“Siku hiyo itakuwa maalumu kwa ajili ya utambulisho wa wachezaji wapya watakaopeperusha bendera kwenye mechi za ushindani na kutakuwa na mchezo wa kirafiki hivyo sio ya kukosa kila kitu kinakwenda vema.”

