skip to Main Content
Je Simba Kuandika Historia Maya Dhidi Ya Wydad Kimataifa Afrika?
WydadSimba -

Je Simba kuandika historia maya dhidi ya Wydad kimataifa Afrika?

Hatma ya Simba kuandikisha rekodi ya kufuzu kucheza nusu fainali ya Klabu bingwa Afrika itafahamika Ijumaa hii katika dimba la mfalme wa 5 huko nchini Morocco, itakapoumana dhidi ya mabingwa watetezi Wydad Athletic Club.

Itakuwa ni mechi ya kisasi kwani mabingwa watetezi walipoteza kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa kwenye ardhi ya Dokta Samia Suluhu Hassan namaanisha nchini Tanzania Jumamosi iliyopita, ambapo mnyama aliunguruma kwa ushindi wa ba 1-0, lililofungwa na mchezaji Jean Baleke.

Simba itakuwa majaribuni kujaribu kuondosha dhana ya kushindwa kuwika ugenini kwenye hatua kama hizi kwani hakuna mchezo war obo fainali ambao wamefanikiwa kushinda ugenini ndani ya misimu mitano iliyopita.

Ikumbukwe wekundu wa msimbazi wamefuzu robo fainali nne za michuano ya CAF,na zote hawajawahi kuwa na tatizo la kupata matokeo chanya nyumbani lakini tatizo limekuwa ni kumaliza mchezo kwenye viwanja vya ugenini.

Kuweka kumbukumbu sawa tangu Mohamed Dewji aichukue Simba wamecheza robo fainali 4. Ya kwanza ilikuwa dhidi ya TP Mazembe na mchezo wa mkondo wa kwanza ulipigwa Jijini Dar es salaam kwa Mkapa mnamo Aprili 16, 2019 na hakukuwa na mbabe na matokeo yalikuwa 0-0.

Mchezo wa mkondo wa pili ulipigwa huko Lubumbashi nchini Congo, ambapo licha ya Simba kupata bao la uongozi la mapema lililofungwa na Emmanuel Okwi, lakini walijikuta wakicharazwa bakora 4-1 na kutupwa nje ya michuano ya Klabu bingwa Afrika na kuwaacha TP Mazembe wakisonga hatua ya nusu fainali.

Safari ya mnyama haikuishia hapo, msimu uliofuata waliduwazwa na UD Songo na kuondolewa mapema kwenye kinyang’anyiro cha michuano hiyo, lakini msimu uliofuatia walijifunga kibwebwe na hatimaye walitinga robo fainali ambapo walikutana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Mchezo wa mkondo wa kwanza wa Mei 15,2021, Simba ilichezea kichapo cha bao 4-0 huko Afrika Kusini lakini waliporejea nchini kwenye mchezo wa marudiano uliopigwa Mei 22,2021, mnyama aliunguruma kwa ushindi wa mabao 3-0 huku John Bocco aking’ara kwa kucheka na nyavu mara mbili lakini haikutosha kuwavusha kuelekea nusu fainali baada ya matokeo ya jumla kuwavusha Kaizer kwa bao 4-3.

Msimu wa mbele yake, Simba haikufua dafu kwenye michuano ya Klabu bingwa baada ya kuondolewa kwa mshtuko na Jwanning Galaxy ya Botswana tena kwa Mkapa kwa bao 3-1 licha ya ushindi wa ugenini wa bao 2-0. Simba walicheza hatua ya mtoano na kutinga kwenye kombe la Shirikisho ambalo walifuzu robo fainali na mpinzani wao alikuwa Orlando Pirates.

April 17,2022 Simba ilikuwa mwenyeji wa mchezo wa mkondo wa kwanza na wakaibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0 lililokwamishwa kambani na beki Shomari Kapombe lakini katika mbungi la marudiano lililopigwa nchini Afrika Kusini April 23-2022, Orlando walishinda kwa penati 4-3 baada ya mchezo kumalizika kwa wenyeji kupata ushindi wa bao 1-0.

Katika mchezo huo Simba iliathirika baada ya aliyekuwa mshambuliaji wake,Chriss Mugalu kuonyeshwa kadi nyekundu.

Ukifuatilia mwenendo wa matokeo ya Simba katika harakati zake inaonyesha haijawahi kutatizika kwenye mechi za nyumbani kwenye hatua ya robo fainali kwani imeshinda michezo mitatu na suluhu mmoja lakini imepokea vipigo vitatu ugenini, tena kwa idadi kubwa ya mabao, ikiwa imeruhusu mabao 9.

Viongozi wa Klabu ya Simba wanakiri kwamba droo ya msimu huu kwenye hatua ya robo fainali ni ngumu zaidi kuliko ile waliyoapangiwa dhidi ya Tp Mazembe, Kaizer Chiefs na Orlando Pirates.

Kwa hatua hii ya sasa wanakabiliana na bingwa mtetezi ambaye si rahisi sana kukubali kutolewa katika hatua kama hii.

Baada ya dakika tisini za mchezo wa kwanza, Rais wa heshima wa Simba, Mohamed Dewji alisema ni jambo zuri kupata ushindi japokuwa walihitaji kushinda zaidi ya idadi hiyo ya mabao ambayo ingewaweka katika mazingira rafiki kuelekea mchezo wa marudiano.

‘’Tumepata ushindi dhidi ya mabingwa watetezi ni mzuri, lakini ukweli ni kwamba ni ushindi mwembamba sana, ingekuwa bora zaidi tungepata bao zaidi ya moja lakini inatubidi tujipange kwa ajili ya mchezo wa marudiano nchini Morocco’’. Alisema Mohammed Dewji.

Upande wa mmoja ya viongozi wa zamani wa bodi ya wakurugenzi wa klabu ya Simba, Mwina Kaduguda alisema, kikubwa timu ya Simba imeshinda nyumbani, na hawawezi kukubali kufungwa nyumbani na ugenini.

‘’Wydad ni kama Al Ahly hivyo kuwafunga sisi ni jambo zuri. Tunasubiri mechi ijayo tuone tutafanya nini’’. Alimalizia Kaduguda.

Wydad ni mabingwa mara tatu wa kihistoria wa michuano hii. Wydad waliwavua ubingwa timu ya Al Ahly msimu uliopita na sasa wanawania taji la nne la Klabu bingwa Afrika.

Mabingwa hawa wa Morocco hawajapoteza mchezo hata mmoja kwenye michuano ya Klabu bingwa msimu huu, vilevile hawajaruhusu bao hata moja kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Hivyo kuifanya mechi dhidi ya mnyama kuwa na mvuto wa aina yake kwani timu ya Simba itatakiwa kufanya kazi ya ziada kupata ushindi ugenini ambapo timu nyingine za Afrika zimeshindwa.

Wydad wamefunga jumla ya mabao 11 wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani, lakini nayo Simba ambayo katika mechi za ugenini msimu huu wameshinda mara tatu katika mchakato mzima tangu hatua ya awali lakini wameshinda mara moja tu katika hatua ya makundi.

Simba vs WydadKatika mchezo uliopita takwimu zilikuwa bora zaidi kwa upande wa wekundu wa msimbazi Simba. Kiwango bora kimeonekana katika maeneo mengi japokuwa hawakupata matokeo yenye magoli mengi.

Historia haiwabebi Simba kwenye ardhi ya Morocco ambapo msimu uliopita hatua ya makundi walinyukwa bao 2-0 dhidi ya RS Berkane licha ya kushinda kwa Mkapa bao 1-0.

Msimu huu kwenye makundi wamefungwa mechi zote mbili dhidi ya Raja Casablanca kwa jumla ya bao 6-1 na mchezo wa hivi karibuni huko Morocco walifungwa bao 3-1. Je Simba ataandikisha historia mpya?

Ni miaka 20 imetimia tangu Simba imuondoe bingwa mtetezi wa michuano ya klabu bingwa ambapo mwaka 2003 waliwatupa nje Zamaleki kwa penati baada ya matokeo kama haya waliyoyapata hapa Tanzania na wakafungwa nchini Misri bao 1-0.

Ni swali la wapenda kandanda nchini Tanzania ambalo litaulizwa siku ya kesho jijini Casablance. Je Simba kuandika historia katika ardhi ya ugenini katika michezo ya klabu bingwa Afrika.

Weka ubashiri wako kupitia tovuti yetu ya sportpesa.co.tz au piga *150*87#

Share this:
Back To Top