DABI YA MOTO SCOTLAND- CELTIC VS RANGERS -Ni patashika nguo kuchanika
Katika mwendelezo wa zile mechi kali kali za soka barani Ulaya kwa wiki hii, huwezi kuacha kuitaja mechi ya mahasimu wawili wa jadi katika ramani ya soka ya ligi kuu ya Scotland.
Timu ya Celtic itaingia uwanjani, ikiwa haijapoteza hata mechi moja, katika dimba lake la nyumbani msimu huu, wakiwa wameshinda mechi zote 15 walizocheza.
Klabu hizi mbili zinakutana wakati timu zote mbili zikiwa katika kiwango bora cha mchezo, ambapo katika mechi 5 za ligi walizocheza hivi karibuni, kila moja imepata matokeo kuvutia, huku Celtic ikiwa na rekodi nzuri zaidi ya kutopoteza kwenye dimba lake la nyumbani.
Rangers wao kwa upande wao wameshinda mechi 11 walizocheza ugenini msimu huu, kutoka sare mechi 2 na kupoteza mara 2. Mechi walizotoa sare ni pamoja na mechi baina ya St Mirren, mechi iliyochezwa Novemba 12-2022, ambapo matokeo yalikuwa(1-1)
Mechi ya sare nyingine ni baina ya Rangers dhidi ya Celtic, mechi hii ilipigwa Tarehe 2 Januari 2023 na matokeo yalikuwa (2-2).
Iwapo Celtic itashinda mchezo huo wa kesho dhidi ya Rangers, basi itaongeza wigo wa alama dhidi ya wapinzani wao hadi kufikia pointi 12. Rangers kwa upande wao iwapo watashinda watapunguza tofauti ya alama dhidi ya Celtic na kubakiza pointi 6. Sare ya aina yoyote itaendelea kufanya tofauti baina yao kuwa alama 9, zilizopo hivi sasa.
Akizungumzia mechi hiyo mmoja wa wachezaji wa zamani wa Celtics Common, ambaye kwa sasa anaandika makala katika kurasa za michezo za gazeti la Daily mail anasema kocha wa Celtic Ange Postecoglou ataitumia mechi hii kutuma salamu za ubingwa kwa timu zingine zinazoshiriki ligi kuu ya Uskochi.
‘’Natumai mechi hii itaonyesha ubora wa kocha Postecoglou, kwani tangu kuanza kwa msimu huu timu ya Celtic imekuwa bora sana na mpaka sasa, baada ya mechi hii tutapata kuona mwelekeo wa timu katika kuyachukua mataji matatu, ambayo timu ya Celtic iko katika naasi nzuri kuyanyakua’’. Alisema Common.
Akiendelea Common anasema imekuwa si jambo la kushangaza kwa timu ya Celtic kufikia ama kuwa katika hali hii ya mafanikio, kwani tangu wakati wa kocha Brenden Rogers pamoja na Martin O Neil ilikuwa ni Jamabo la kawaida kwa timu hii kushinda mataji matatu katika kila misimu waliyohudumu katika klabu.
‘’Kila mtu anajua falsafa ya kocha wetu wa sasa katika staili yake ya ufundishaji na uchezaji. Nadhani kwa siku za karibuni imekuwa ni burudani sana kukaa na kuitazama timu ikicheza mpira uwanjani. Kumekuwa na matokeo ya kufarahisha na pia nyakati ambazo ni nzuri katika mchezo wa soka nchini mwetu’’.
Common anatoa angalizo kwamba haitakuwa rahisi kwa timu ya Rangers kukubali kusalimu amri kirahisi, kwa kuwa timu hizi mbili zina upinzani wa jadi ambao hauruhusu mmoja wapo kukubali kushindwa kirahisi.
Timu hizi zinatarajiwa kukutana tena katika mechi ya kombe la nusu fainali ya U skochi (Scottish Cup Semi-final), baadae mwezi huu, akiwatabiria Celtic ya kuwa mpaka kufikia wakati huo, tayari timu hiyo itakuwa imeshatawazwa ubingwa wa ligi kuu.
Mpaka sasa timu hizi mbili zimeshacheza mechi 30 za ligi kuu kila mmoja na kwa kuangalia msimamo ulivyo Celtic anaongoza ligi akiwa na jumla ya pointi 85, akifuatiwa na Rangers wenye jumla ya pointi 76.
Kwa kuangalia takwimu wakati timu hizi zitakapokutana kesho itakuwa ni mechi ya 96 baina yao. Celtic wakiwa wameshinda jumla ya mechi 48 na Rangers akiwa ameshinda mechi 32 na kutoa sare mechi 15 baina yao.
Yote kwa yote mechi hii inategemewa kuwa ya ushindani uwanjani kwa kuwa ni Debi yenye hamasa kubwa sio tu kwa mashabiki, bali pia kwa wachezaji na benchi la ufundi kwa timu zote mbili.
Timu ya Celtic itaingia uwanjani siku ya kesho ikiwategemea wachezaji wake wenye takwimu bora za kufunga mabao, ambao ni pamoja na Kyogo Furuhashi (20), Liel Abadan na Jota kila mmoja akiwa na mabao 10.
Rangers kwa upande wao watakuwa wanawategemea wachezaji wao hatari kwa kucheka na nyavu, akiwemo Antonio Colak na James Tavenier, ambao kila mmoja ana mabao 13.
Kuangalia historia ya mechi mbali mbali tembelea hapa.

