skip to Main Content
TP MAZEMBE KULIPA KISASI KWA YANGA!
TP-Mazembe-

TP MAZEMBE KULIPA KISASI KWA YANGA!

Klabu ya soka ya Young Africans (Yanga), kesho wanatarajiwa kucheza mchezo wao wa mwisho wa hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Tout Puissant Mazembe.

Mchezo huu wa kumalizia, mechi za makundi unatarajiwa kuchezwa saa mbili kamili usiku kwenye Uwanja wa Stade De TP Mazembe uliopo katika kitongoji cha Kamalondo mji wa Lubumbashi kule DRC Congo.

Aidha mara ya mwisho kwa timu hizi mbili kukutana ilikuwa Tarehe 19 Februari 2023, ambapo, Yanga ilifanikiwa kuwafunga TP Mazembe jumla ya 3-1, katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Katika mchezo huo, mabao ya Yanga yalifungwa na Mudathiri Yahya, Kennedy Musonda na Jesus Moloko aliyekuwepo katika kiwango bora hivi sasa.

TP Mazembe katika mchezo huu wataingia uwanjani wakiwa na hasira hiyo ya kufungwa mabao 3-1, hivyo watacheza kwa nguvu kwa lengo la kulipa kisasi katika mchezo unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa.

Yanga wanatakiwa kufanya maboresho katika baadhi ya maeneo ikiwemo ya ulinzi kwa kupunguza faulo nyingi golini kwao kutokana na ubora wa wachezaji wa TP Mazembe wenye uwezo mkubwa wa kupiga mipira ya aina hiyo.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia Nasreddine Nabi amelazimika kukifanyia mabadiliko kikosi chake cha kwanza katika mchezo huu kutokana na baadhi ya wachezaji kutumikia adhabu ya kadi mbili za njano.

Wachezaji hao waliozipata kadi hizo za njano katika mchezo uliopita dhidi ya US Monastir ya nchini Tunisia uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa ambao ni pamoja na Djigui Diarra, Shaaban Djuma na Khalid Aucho.

Kutokuwepo kwa wachezaji hawa, huenda likawa pengo kubwa kwa Yanga, kutokana na umuhimu mkubwa wa wachezaji hao katika kikosi cha kwanza, kwani  wamekuwa tegemeo katika michezo iliyopita.

TP Mazembe

Nafasi ya Diarra inatarajiwa kuzibwa na kipa Metacha Mnata, wakati mchezaji namba mbili Djuma Shaaban nafasi yake itazibwa na Kibwana Shomari, huku kiungo machachari Khalid Aucho pengo lake likizibwa na Zawadi Mauya, mchezaji ambaye ana umiliki mzuri wa mpira na kupiga pasi ndefu kwa wachezaji wa mbele.

Kuelekea mchezo huu, Yanga wanatakiwa kumchunga winga wa TP Mazembe, Philippes Kinzumbi ambaye katika mchezo uliopita, alikuwa hatari katika safu ya ulinzi ya timu hiyo, ambaye ndie aliyesababisha bao lililotokana na faulo iliyopatikana nje ya 18.

Kinzumbi ni mchezaji mzuri sana, hasa hasa wakati wa kukokota mipira huku akiwapiga chenga mabeki akiwa anatokea pembeni akpeleka mashambulizi mbele. Hivyo beki wa kushoto wa Yanga Joyce Lomalisa ana kibarua kigumu cha kumzuia winga huyo.

Uzuri ni kwamba Lomalisa anafahamu vizuri Kinzumbi ambaye Mkongomani mwenzake, waliwahi kukutana wakiwa wanacheza ligi moja ya Congo.

Pia Yanga wanatakiwa kumchunga mshambuliaji wa kimatifa kutoka Zambia mkongwe Rainford Kalaba na Mercey Ngimbi, ambao wote wana uwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi za mabao kwa wachezaji wenzao.

Vita kubwa itakuwepo katika safu ya kiungo katika mchezo huu itakayowakutanisha aliyekuwa kiungo wa Yanga, Mukoko Tonombe na Mudathiri Yahya, ambaye yupo katika kiwango bora cha uchezaji hivi sasa.

Viungo hao wote wanacheza aina moja ya uchezaji ya kutumia nguvu nyingi, kila mmoja atataka kumuonyeshea mwenzake ubora wake huku Mukoko akitaka kutumia ushawishi mwingi kwa kuonyesha kiwango bora ili arejeshwe Yanga.

Akizungumzia mchezo huu, Kocha wa Yanga Nasrenadine Nabi anasema kuwa anataka kuona vijana wake wakipambana kupata pointi tatu zitakazoifanya timu iendelee kukaa kileleni katika msimamo wa ligi ya shirikisho.

“Ninafurahi kwa namna ambavyo nafasi yetu kwenye kundi hili ilivyo. Tukiweza kufanikiwa kumaliza tukiwa kileleni, tutakuwa na nafasi nzuri ya kukutana na timu za kawaida katika robo fainali ya michuano hii ya kombe la Shirikisho.

Hivyo kurahisisha kazi yetu katika mechi za hatua inayofuata, ambayo ni robo fainali, huku ikitegemewa, mshindi wa kwanza wa kundi moja anakutana na mshindi wa pili wa kundi lingine.

“Tayari nimewaambia wachezaji wangu umuhimu wa mchezo huu, kuwa ni lazima tushinde ili tujiweke katika nafasi nzuri ya kukaa kileleni na hilo linawezekana kwetu kupata ushindi katika mchezo huo,” anasema Nabi.

Share this:
Back To Top