- Simba SC inautaka ubingwa wa CAF mbele ya wapinzani wao RS Berkane.
- Ellie Mpanzu, Aishi Manula, Yusuph Kagoma, Jean Ahoua kwenye kibarua kingine nyumbani.
- RS Berkane kuwasili mapema na ndege yao binafsi kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kuikabili Simba SC fainali ya maamuzi.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC ameweka wazi kuwa mpango mkubwa wa timu hiyo ni kutwaa taji la ubingwa Afrika, (CAF) kwenye mchezo wa hatua ya pili ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco unaotarajiwa kuchezwa Mei 25 2025, Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Awali mchezo huo ulitarajiwa kuchezwa Dar, Uwanja wa Mkapa ambapo tayari viingilio vilianza kuuzwa kwa ajili ya mashabiki kushuhudia fainali ya pili. Taarifa kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika, (CAF) iliamua kuwa mchezo huo uchezwe Uwanja wa Amaan Complex.
CAF walibainisha kuwa sababu kubwa ni sehemu ya kuchezea ya Uwanja wa Mkapa kutofikia viwango ambavyo vinatakiwa kuelekea kwenye fainali hiyo jambo ambalo walielekeza mchezo uchezwe Zanzibar.
Licha ya jitihada za Serikali, Simba SC na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, (TFF) kupambania mchezo uchezwe Uwanja wa Mkapa kutokana na maboresho ambayo yamefanyika kwenye uwanja huo bado msimamo wa CAF ulibaki palepale.

CAF walitoa taarifa kwamba wanatambua jitihada ambazo zimefanyika kwa ajili ya kuuboresha uwanja huo na wanaamini viwango ambavyo vinaendelea kufanyiwa kazi vitatoa nafasi kwa uwanja huo kutumika kwenye mashindano mengine ikiwa ni pamoja na CHAN.
Inahusiana na hii: Simba SC vs RS Berkane CAF waipeleka Uwanja wa Amaan
Kuhusu tiketi zilizouzwa kwa mashabiki kuelekea fainali
Kwa mujibu wa Ahmed Ally, ameweka wazi kuwa kuna tiketi ambazo zilikuwa tayari zimeuzwa kwa mashabiki wa Simba SC kuelekea kwenye mchezo wa fainali ya pili dhidi ya RS Berkane. Baada ya kikao wameamua kusitisha zoezi la kuuza tiketi za Uwanja wa Mkapa.
“Baada ya kikao tumeamua kusitisha zoezi la kuuza tiketi za mechi ya fainali kwa Uwanja wa Mkapa. Zile tiketi zaidi ya 12,000 ambazo zipo kwa mashabiki hizi tunawaomba wazitunze watazitumia kwenye Simba Day ya 2025.

“Tukumbuke kwamba tamasha la Simba Dya 2025 linakuja. Kupitia tamasha hili mashabiki walioununua tiketi za mechi yetu ya fainali dhidi ya RS Berkane watapata fursa kuzitumia na kushudia utambulisho wa wachezaji wetu wapya na wale ambao wataendelea kuwa katika kikosi chetu. Kuelekea mchezo wa fainali Uwanja wa Amaan tumeanza kuuza tiketi mpya.”
Msafara kuibukia Zanzibar mapema
Msafara wa kikosi cha Simba SC na benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids umeanza safari kueleka Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wa hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane.
Ipo wazi kwamba katika fainali ya kwanza iliyochezwa Morocco baada ya dakika 90 ubao ulisoma RS Berkane 2-0 Simba SC. Hivyo Simba SC ina kibarua cha kusaka ushindi wa mabao 3-0 kwenye mchezo wa hatua ya fainali ya pili Uwanja wa Amaan Complex.
Miongoni mwa wachezaji waliopo kwenye msafara wa kikosi cha Simba SC ni Kibu Dennis, Mzamiru Yassin, Leonel Ateba, Fabrince Ngoma, Duchu, Jean Ahoua, Zimbwe Jr na Moussa Camara.
Kipa Aishi Manula ambaye alikosekana kwenye mchezo uliopita ugenini naye ni miongoni mwa wachezaji waliopo kwenye msafara huo unaotarajia kuanza maandalizi yake mapema Mei 21 kuelekea mchezo wa hatua ya fainali Mei 25.
Matokeo ya fainali ya kwanza RS Berkane 2-0 Simba SC
Kwenye mchezo wa kwanza ugenini uliochezwa Mei 17 2025 kwenye mchezo wa hatua ya fainali ya kwanza baada ya dakika 90 ubao ulisoma RS Berkane 2-0 Simba SC. Watupiaji kwenye mchezo huo walikuwa ni Mamadou Camara dakika ya 8 na Ousama Lamlioui dakika ya 15.

Wapinzani wa Simba SC, RS Berkane wanatarajiwa kuwasili Tanzania, Aprili 22 2025 siku ya alhamisi mapema kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo huo ambapo wanatarajiwa kuja kwa ndege yao binafsi kukamilisha dakika 90 za mchezo.
Inahusiana na hii: RS Berkane 2-0 Simba SC: Magoli, takwimu, yaliyotokea ‘haijaisha mpaka iishe’
RS Berkane ni miongoni mwa timu ambazo zina wachezaji wenye spidi kubwa uwanjani na imara kwenye matumizi ya mapigo huru hasa kona na faulo kwa kuwa hata bao la kwanza walilofunga mbele ya Simba SC lilitokana na pigo la kona lilikutana na kichwa cha Camara ambaye alimtungua kipa namba moja wa Simba SC.

