- RS Berkane 2-0 Simba SC, katika hali isiyo ya kawaida maelfu ya mashabiki wa Simba walilipuka kwa shangwe, mara baada ya kumalizika kwa mchezo huu wa fainali ya mkondo wa kwanza ya Kombe la shirikisho Afrika jana.
- Mechi ya fainali ya mkondo wa pili inayotarajiwa kupigwa nchini Tanzania itachezwa Mei 25, mwaka huu.
- Mpaka sasa katika michezo mitatu ambayo timu hizo zimekutana ikiwemo mchezo wa jana Jumamosi, Berkane wameshinda mechi 2, Simba wameshinda 1.
RS Berkane 2-0 Simba SC, ndivyo ubao wa matokeo wa Uwanja wa Manispaa ya Berkane ulionyesha baada ya mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika kumalizika, katika hali isiyo ya kawaida maelfu ya mashabiki wa Simba walilipuka kwa shangwe.
Mchezo huu ndio ulikuwa habari kubwa ya soka wikiendi hii, ambapo Simba walikuwa mgeni wa Berkane nchini Morocco, kwenye mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
RS Berkane 2-0 Simba SC; Mchezo ulikuwaje?

Kama ilivyotarajiwa mchezo ulikuwa wa ushindani mkubwa, huku timu zote mbili zikigawana vipindi. Berkane wakiuteka mchezo kipindi cha kwanza kabla ya Simba kutawala kipindi cha pili.
Ni mabao ya mapema mawili ambayo yalifungwa na Berkane kiungo, Mamadou Camara dakika ya 8 na Oussama Lamlaoui dakika ya 14 ndiyo yaliweka utofauti wa mchezo huo kwa dakika 90.
Kwa ujumla wenyeji walikuwa hatari zaidi kwa kutengeneza nafasi za kufunga na kumpa kazi kubwa kipa, Moussa Camara ambaye alifanya kazi kubwa kuokoa michomo hatari ikiwemo zile za uso kwa uso na washambuliaji wa Berkane.
SOMA HII PIA: RS Berkane vs Simba SC 17/05/2025 LIVE H2H, Vikosi, Uchambuzi, matamko Leo Kitawaka!
Dakika 6 magoli 2, yote makosa ya walinzi Simba

Simba wameadhibiwa kwa kutokuwa makini katika safu yao ya ulinzi, kwani ukiangalia magoli yote mawili ambayo wamefungwa ni makosa ya walinzi wao.
Goli la kwanza la Camara dakika ya 8 lilitokana na mpira wa kutenga wa kona ambao wachezaji, Fabrice Ngoma na Chamou Karabou walishindwa kuruka na kumpa nafasi huru ya kichwa ‘free header’ mfungaji Camara.
Goli la pili lilitokana na kiungo wa ulinzi, Yusuph Kagoma kupoteza mpira karibu na box lao la 18, huku Berkane wakitumia mpira huo kuwaadhibu Simba kwa bao la 2 la Oussama.
SOMA HII PIA: RS Berkane vs Simba SC 17/5/2025, Steven Mukwala aongoza jeshi la Simba kutua kwa kishindo Morocco
Semaji, Ahmed Ally atoa tamko zito kuelekea Simba SC vs RS Berkane 25/05/2025

Mara baada ya mchezo huo, Meneja wa Habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally ameweka wazi kuwa ngoma bado haijaisha na waarabu watatapika uongozi wa mabao yao mawili watakapokuja Tanzania.
Akizungumzia mchezo huo, Ahmed amesema: “Kwanza niwahakikishie wanasimba kuwa hatujapoteza mchezo huu, bao mbili ni chache sana na kwa uwezo wa Mungu hizi goli mbili watazitapika Uwanja wa Mkapa.
“Ukiwaangalia wachezaji wao na mashabiki wao wanajua fika kuwa hawana matumaini ya ubingwa, hasa kutokana na historia ya Simba wanapocheza Tanzania. Tunarudi nyumbani kujiandaa na mchezo wa marudiano.
“Tuna matumaini makubwa ya kuibuka na ubingwa wa mashindano haya na tunaendelea na kauli mbiu yetu kuwa Hii tunabeba na tutatumia Hashtag ya Watazitapika.”
SOMA HII PIA: Simba SC vs RS Berkane Uwanja wa Mkapa waleta sekeseke CAF, tamko latolewa
Kocha Simba acharuka asisitiza vita itakuwa kali Mei 25

Mara baada ya mchezo huo Kocha wa Simba, Fadlu akizungumzia mchezo wa marudiano amesema: “Utakuwa mchezo mgumu kuliko yote ambayo tumecheza msimu huu, tunafanyia kazi makosa tuliyofanya kuanzia hatua ya awali.
“Hatupaswi kufanya makosa hayo kwenye mchezo wa pili ambayo yanaweza kutugharimu, tunahitaji kucheza kwa umakini,” amesema Fadlu.
Kikosi cha Simba kilichoanza mchezo dhidi ya Berkane ni; Camara, Kapombe Zimbwe Jr, Chamou, Hamza, Kagoma, Kibu Ngoma, Ateba, Ahoua, Mpanzu.
Tujikumbushe mambo muhimu kuyajua kuhusu RS Berkane vs Simba SC
- Haijawahi kutokea sare timu hizo mbili zilipokutana, mara baada ya mchezo wa jana sasa wamekutana katika michezo mitatu, Simba wakishinda mechi 1 na RS Berkane wakishinda 2.
- Simba imesafiri na kikosi cha mastaa 24 kwenda Morocco ambapo ni Hamza na Kibu ndio ambao wamepata majeraha baada ya mchezo wa juzi.
- Bado kuna sintofahamu juu ya wapi mchezo wa marudiano ambao unatarajiwa kupigwa Mei 25, hii ni baada ya Caf kutangaza kuuhamishia mchezo huo, Uwanja wa Amaani Zanzibar, huku viongozi mbalimbali wa Simba wakionekana kugomea uamuzi huo.

