Ahmed Ally CoachAhmed Ally Coach
  • Simba SC ilipata ushindi kwa pigo la penati mzunguko wa kwanza dakika ya 90 kupitia kwa Jean Ahoua.
  • JKT Tanzania safu yake ya ushambuliaji imetupia mabao 24 na ukuta wao umeruhusu mabao 24.
  • Simba SC inaongoza kwa kufunga mabao mengi ya penati ndani ya ligi ambayo ni 11 katika penati 12 walizopata.

Vita ya msako wa pointi tatu inatarajiwa kupigwa leo Mei 5 2025 kwa wababe wawili JKT Tanzania chini ya Kocha Mkuu, Ahmed Ally dhidi ya Simba SC inayonolewa na Fadlu Davids Uwanja wa Isahmuyo, ikiwa ni mzunguko wa pili.

Coach Fadlu
Fadlu Davids, Kocha Mkuu wa Simba SC, 2024/25. Source: Simba SC.

Sio mchezo mwepesi kwa wababe hawa wawili kutokana na kila timu kupiga hesabu kusepa na pointi tatu mazima ndani ya uwanja baada ya dakika 90 kugota mwisho.

Mchezo uliopita kwa Simba SC ilikuwa Uwanja wa KMC Complex ilikomba pointi tatu mbele ya Mashujaa FC ubao uliposoma Simba SC 2-1 Mashujaa FC.

Ubaya wao upo hapa

Ubaya kwa wapinzani hawa upo kwenye hesabu zilizopita katika mchezo wa mzunguko wa kwanza baada ya dakika 90 ubao kusoma Simba SC 1-0 JKT Tanzania na bao la ushindi likifungwa na Jean Ahoua.

------------------------------------------------n
Jean Ahoua kiungo mshambuliaji wa Simba SC aliyefunga bao mchezo dhidi ya JKT Tanzania mzunguko wa kwanza. Source: Simba SC.

Ahoua alipachika bao hilo dakika ya 90 kwa mkwaju wa penati baada ya beki Shomari Kapombe kuchezewa faulo ndani ya 18 katika dakika za lala salama.

Ipo wazi kwamba kwenye ligi Simba SC ni namba moja kwa timu namba kwa kupata penati ikiwa imepata jumla ya penati 12 na katika hizo 7 zilipigwa na Leonel Ateba ambaye alifunga sita na kukosa moja huku tano zikifungwa na Jean Ahoua.  

Kwenye mchezo uliochezwa Desemba 24 2024 mwamuzi wa kati alikuwa ni Kepha Kayombo, aliamua adhabu ya penati kwa Simba SC baada ya Kapombe kuchezewa faulo ndani ya 18.

Dakika 90 zilizopita

Dakika 90 zilizopita kwa JKT Tanzania ilipoteza pointi tatu dhidi ya Tanzania Prisons kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine Mbeya, ilikuwa Aprili 18 2025.

Kichuya
Kichuya kiungo mshambuliaji wa JKT Tanzania ambaye aliwahi kucheza Simba SC. Source: JKT Tanzania.

Baada ya dakika 90 ilikuwa Tanzania Prisons 3-2 JKT Tanzania, ikiwa ni siku mbaya kazini kwa JKT Tanzania na kicheko kwa Tanzania Prisons waliokomba pointi tatu mazima wakiwa nyumbani.

Simba SC ilicheza na Mashujaa FC kwenye mchezo uliopita ilikuwa ni Mei 2 2025 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa KMC Complex ukasoma Simba 2-1 Mashujaa FC hivyo pointi tatu zilibaki Msimbazi.

Nafasi zao kwenye msimamo

JKT Tanzania kwenye msimamo ipo nafasi ya 7 ikiwa na pointi 32 kibindoni, ushindi ni kwenye mechi 7, sare 11 na ilipoteza mechi 8 msimu wa 2024/25 katika hizo moja ilipoteza dhidi ya Simba SC mzunguko wa kwanza.

Dotto
Dotto kocha msaidizi wa JKT Tanzania. Source: JKT Tanzania.

Safu ya ushambuliaji ya JKT Tanzania ni mabao 24 imetupia na ukuta umeruhusu mabao 24 inakutana na timu namba mbili kwenye kufunga mabao mengi ndani ya ligi.

Simba SC kwenye msimamo ni namba mbili ikiwa imetupia mabao 54 baada ya kucheza mechi 23 ndani ya ligi. Ukuta wa Simba ni namba moja kuruhusu mabao machache ambayo ni 9 baada ya mechi 23 ni pointi 60 imekusanya kibindoni.

Vinara kwenye msimamo ni Yanga SC inayonolewa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi kibindoni ina pointi 70 baada ya mechi 26.

Hawa hapa JKT Tanzania wenyewe

Raymond Dotto, kocha msaidizi wa JKT Tanzania amewea wazi kuwa kila mchezo una mbinu zake zinazotumika kwa ajili ya kupata matokeo chanya.

Dotto amebainisha kuwa wanatambua uimara wa wapinzani wao ulipo hivyo wataingia kwa mbinu ambazo watazipanga ili kupata matokeo chanya ndani ya uwanja.

“Kila mchezo una mbinu zake kwenye kutafuta matokeo, aina ya mpinzani ambaye tunakutana naye tunatambua ubora wake nasi tumejipanga ili kupata matokeo mazuri.”

Neno la Fadlu    

Fadlu Davids, Kocha Mkuu wa Simba SC amebainisha kuwa hakuna muda wakupumzika kwa sasa kutokana na kuwa na mechi ngumu ambazo zinahitaji umakini kwenye kupata matokeo.

Fadlu amebainisha kuwa kila mchezo ambao upo mbele yao ni mgumu na hawana muda wakupumzika kutokana na ratiba kuwa hivyo lazima wapambane kupata matokeo mazuri.

“Tuna mechi kila baada ya siku mbili unaona namna ilivyo hapo hakuna muda wakupumzika ni kazi kwa kazi ili kuona namna gani tunapata matokeo mazuri hakuna mchezo mwepesi kwetu.

“Wachezaji waliopo wanatambua kwamba kila mchezo kwetu ni muhimu kupata pointi tatu hivyo makosa yaliyopita tunafanyia kazi ili kuwa imara kwa mechi zijazo na mchezo wetu ujao ni dhidi ya JKT Tanzania.”

Share this: