- Yanga SC yashikilia msimamo wao palepale kuhusu mchezo namba 184 hawatashiriki kwa namna yoyote.
- TPLB yatangaza tarehe mpya ya Kariakoo Dabi kukamilisha msimu wa 2024/25.
- Kivumbi kufahamika itakuaje Juni 15 2025 siku iliypangwa na TBLP
BODI ya Ligi Kuu Tanzania Bara, (TPLB) Mei 6 2025 imetoa ratiba mpya kwa ajili ya kukamilisha msimu wa 2024/25 huku mchezo namba 184 wa Yanga SC na Simba SC ukipangwa kupigwa Juni.

Ikumbukwe kwamba mchezo huo ulitarajiwa kuchezwa Machi 8 2025 ukayeyuka baada ya TPLB kutangaza kuwa mchezo huo utapangiwa tarehe nyingine haraka iwezekenavyo.
Hii hapa taarifa ya Machi 8 2025

Taarifa rasmi imeeleza namna hii: “Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Ligi Kuu Tanzania, (TPLB) katika kikao chake cha Machi 8 2025 ilipitia shauri la Klabu ya Simba kuzuiliwa kuingia kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC, (Yanga na Simba ) uliopangwa kufanyika kwenye uwanja huo kuanzia saa 1:15 usiku.
“Katika shauri hilo, Klabu ya Simba iliiandikia barua Bodi ya Ligi kueleza kuhusu tukio tajawa hapo juu huku pia ikieleza nia yao ya kutoshiriki mchezo huo kwa sababu imezuiliwa kutumia haki yao ya kikanuni kama ilivyoainishwa kwenye kanuni ya 17:45 ya ligi kuhusu Taratibu za mchezo.
“Baada ya kupokea barua hiyo, Bodi ya Ligi iliwaagiza maofisa wake wa mchezo, (ambao walishuhudia tukio hilo) kutuma taarifa za tukio haraka ili hatua zinazostahili kuchukuliwa ikiwemo kuitishwa kwa kikao cha dharula cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi.
“Baada ya kupitia taarifa mbalimbali zikiwemo za maofisa wa mchezo na vyanzo vingine, kamati ilibaini kuwa Klabu ya Simba wakati ikielekea kutumia haki yake iliyoainishwa kwenye kanuni 17:45 ya Ligi Kuu haikuwasiliana na ofisa yeyote wa mchezo, timu mwenyeji wala mamlaka ya uwanja kuhusu nia yao ya kufanya mazoezi katika uwanja huo ili maandalizi ya kikanuni yafanyike.
“Katika taarifa hizo, kamati ilibaini pia kuwa walinzi ambao baadhi walifahamika kwa sura kuwa ni wa Klabu ya Yanga walishiriki tukio la kuzuia basi la Simba kuingia uwanjani kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:47 ya ligi kuhusu taratibu za mchezo.
“Kwa sababu bodi ilipokea taarifa ya ofisa usalama wa mchezo ambayo imeanisha matukio kadhaa yaliyoambatana na tukio hilo la Klabu ya Simba kushindwa kufanya mazoezi na kwamba baadhi ya matukio yanahitaji uchunguzi ambao hauwezi kukamilika kwa wakati. Bodi ya Ligi Kupitia Kamati yake ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeamua kuahirisha mchezo tajwa hapo juu kwa mujibu wa kanuni ya 34:1, (1.3) ya Ligi Kuu kuhusu kuahirisha mchezo ili kutoa nafasi yakupata taarifa zaidi zitakazosaidia kufanya maamuzi ya haki.
“Bodi itatoa taarifa kamili kuhusiana na tukio hilo na kutangazatarehe ya mchezo huo mapema iwezekanavyo.”
Ratiba mpya hii hapa
Ni Juni 15 2025 mchezo huo unatarajiwa kuchezwa licha ya Yanga SC kueleza kuwa maamuzi yao yapo palepale hawatajihusisha na mchezo huo.
Msimamo wa Yanga SC
Taarifa ya Yanga SC iliyotolewa Mei 5 2025 ilieleza namna hii:-“Uongozi wa Yanga unapenda kuutarifu umma kuwa umepokea majibu kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo, (CAS) kuhusu kesi namba CAS 2025/A/11298.
“CAS imeilekeza Yanga SC kurudi kwanza kwenye Kamati za ndani za soka ili kushughulikia kesi hiyo kabla ya kurudi kwao kwa ajili yah atua za rufaa.

“Lakini kutokana na uonevu, uvunjwajwi mkubwa wa kanuni na upendeleo wa dhahiri kwa baadhi ya timu unaoendelea kufanywa na mamlaka za soka Tanzania, uongozi wa Yanga hauna imani na hauko tayari kupeleka shauri hilo kwenye mamlaka ambazo zinatenda dhuluma.
“Aidha uongozi wa Yanga unapenda kuujulisha Umma kuwa msimamo wa klabu ya Yanga upo palepale kuwa hautashiriki mchezo namba 184 wa ligi msimu wa 2024/25 uko palepale kuwa hawatashiriki kwenye mchezo huo kwa namna yoyote ile.
“Wanayanga wote watakuwa tayari kuipambania haki yao kivyovyote vile ili kukomesha dhuluma na uvunjwaji mkubwa mkubwa unaoendelea kufanywa na mamlaka za soka kwa maslahi mapana ya maendeleo la soka.”
Taarifa ya TPLB
Taarifa ambayo ilitolewa na TPLB Mei Mosi 2025 mapema baada ya CAS kutoa majibu kuhusu kesi hiyo ilikuwa namna hii:- “Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo , (CAS) imetupa rufani ya klabu ya Yanga yenye kumbukumbu namba CAS 2025/A/11298 ambayo klabu hiyo ilifungua dhidi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, (TFF) kuhusiana na mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC , (Young Africans SC vs Simba SC).
“Walalamikiwa wengine katika shauri hilo ambapo pamoja na mengine, klabu ya Yanga iliomba mechi tajwa hapo juu isipangiwe tarehe mpaka litakapotolewa uamuzi ni Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, (TPLB) na klabu ya Simba SC.
“Kutokana na uamuzi huo wa CAS, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara inaendelea na maandalizi yake ya kuhitimisha msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2024/25 na kufanya maboresho ya ratiba ya ligi (ikiwemo mchezo namba 184- Young Africans vs Simba SC) kisha kutangaza ratiba mpya mapema iwezekanavyo.”

