Mzize ClementMzize Clement

MPANGO kazi wa kusaka pointi sita kwa wababe wawili, Tabora United na Yanga umegota mwisho ndani ya dakika 180, wakitoshana nguvu katika msako wa pointi sita msimu wa 2024/25 kwa kila timu kuvuna tatutatu ugenini. Kwenye mchezo wa mzunguko wa pili, Yanga walilipa kisasi kwa kuvuna pointi tatu kwa kuwa mzunguko wa kwanza walipoteza.

Chikola
Chikola nyota aliyefanya kazi kubwa kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza mbele ya Yanga, Uwanja wa Azam Complex kwa kumtungua Diarra. Source: Tabora United.

Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Novemba 7 2024 ubao ulisoma Yanga 1-3 Tabora United ambao waliandika rekodi yakuwa timu iliyopata ushindi mkubwa mbele ya Yanga kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza.

Mchezo wa Aprili 2 2025, ubao wa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ulisoma Tabora United 0-3 Yanga na bao la ufunguzi kwa Yanga likifungwa na beki Israel Mwenda dakika ya 20 kwa pigo la faulo akiwa nje ya 18 akitumia mguu wa kulia.

Clement Mzize na Dube
Clement Mzize na Dube washambuliaji wenye mabao 11 ndani ya kikosi cha Yanga msimu wa 2024/25. Source: Yanga.

Clement Mzize alifunga bao la pili dakika ya 57 likiwa ni bao lake la 11 ndani ya ligi na Prince Dube alifunga bao la tatu kwenye mchezo huo naye akifikisha mabao 11 kwenye ligi akiwa ametoa jumla ya pasi 7 msimu wa 2024/25.

POINTI 61 KIBINDONI

Yanga inafikisha jumla ya pointi 61 kwenye ligi na safu ya ushambuliaji imefunga mabao 61 kibindoni ikiwa ni timu inayoongoza kwa kufunga mabao mengi msimu wa 2024/25. Washambuliaji wawili wamefunga mabao 11 ambao ni Mzize na Dube.

Miloud Hamdi
Miloud Hamdi mchora ramani ndani ya kikosi cha Yanga kwenye mechi za ushindani 2024/25. Source: Yanga.

Ikumbukwe kwamba kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza Mzize alianzia benchi na alipoingia alifunga bao moja hivyo kwenye mabao 11 aliyonayo, mawili kawatungua Tabora United.

HIKI HAPA KIKOSI CHA YANGA KILICHOANZA

Kikosi cha Yanga inayodhaminiwa na SportPesa kilichoanza kilikuwa namna:-Djigui Diarra, Israel Mwenda, Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Prince Dube, Pacome na Clement Mzize.

Wachezaji wa akiba ni Aweso ambaye ni kipa, Nickson Kibabage, Bakari Nondo, Kibwana Shomari, Dennis Nkane, Sure Boy, Farid Mussa na Ikanga Lombo Jonathan.

MCHEZAJI BORA MTAMBO WA MABAO

Pacome Zouzoua kiungo mshambuliaji wa Yanga ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora mbele ya Tabora United ni mtambo wa mabao kwa kuwa alihusika kwenye mabao mawili kati ya matatu yaliyofungwa ndani ya dakika 90.

Pacome alitoa pasi kwa Mzize dakika ya 56 kwa mguu wa kulia akiwa nje ya 18 ikaleta bao la pili baada ya shambulizi la kushtukiza na alitoa pasi ya pili kwa Dube dakika ya 67 akiwa nje ya 18 kwa mguu wake wa kulia.

Pacome KMC
Pacome kiungo mshambuliaji wa Yanga ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora mchezo dhidi ya Tabora United. Source: Yanga.

Pacome anafikisha jumla ya pasi 8 za mabao ndani ya ligi akiwa ni namba mbili kwa mastaa wenye pasi nyingi huku kinara akiwa ni Feisal Salum wa Azam FC mwenye pasi 12 kibindoni akiwa katupia mabao manne.

Pacome katupia mabao 7 hivyo kahusika kwenye jumla ya mabao 15 yaliyofungwa na timu hiyo inayodhaminiwa na SportPesa wakiwa ni mabingwa watetezi.

JKT TANZANIA V DODOMA

Aprili 3 2025 kutakuwa na msako wa pointi tatu kwa wababe wawili ndani ya uwanja ikiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara ambayo ni namba nne kwa ubora Afrika.

JKT Tanzania iliyo nafasi ya 6 kwenye msimamo baada ya mechi 23 huku safu ya ushambuliaji ikiwa imetupia mabao 18 na ukuta kuruhusu mabao 17 na pointi zao kibindoni 30 itawakaribisha Dodoma Jiji, Uwanja wa Isahmuhyo, Dar saa 10:00 jioni.

Dodoma Jiji kwenye msimamo nafasi ya 8 pointi 27 baada ya mechi 23, safu ya ushambuliaji imetupia mabao 22 na ukuta umeruhusu jumla ya mabao 33 kufungwa ndani ya uwanja.

Ken Gold iliyo nafasi ya 16 na pointi 16 baada ya mechi 23 itawakaribisha matajiri wa Dar Azam FC, Uwanja wa Sokoine, Mbeya saa 10:00 jioni.

Fei Toto
Fei Toto kiungo mshambuliaji wa Azam FC ambaye ni namba moja kwa wakali wa pasi za mwisho akiwa nazo 12. Source: Azam FC.

Kagera Sugar iliyo nafasi ya 14 na pointi 19 itamenyana na Coastal Union iliyo nafasi ya 10 na pointi 25 itakuwa ni Uwanja wa Kaitaba, Kagera inatarajiwa kuchezwa saa 1:00 jioni.

SIMBA KUWAKABILI MASHUJAA

Fadlu Davids (-)
Fadlu Davids, Kocha Mkuu wa Simba iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi msimu wa 2024/25. Source: Simba.

Kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids ndani ya Aprili hawatakuwa na mchezo wa ligi kete yao itakuwa dhidi ya Mashujaa hii inatarajiwa kuchezwa Mei 2 2025, Uwanja wa KMC Complex, Dar.

Share this: