Kapombe na MutaleKapombe na Mutale

KITAUMANA Uwanja wa KMC Complex kwa wababe wawili kusaka pointi tatu muhimu ndani ya dakika 90 kwenye mchezo wa ligi itakuwa ni Simba dhidi ya Dodoma Jiji mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani kwa pande zote mbili Machi 14 2025, saa 10:00 jioni.

Fadlu Davids
Fadlu Davids, Kocha Mkuu wa Simba iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya mechi 21. Source: Simba.

Chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids Simba ilikomba pointi tatu ugenini kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza hivyo kisasi kinatarajiwa kuwa kwa upande wa Dodoma Jiji huku rekodi zikipambaniwa kulindwa kwa wababe kutoka Kariakoo, Simba.

Simba kwenye msimamo ni nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 21 ikiwa imekusanya jumla ya pointi 54 katika mechi hizo ni ushindi kwenye mechi 17, ilitoshana nguvu katika mechi tatu ilipoteza mchezo mmoja ilikuwa dhidi ya Yanga inayodhaminiwa na SportPesa.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Yanga, baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 0-1 Yanga bao la Kelvin Kijili ambaye alijifunga dakika ya 88 kwenye harakati za kuokoa hatari.

Ateba na Mutale
Leonel Ateba akiwa na wachezaji wenzake wa Simba wakishangilia moja ya bao kwenye mechi ya ushindani. Source: Simba.

Safu ya ushambuliaji ya Simba inayoongozwa na Leonel Ateba ambaye amecheza mechi 16 akikomba dakika 1,156 akitupia mabao 8 na pasi tatu za mabao na Steven Mukwala ambaye kacheza mechi 19 akikomba dakika 666 na kutupia mabao 8 na pasi mbili za mabao imetupia jumla ya mabao 46.

Kinara wa utupiaji ndani ya kikosi cha Simba ni Jean Ahoua ambaye katupia mabao 10 kibindoni akiwa amecheza jumla ya mechi 20 akikomba dakika 1,460 ni pasi sita za mabao katoa kiungo huyu akiwa kahusika kwenye mabao 16 kati ya 46 yaliyofungwa na Simba.

Kwenye upande wa ukuta ni mabao 8 timu hiyo imeruhusu ikiwa ni timu namba moja katika ligi kufungwa mabao machache kwenye msimamo ni pointi zao 54 zipo kibindoni.

Mchezo wao uliopita Simba ilikuwa ugenini Machi Mosi dhidi ya Coastal Union baada ya dakika 90 ubao ulisoma Coastal Union 0-3 Simba, mabao yote yakifungwa na Steven Mukwala ambaye ni nyota wa kwanza ndani ya kikosi cha Simba kufunga hat trick msimu wa 2024/25.

HAWA KUKOSEKANA

Che Malone
Che Malone beki wa kati wa Simba ambaye alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Azam FC. Source: Simba.

Huenda beki wa Simba, Che Malone ambaye ni kiongozi kwenye safu ya ulinzi atakosekana kwenye mchezo wa leo kwa kuwa alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Azam FC ambao ulikuwa ni Mzizima Dabi.

Mbali na Che Malone kipa namba moja, Mousa Camara huenda akakosekana kwenye mchezo ujao kwa kuwa naye alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Azam FC.

KIPORO KITALIKA?

Machi 7 mchezo wao uliopita ilikuwa wa ligi baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ulisoma Dodoma Jiji 0-0 Coastal Union wakigawana pointi mojamoja

Mchezo huu ni kiporo ambao uliahirishwa baada ya Februari 10 2025 Dodoma Jiji kupata ajali wakiwa njiani kuja Dar kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo dhidi ya Simba. Hivyo swali kubwa ndani ya dakika 90 ni kujua kwamba kiporo kitalika ama kitachacha kwa wababe hawa?

Ikumbukwe kwamba Dodoma Jiji ilitoka kucheza mchezo wa ligi dhidi ya Namungo ilikuwa ni Februari 9 2025 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Majaliwa ulisoma Namungo 2-2 Dodoma Jiji na kip awa Dodoma Jiji, Ngeleka Katembua alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo.

HAWA HAPA DODOMA JIJI KWENYE REKODI

Kwenye msimamo wa ligi, Dodoma Jiji ipo nafasi ya 8 baada ya kucheza mechi 22 ilipata ushindi kwenye mechi 7 ilipata sare kwenye mechi 6 na mechi 9 ilipoteza kibindoni imekusanya jumla ya pointi 27.

Paul Peter
Paul Peter nyota wa Dodoma Jiji ambaye alifunga moja ya bao kwenye mchezo dhidi ya Namungo,Uwanja wa Majaliwa. Source: Dodoma Jiji.

Safu ya ushambuliaji ya Dodoma Jiji ni mabao 22 imetupia na ukuta umeruhusu kutunguliwa jumla ya mabao 27. Katika mabao hayo 27 bao moja walifungwa na Simba kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Kwenye mchezo wa Septemba 29 2024 baada ya dakika 90 ubao ulisoma Dodoma Jiji 0-1 Simba, bao la ushindi likifungwa na Jean Ahoua kwa mkwaju wa penati iliyosababishwa na Mohamed Hussen ilidumu mpaka mwisho wa mchezo huo.

Rekodi zinaonyesha kuwa Dodoma Jiji haijawahi pata Bahati ya kukomba pointi tatu mbele ya Simba kwenye mechi za ushindani ndani ya ligi zaidi iligotea kufunga bao moja katika mechi 9 zilizopita na safu ya ushambuliaji ya Simba ikifunga jumla ya mabao 19.

Share this: