FADLU Davids, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa walikuwa tayari kwa mchezo wa Kariakoo Dabi hivyo kuahirishwa kwake kuliwapa kazi nyingine kufanya maandalizi kuwakabili TMA Stars ndani ya dakika 90 kwenye mchezo wa CRDB Federation Cup.
Ikumbukwe kwamba Machi 8 2025 ilitarajiwa Kariakoo Dabi kati ya Yanga inayodhaminiwa na SportPesa dhidi ya Simba kuchezwa mchezo huo uliahirishwa na taarifa ilielezwa namna hii:-

Taarifa rasmi imeeleza namna hii: “Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Ligi Kuu Tanzania, (TPLB) katika kikao chake cha Machi 8 2025 ilipitia shauri la Klabu ya Simba kuzuiliwa kuingia kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC, (Yanga na Simba ) uliopangwa kufanyika kwenye uwanja huo kuanzia saa 1:15 usiku.
“Katika shauri hilo, Klabu ya Simba iliiandikia barua Bodi ya Ligi kueleza kuhusu tukio tajawa hapo juu huku pia ikieleza nia yao ya kutoshiriki mchezo huo kwa sababu imezuiliwa kutumia haki yao ya kikanuni kama ilivyoainishwa kwenye kanuni ya 17:45 ya ligi kuhusu Taratibu za mchezo.
“Baada ya kupokea barua hiyo, Bodi ya Ligi iliwaagiza maofisa wake wa mchezo, (ambao walishuhudia tukio hilo) kutuma taarifa za tukio haraka ili hatua zinazostahili kuchukuliwa ikiwemo kuitishwa kwa kikao cha dharula cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi.
“Baada ya kupitia taarifa mbalimbali zikiwemo za maofisa wa mchezo na vyanzo vingine, kamati ilibaini kuwa Klabu ya Simba wakati ikielekea kutumia haki yake iliyoainishwa kwenye kanuni 17:45 ya Ligi Kuu haikuwasiliana na ofisa yeyote wa mchezo, timu mwenyeji wala mamlaka ya uwanja kuhusu nia yao ya kufanya mazoezi katika uwanja huo ili maandalizi ya kikanuni yafanyike.
“Katika taarifa hizo, kamati ilibaini pia kuwa walinzi ambao baadhi walifahamika kwa sura kuwa ni wa Klabu ya Yanga walishiriki tukio la kuzuia basi la Simba kuingia uwanjani kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:47 ya ligi kuhusu taratibu za mchezo.
“Kwa sababu bodi ilipokea taarifa ya ofisa usalama wa mchezo ambayo imeanisha matukio kadhaa yaliyoambatana na tukio hilo la Klabu ya Simba kushindwa kufanya mazoezi na kwamba baadhi ya matukio yanahitaji uchunguzi ambao hauwezi kukamilika kwa wakati , Bodi ya Ligi Kupitia Kamati yake ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeamua kuahirisha mchezo tajwa hapo juu kwa mujibu wa kanuni ya 34:1, (1.3) ya Ligi Kuu kuhusu kuahirisha mchezo ili kutoa nafasi yakupata taarifa zaidi zitakazosaidia kufanya maamuzi ya haki.
“Bodi itatoa taarifa kamili kuhusiana na tukio hilo na kutangazatarehe ya mchezo huo mapema iwezekanavyo.”

USHINDI WA SIMBA DHIDI YA TMA STARS
Katika mchezo wa hatua ya 32 bora, baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa KMC ulisoma Simba 3-0 TMA Stars huku mabao yakifungwa na Valentin Nouma dakika ya 15 kwa pigo la faulo iliyosababishwa na Awesu Awesu.
Bao la pili dakika ya 19 alijifunga Sixtus Sabilo kwenye harakati za kuokoa na bao la tatu alifunga Leonel Ateba dakika ya 75 kwa Krosi ya Kelvin Kijili. Katika mchezo huo Ateba alikomba dakika 90 na kiungo mshambuliaji Joshua Mutale ambaye alianza kikosi cha kwanza.
Fadlu amesema: “Ulikuwa ni mchezo mgumu hasa ukizingatia kwamba timu ambayo tumekutana nayo haipo kwenye ligi na tulitoka kufanya maandalizi ya Kariakoo Dabi ambayo haikuchezwa hivyo tulikuwa na kazi yakufanya kuwarejesha wachezaji kwenye hali ya kawaida na kupata matokeo.”
UWANJA WA MKAPA WAFUNGIWA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika, (CAF) limeufungia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa muda kutokana na eneo la kuchezea kuendelea kupungua ubora wake.

CAF imeelekeza eneo hilo liboreshwe haraka kufikia viwango vinavyotakiwa ili kuepeuka uwanja huo kufungiwa kwa muda mrefu.
Mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho CAF kati ya Simba v Al Masry imepangiwa kuchezwa uwanja huo Aprili 9 2025 ili kuondoa usumbufu Shirikisho la Mpira Tanzania, (TFF) limetakiwa kutuma jina la uwanja mbadala utakaotumiwa na Simba Machi 14 2025.
Taarifa hiyo imetolewa na TFF, Machi 12 2025 ambapo Simba ni wawakilishi wa Tanzania kwenye mechi za kimataifa wanautumia Uwanja wa Mkapa katika mechi za nyumbani.

