Clatous ChamaChama Jr

KIKOSI cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi hakina jambo dogo kwenye suala la kucheka na nyavu wakiwa ni namba moja kwenye eneo hili kwa kukusanya mabao mengi zaidi msimu wa 2024/25.

Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ni mechi 22 za ligi dakika 1,980 ilishuka uwanjani safu ya ushambuliaji ya Yanga ni namba moja ikiwa na jumla ya mabao 58 ina wastani wakufunga bao moja kila baada ya dakika 34.

Hamdi Yanga
Miloud Hamdi, Kocha Mkuu wa Yanga ambao ni vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2024/25. Source: Yanga.

Timu hiyo ilianza kwa mwendo wa kusuasua mzunguko wa kwanza ambapo mchezo wake wa kwanza ikiwa ugenini Agosti 29 2024 dhidi ya Kagera Sugar baada ya dakika 90 ubao ulisoma Kagera Sugar 0-2 Yanga na mchezo wa pili ilikuwa Ken Gold 0-1 Yanga.

Ndani ya dakika 180 safu ya ushambuliaji ya Yanga ilitupia mabao matatu huku ukuta ukiwa haujaruhusu bao ndani ya mechi hizo za ugenini na bao la ushindi kwenye mchezo dhidi ya Ken Gold, Uwanja wa Sokoine, Mbeya lilifungwa na Ibrahim Bacca ambaye ni beki namba moja kwa kutupia mabao mengi ambayo ni manne.


DUBE NA REKODI YAKE BONGO

Prince Dube huyu ni nyota wa kwanza kufunga hat trick ilikuwa ni Desemba 19 2024, Uwanja wa KMC, Complex baada ya dakika 90 ubao ukasoma Yanga 3-2 Mashujaa. Kwenye mchezo huu alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo.

Dubeee
Prince Dube mshambuliaji wa Yanga akiwa na mabao 10 ndani ya ligi msimu wa 2024/25. Source: Yanga.

 Clement Mzize ni mzawa namba moja mwenye mabao mengi ndani ya ligi namba nne kwa ubora Afrika akiwa katupia mabao 10 sawa na Dube, muuaji anayetabasamu ambaye ana tuzo ya mchezaji bora ndani ya ligi kwa Februari.

MTUPIAJI WA KWANZA YANGA

Maxi Nzengeli huyu ni nyota wa kwanza kufunga ndani ya kikosi cha Yanga msimu wa 2024/25 ilikuwa dhidi ya Kagera Sugar, kibindoni ana mabao matano na katoa pasi 7 za mabao.

Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 58 baada ya mechi 22 safu yao ya ushambuliaji ni namba moja kwa kufunga mabao mengi ambayo ni 58. Timu namba mbili ni Simba ambayo safu yao ya ushambuliaji imetupia mabao 52 baada ya mechi 22.

VITA YAO NA MNYAMA

Kwenye vita ya kuwania ubingwa ndani ya ligi kuu bara inayodhaminiwa na NBC ngoma bado ni mbichi kwa kila timu kupambania pointi tatu ndani ya dakika 90 huku Simba ikipigwa bao mazima na Yanga kwenye eneo la kucheka na nyavu.

Bacca na Ateba
Leonel Ateba mshambuliaji wa Simba akiwa kwenye vita ya kuwania mpira na Bacca wa Yanga katika moja ya Kariakoo Dabi. Source: Yanga.

Kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi ni namba moja kwenye timu zenye mabao mengi ambayo ni 58 baada ya mechi 22 ambazo ni dakika 1,980 ikiwa na wastani wakufunga bao moja kila baada ya dakika 34.

Wakati Yanga ikiwa ni namba moja imewapiga bao watani zao wa jadi Simba kwenye eneo hilo kwa kuwaacha kwa tofauti ya mabao sita kwa kuwa safu ya ushambuliaji ya Simba imetupia jumla ya mabao 52. Simba ni eneo la kufungwa mabao machache ikiwa imefungwa mabao 8 na Yanga imefungwa mabao 9.

Kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids kimetupia mabao 52 baada ya kucheza mechi 22 ambazo ni dakika 1,980 msimu wa 2024/25 kikiwa na wastani wakutupia bao moja kila baada ya dakika 38.

Simba kwa msimu wa 2024/25 imekuwa na wastani wakufunga bao kwenye kila mchezo ambapo katika mechi 22 ambazo ilicheza ni mchezo mmoja pekee ilikwama kufunga ilikuwa dhidi ya Yanga.

Katika mchezo huo wa mzunguko wa kwanza wa Kariakoo Dabi baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 0-1 Yanga, bao la Kelvin Kijili ambaye alijifunga kwenye harakati za kuokoa hatari ndani ya uwanja.

Ahoua Namungo
Ahoua kiungo mshambuliaji wa Simba ambaye ni kinara wa utupiaji mabao kwenye ligi ya Bongo akiwa katupia mabao 12. Source: Simba.

Mchezo ambao Simba ilikusanya mabao mengi ilikuwa dhidi ya Dodoma Jiji ambao ulichezwa Uwanja wa KMC Complex kwenye mchezo huu baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 6-0 Dodoma Jiji huku Kibu Dennis akifungua akaunti ya mabao baada ya kupitisha wiki 70 bila kufunga ndani ya ligi.

Jean Ahoua kwenye mchezo huo uliochezwa Machi 14 2024 alitupia mabao mawili akifikisha mabao 12 na pasi zake ni sita akiwa ni namba moja kwa wakali wenye mabao mengi ndani ya ligi.

Share this: