STORI kubwa kwa sasa katika vijiwe vya soka na majukwaa mbalimbali ya uhabarishaji wa habari ni kuhusu kuahirishwa kwa mchezo mkubwa wa Dabi ya Kariakoo kati ya Yanga ambao wanadhaminiwa na Kampuni bora ya michezo ya kubashiri ya SportPesa dhidi ya Simba.
Mchezo huo ambao ulipaswa kupigwa siku ya Jumamosi Machi 8, mwaka huu uliahirishwa na bodi ya Ligi Kuu Bara, uamuzi ambao ulitangazwa majira ya mchana siku ya mchezo yaani Jumamosi kufuatia kikao cha dharura kilichofanyika asubuhi ya siku hiyo.

Chanzo kikubwa cha kuahirishwa mchezo huo ni timu ya Simba ambayo kupitia uongozi wao walitoa taarifa ya kususia mchezo huo, mara baada ya kile walichokiita uvunjifu wa kanuni wa kufanyiwa vurugu na kunyiwa haki yao ya kufanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa mchezo yaani Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Msimamo wa Yanga kupitia Kamati Tendaji ya timu hiyo mara baada ya matukio hayo yote ni kuwa;
1: Klabu ya YANGA kupewa haki yake ya ushindi kama inavyoelezwa kwenye kanuni, pindi timu moja inapogomea mechi.
2: Kamati ya Utendaji ya YANGA imekubaliana kutoshiriki mchezo namba 184 kwa tarehe yoyote itakayopangwa.
3. Kutokana na mfululizo wa uvunjifu na kushindwa kusimamia kanuni za Ligi Kuu, Klabu ya YANGA imekosa imani na Kamati ya Uendeshaji ya Ligi Kuu, chini ya Mwenyekiti wake Steven Mnguto na Katibu wa Kamati hiyo Almas Kasongo, hivyo tunaliomba Shirikisho la Mpira wa miguu – TFF kuivunja kamati hiyo na kuteua viongozi wengine waadilifu na wenye nia njema kwa maslahi mapana ya mpira wetu.

Kama sehemu ya wadau muhimu wa soka, wachambuzi mbalimbali wametoa maoni yao kuhusu sakata hilo kama ifuatavyo;
Hans Raphael
“Ukisoma vizuri kanuni za ligi zinasema kosa la kikanuni litaadhibiwa kikanuni, ila kwenye Simba na Yanga kanuni huwa zinakufa kwa Muda. Kwa kifupi Simba na Yanga ni wakubwa kuliko kanuni, wanafanya wajisikiacho, wakitaka kugoma wanagoma, wakitaka muda wa mechi ubadilishwe unabadilishwa yani Tanzania ya kwetu kivyetu
Farhan Kihamu
“Kumbe sasa naanza kupata picha kamili ya sakata hili, nakumbushwa kuwa kwenye historia ya Derby ya Kariakoo, huwa wote wawili hawafanyi mazoezi pale uwanjani siku moja kabla ya mchezo, uwe Mgeni au uwe Mwenyeji huruhusiwi kuugusa uwanja, imekuwa hivyo kwenye historia ya mechi zao na uwanja unalindwa, kila mmoja anapaswa kufanya mazoezi anapofanyiaga, japo hii haipo kikanuni hii kitu ndio nimejua leo, imenishangaza sana.
“Maswali yanakuja, kama mchakato huu haupo Kikanuni na walikuwa wanafuata wote wawili, je walikuwa wanasimamiwa na nani wote wawili kutekeleza kanuni hii mficho? Maana hata mechi ya raundi ya kwanza Mgeni Yanga hakusogea kabisa kwa Mkapa, nimetumiwa picha kuwa walifanya mazoezi Kigamboni, hili sakata.
“Ligi ina kanuni, utaratibu au makubaliano ambayo hatuyajui ama? Rasmi nimefunga mikono yangu, siandiki tena hii kitu kumbe ina mambo mengi sana, tunaweza kukomaa na Kanuni kumbe wala watu hawapo huko kwenye karatasi zetu.”
Jemedari Said

“Nimefuatilia maoni ya watu wengi wenye ushawishi, nguvu, busara na maarifa juu ya kughairishwa kwa mechi ya “DABI YA KARIAKOO”. Wengi wamejaribu kuwalaumu Bodi ya Ligi “KWA KUGHAIRISHA MECHI” bila kujali mazingira yaliyopelekea mechi kughairishwa.
“Ukisikia taarifa za watu waliozuia Simba SC kufanya mazoezi kwamba walikusanywa kutoka maeneo ya karibu na uwanja wa Taifa kuja kufanya jambo hilo, unajiuliza kwa manufaa ya nani na kwajili gani? Ukiona na kusikia namna Simba SC walivyoghasiwa na kuzuiwa isivyohalali kufanya mazoezi tena na watu wa timu mwenyeji wa mchezo, inakupa picha ya hisia za kuonewa ambazo wachezaji, viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba walikuwa nazo wakati na baada ya pale.
“Kama viongozi wa Simba wangekosa busara wakaamua na wenyewe kusomba wahuni wa klabu yao kutoka maeneo ya karibu ya uwanja wa Taifa kuja kushinikiza wafanye mazoezi, hali ingekuaje. Lakini Simba SC wenye hisia kali za kuonewa jana, wangekuwa Taifa muda wanacheza mechi na watesi wao kwa mfano, halafu itokee bahati mbaya kuwe na kosa la kibinadamu kama ilivyokuwa kwa DABI iliyotangulia ya Kayoko, unadhani hali ingekuwaje?
“Mpirani usalama wa wachezaji na mashabiki ndiyo kilakitu, tayari kulikuwa na mazingira ya usalama mdogo/kutokuwa na usalama wa kutosha (insecurity), kughairisha mechi ni busara na akili kubwa sana na sio vinginevyo.”
“Kuwalazimisha Simba SC walioonewa baada ya Bodi kuthibitisha haki yao ya kikanuni kuzuiliwa na wapinzani wao, isingekuwa jambo la busara hasa baada ya kuwasilisha malalamiko yao na kuonyesha nia ya kutocheza. Kama wasingefika kwenye mechi ingebidi wapokwe alama 15 ambazo zingezua mzozo mkubwa zaidi, kughairisha mechi kwa mazingira haya ilikuwa ndiyo jambo pekee la busara za kiuongozi.
“Sisi wenyewe watanzania tumezifanya Simba na Yanga kuwa miungu watu na MPIRA wetu unazidi kuharibika kutokana na usimba na uyanga ndiomaana napinga wale wote wanaoisema bodi kwasababu haya yanayoendelea sasa hayajaanza leo. Watu wanapaswa kufuata kanuni na sheria za ligi kuu ndio maana timu zote za ligi kuu zimepewa hizo kanuni ili wazisome kwamba kila timu inaruhusiwa kufanya mazoezi siku moja kabla ya mchezo”
Shaffih Dauda
“Tanzania ina bahati ya kuwa na Ligi yenye ushindani na yenye mvuto wa kibiashara, kama hakuna mtu wa kusafisha hali ya sasa, mediocrity itaendelea kutawala. Suluhisho linapaswa kuwa;
• FIFA ichukue hatua kali kwa TPLB na mamlaka za soka nchini ( Wote wanaosimamia mpira)
• Yafanyike Mageuzi ya utawala wa soka na kuhakikisha viongozi wanakuwa na sifa rasmi za kiutawala hasa wa mpira ( Mpira uongozwe na watu wa mpira) Hii ni kuanzia Ngazi za Juu , Vilabu hadi chini kabisa.
• Vyombo vya habari virudi kwenye msingi wa kuhabarisha , kuelimisha , kukosoa, kuburudisha inapobidi na uchambuzi wa kweli badala ya ushabiki
• Mashabiki waache ushabiki wa kipofu na waweke shinikizo kwa mamlaka za soka kuboresha hali ya ligi
“Kwa sasa, Tanzania imefika mahali ambapo mediocrity imehalalishwa—mashabiki, viongozi, vyombo vya habari, na hata baadhi ya wachezaji wanaishi ndani ya mfumo uliooza, lakini hakuna anayepiga kelele kwa nguvu ya kutosha.”

