Kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tabora United ambao unatarajiwa kupigwa siku ya Jumapili mkoani Tabora, kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka rasmi kesho Jumamosi kuwafuata wapinzani wao.
Uongozi wa Simba haujauchukulia poa mchezo huo kwani maandalizi kabambe yameendelea kufanyika huku uongozi ukitenga siku 5 kumaliza kazi.
Iko hivi, kikosi cha Simba kilirejea kambini rasmi siku ya Januari 28, mwaka huu kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo huo ambau unatarajiwa kupigwa katika Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi.
Unaweza kubashiri mchezo huu na kushinda mamilioni kwa kuweka mkeka wako kupitia Kampuni bora ya kubashiri ya SportPesa kwa kubonyeza link hii www.sportpesa.co.tz
TAMKO LA SEMAJI AHMED

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema wachezaji wote waliokuwa wamepewa mapumziko tayari walikwisharejea na kikosi kameendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo huo.
Ahmed pia amekiri kuwa wanautarajia mchezo mgumu hasa kutokana na ubora wa Tabora United msimu huu, lakini ametamba kuwa wamejipanga kuendeleza moto wa kukusanya pointi tatu muhimu.
Katika hatua nyingine Ahmed ameweka wazi kuwa kikosi chao kinatarajia kuanza rasmi safari ya kuwafuata Tabora kesho Jumamosi.
“Wachezaji walipewa mapumziko ya siku chache baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 6-0 tuliopata dhidi ya Kilimanjaro Wonders wikiendi iliyopita kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB.
“Lkaini tayari kikosi kilikwisharejea mazoezini, ambapo hata wale ambao walipewa mapumziko marefu kidogo hasa wa kikosi cha kwanza nao wamerejea na wanaendelea na mazoezi. Tunafahamu itakuwa mechi ngumu lakini tunaendelea na maandalizi lengo ni kuchukua alama zote tatu.
“Tabora ni timu ngumu na kila mmoja ameshuhudia jinsi gani wamekuwa bora msimu huu na hii ni mara baada ya kufanikiwa kuzifunga timu zote za Dar es Salaam kasoro Simba pekee.” amesema Ahmed.
MZUNGUKO WA PILI UNAANZA RASMI

Mchezo dhidi ya Tabora United unatarajia kuthitisha kuanza rasmi kwa mzunguko wa pili wa ligi ambayo mpaka inasimama kupisha ratiba ya mashindano ya kimataifa Simba ndio wameendelea kuwa vinara na pointi zao 40 walizokusanya katika michezo 15.
KOCHA SIMBA ATOA SABABU ZA KUPANGUA KIKOSI

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids ametolea ufafanuzi mabadiliko aliyoyafanya kwenye kikosi chake hususani katika mchezo wa ushindi mnono wa mabao 6-0 walioupata dhidi ya Kilimanjaro Wonders katika mchezo wa hatua ya 64 ya CRDB Federation Cup na kukiri mchezo huo ulimpa changamoto kubwa uwanjani.
Fadlu amelipongeza benchi la ufundi la timu hiyo pamoja na wachezaji kwa kazi kubwa waliyofanya ingawa Simba iliwazidi hadhi pamoja na uzoefu wa mashindano.
Akizungumzia kuhusu mabadiliko makubwa kwenye kikosi katika mchezo wa leo, Fadlu amesema lengo ni kuhakikisha wachezaji wanapata nafasi kubwa ya kucheza kwakuwa wameingia mzunguko wa pili na mechi ni nyingi zilizo mbele yao.
“Ukimtoa Aishi Manula ambaye alikuwa anasumbuliwa na mafua wachezaji wengine wote walikuwa fiti, mabadiliko ya mchezo dhidi ya Kilimanjaro Wonders yalitokana na kutaka kuwapa nafasi wachezaji wengine kwakuwa tunafahamu ratiba itakuwa ngumu siku za usoni,” amesema Fadlu.
Aidha Fadlu amewasifia wachezaji kwa kuonyesha kiwango safi huku wengi wao wakiwa hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara.
SIMBA NDANI YA 32 BORA KOMBE LA SHIRIKISHO LA CRDB
Ushindi walioupata Simba dhidi ya Kilimanjaro Wonders umeifanya timu hiyo kufanikiwa kutinga hatua ya 32 bora ya CRDB Federation Cup kwa kishindo, hii ni baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa KMC Complex.
Katika mchezo huo straika kinda wa Simba, Valentino Mashaka aliwapatia bao la kwanza dakika ya kwanza akimalizia mpira wa krosi uliopigwa na Valentine Nouma. Ladaki Chasambi aliwapatia bao la pili dakika ya tatu baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na David Kameta ‘Duchu’.
Patrick Sebastian alijifunga dakika ya 10 na kufanya ubao ufikishe bao la tatu wakati akiwa katika jitihada za kuokoa shuti lililopigwa na Augustine Okajepha. Joshua Mutale aliipatia Simba bao la nne dakika ya 20 kufuatia mlinda mlango wa Kilimanjaro kukosea kutoa pasi iliyomkuta nyota huyo raia wa Zambia.
Steven Mukwala aliipatia Simba bao la tano dakika ya 48 kwa kichwa baada ya kumalizia vema mpira wa krosi uliopigwa na Duchu. Dakika ya 80 Edwin Balua aliipatia bao la sita kwa shuti la chini chini akiwa ndani ya 18 lililomshinda mlinda mlango wa Kilimanjaro.
Ikumbukwe katika mchezo huo kikosi cha Simba kilikuwa kama ifuatavyo: Ally, Duchu, Nouma, Chamou, Hamza (Kijili 82′), Okajepha (Balua 45′), Chasambi, Mzamiru (Fernandez 65′), Mashaka (Mukwala 45′), Awesu (Omary 30′), Mutale

