KOCHA Mkuu wa Simba Fadlu Davids amekuwa na zali la ushindi kutokana na mwendo anaokwenda nao katika kikosi hicho ambacho kinaongoza ligi namba nne kwa ubora Afrika na Januari 26 2025 alikuwa shuhuda dakika 90 zikikamilika kwa ushindi wa mabao 6-0 Kilimanjaro Wonders, mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC, Complex.

Ikumbukwe kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa, Januari 25 2025 ilipata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Copco mchezo wa CRDB Federation Cup, hivyo ndani ya dakika 180 ni mabao 11 yamefungwa Uwanja wa KMC na vigogo hao wawili Bongo.
Simba ndani ya msimu wa 2024/25 kwenye ligi baada ya kucheza mechi 15 imekusanya jumla ya pointi 40 ikiwa namba moja huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 31 ikiwa ni namba mbili kwa timu zenye mabao mengi.

Ukuta wa Simba inayoongozwa na Fadlu ni namba moja kwa timu ambazo zimefungwa mabao machache ambayo ni 5 yote hayo alitungulia Mousa Camara ambaye ni kipa namba moja wa Simba akiwa kinara kwa makipa wenye hati safi akiwa hajafungwa kwenye mechi 12.
Ndani ya dakika 1,350 ambazo ni mechi 15 Simba safu yake ya ushambuliaji imekuwa na wastani wa kuwa na hatari kila baada ya dakika 43 huku ikiruhusu kufungwa kila baada ya dakika 270.
Kwenye mechi 15 ambazo imecheza Simba ni mechi moja ilipoteza ilikuwa Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga ambapo baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa, Fadlu alishuhudia ukisoma Simba 0- Yanga kwa bao la kujifunga la Kelvin Kijili.
Ukiweka kando kupoteza mchezo mmoja, mchora ramani Fadlu ameshuhudia timu hiyo ikiambulia sare moja ilikuwa Uwanja wa KMC Complex baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 2-2 Coastal Union. Kwa upande wa ligi wakiwa ni namba moja pia mipango ya Fadlu kwenye anga la kimataifa katika mechi 6 za hatua ya makundi ilijibu kwa kugota nafasi ya kwanza wakiwa na pointi 13.

Katika mechi sita ambazo walicheza kila waliposhuka uwanjani wachezaji wa Simba walikuwa wakifunga iwe ugenini ama nyumbani jambo ambalo limeongeza hali ya kujiamini licha ya makosa ya safu ya ulinzi inayoongozwa na Che Malone kuruhusu mabao manne kufungwa.
Safu ya ushambuliaji ni mabao 8 ilifunga kwenye mechi sita na kinara wa utupiaji ni kiungo mshambuliaji Kibu Dennis ambaye katupia mabao matatu katika anga la kimataifa.
Fadlu ameweka wazi kuwa kikubwa ni ushirikiano na malengo ilikuwa ni kupata ushindi kwenye mechi ambazo walikuwa wanacheza jambo ambalo liliwezekana.
“Kila mchezo ambao tunacheza kwetu muhimu kupata ushindi na tumekuwa tukishirikiana kila mara kikubwa ni kuendelea kuwa kwenye mwendelezo mzuri tunaamini kwamba kazi bado ipo.”
Katika mechi 21 ikiwa ni 15 za ligi na 6 za hatua ya makundi, ushindi kwa Fadlu ni kwenye mechi 17, sare mbili na kupoteza mechi mbili.Kwenye ligi ushindi ni mechi 13, sare moja, kupoteza mchezo mmoja.
Katika anga la kimataifa hatua ya makundi ushindi ni mechi nne sare mchezo mmoja na kupoteza mchezo mmoja kibindoni pointi zao ni 13 wakiwa vinara kitaifa na kimataifa.
BEKI WAKE WA KAZI

Kwenye eneo la ulinzi ndani ya kikosi cha Simba kuna mtu wa kazi ngumu anayezidi kuimarika kila leo kutokana na kujituma kwake katika kutimiza majukumu licha ya makosa ambayo amekuwa akifanya kwenye baadhi ya mechi.
Ni Abdlazack Hamza, beki wa kazi ndani ya kikosi cha Simba ambaye amekuwa ni chaguo la kwanza katika kikosi cha Fadlu kwenye mechi za ushindani kitaifa na kimataifa akiwa anapewa majukumu yakufanya kwenye mechi hizo.
Kwenye mchezo dhidi ya Constantine ugenini nyota huyo alijifunga bao katika harakati za kuokoa na bao la pili ambalo Simba walifungwa ni Che Malone katika harakati za kuokoa mpira wake ukakutana na nyota wat imu pinzani ambaye alimtungua Moussa Camara, hivyo kuna umuhimu wa safu ya Simba kwenye ulinzi kuongeza umakini.
Rekodi zinaonyesha kuwa kwenye ligi Hamza ni mechi 10 amecheza kati ya 15 ambazo Simba imecheza akikosekana katika mechi tano pekee ndani ya uwanja. Katika mechi hizo 10 beki huyo mzawa ni dakika 800 kakomba akiwa hajafunga bao wala kutoa pasi ya bao na timu ya Simba ikiwa ni namba moja kwenye msimamo wa ligi na pointi zaoni 40.
Ukiweka kando Simba kuongoza ligi ni timu namba moja kufungwa mabao machache ndani ya msimu wa 2024/25 ambayo ni matano kwa mzunguko wa kwanza hivyo kuna kazi kubwa ya kufanywa ndani ya Simba kwenye mzunguko wa pili.

