KOCHA mkuu wa Simba Msauz, Fadlu Davis ni kama ameshtukia jambo kwenye ishu ya vita ya ubingwa msimu huu, hii ni mara baada ya kufanya maamuzi magumu ya kufuta mapumziko mara baada ya timu hiyo kutoka Mbeya na moja kwa moja kuamuru mastaa wote warudi kambini kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mchezo wao wa Ijumaa hii dhidi ya Namungo.
Simba ambao wamewahi kulamba udhamini wa SportPesa juzi Jumatano walirejea rasmi Dar es Salaam kutokea jijini Mbeya ambapo walikuwa na ratiba ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons uliopigwa siku ya Jumanne na kushuhudia wababe hao wakirejea tena kwenye njia ya ushindi baada ya kupita michezo miwili bila matokeo ya pointi tatu muhimu.
USHINDI BAADA YA DAKIKA 180

Simba juzi Jumanne walifanikiwa kurejea tena kwenye njia ya ushindi mara baada ya kupita michezo miwili sawa na dakika 180, hii ni baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya wenyeji wao Tanzania Prisons.
Mchezo huo ulipigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ambapo Simba waliingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu mbaya baada ya kuvuna pointi moja tu katika michezo miwili iliyopita wakiambulia sare ya mabao 2-2 na Coastal Union kabla ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga.
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 16, zinazowaweka katika nafasi ya tatu kwenye msimamo baada ya kucheza mechi saba.
Kikosi cha ushindi kilikuwa: Camara, Kapombe Zimbwe Jr (Balua 62′)Che Malone, Chamou, Ngoma, Kibu, Okajepha, Ateba (Mukwala 72′)*, Awesu (Mutale 62′), Chasambi (Mzamiru 84′)
KIKOSI CHATUA DAR, KOCHA AFUTA MAPUMZIKO

Mara baada ya mchezo huo kikosi cha Wanasimba kimerejea jijini Dar es Salaam, huku kocha wao mkuu Fadlu akiamuru moja kwa moja nyota wote kuingia kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya Namungo ambao unatarajia kupigwa Ijumaa saa 10 jioni Uwanja wa KMC Complex.
Kuelekea mchezo huo kikosi cha mnyama leo Alhamisi kimefanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa KMC Complex, ambapo wachezaji wote wameshiriki mazoezi hayo kikamilifu na wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo ambao wameweka wazi wanatarajia utakuwa mgumu.
Uongozi wa Simba umetamba kuwa kwa sasa kila mchezo ulio mbele yao wanaupa umuhimu mkubwa lengo likiwa kuibuka na ushindi na kupata pointi tatu.
ALICHOSEMA KOCHA SIMBA

Kupitia mkutano wa kabla ya mechi kocha Msaidizi wa timu hiyo, Darian Wilken amesema mchezo dhidi ya Namungo utakuwa mgumu, lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi watakapocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Kocha Wilken amesema Namungo ni timu nzuri, hasa ikichangiwa na kuwa na Kocha mpya ambaye amewaongezea morali wachezaji wake, lakini akatamba kuwa watakutana na Simba ambao ni wapinzani bora zaidi.
Wilken ameongeza kuwa pamoja na ugumu wa ratiba wa kucheza mechi karibu karibu kunakosababisha wachezaji kupata majeraha, lakini ametamba kuwa wao ni timu kubwa na wanatakiwa kupambana katika kila mchezo, ili kupata pointi tatu.
“Utakuwa mchezo mgumu, Namungo ni timu imara yenye wachezaji wazoefu na tayari imepata kocha mpya, lakini Simba ni kubwa zaidi na ipo tayari kupambana hadi mwisho kwa ajili ya kupata pointi tatu,” amesema Kocha Wilken.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinda mlango wa timu hiyo, Ally Salim amesema kwa upande wao wapo tayari kupambana hadi mwisho kwa ajili ya kupata pointi tatu. Ally amesema Namungo ina wachezaji wengi wazoefu ambao wengi walikuwa nao lakini Simba ni kubwa na pamoja na changamoto zote ila wapo tayari kwa ajili ya pointi tatu muhimu za nyumbani.
“Sisi tupo tayari kwa mchezo, Namungo tunawaheshimu ni timu bora lakini Simba ni bora zaidi na tupo kwa ajili ya kupigania alama tatu,” amesema Ally Salim.
Ikiwa Simba iliyo chini ya kocha Fadlu Davis itapata ushindi watazidi kujiweka kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi ambapo watakuwa wamefikisha pointi 19 katika michezo yao nane ambayo watakuwa wamecheza, wakishinda mechi sita wamepata sare mchezo mmoja na kupoteza mchezo mmoja.

