SAA zikiwa zinahesabika kuelekea Kariakoo Dabi, wenyeji wa mchezo huo ambao ni Simba wamebainisha kuwa hawana hofu itakuwa ni mwendo wa Ubaya Ubwela uliochanganyika na Pumzi ya Moto kwenye dakika 90 za kazi katika msako wa pointi tatu muhimu kwa watani hao wa jadi wenye maskani yao wote Kariakoo.
Ipo wazi kuwa Simba yenye maskani yake Msimbazi inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids wao ni wenyeji wa mchezo huo ambapo kwa msimu wa 2024/25 hawajapoteza mchezo ndani ya ligi zaidi ya kuambulia sare ya kufungana mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC, Mwenge.

Yanga yenye maskani yake Jangwani inayodhaminiwa na SportPesa kwenye mechi zake ilizocheza msimu wa 2024/25 haijapoteza zaidi ya kukomba pointi tatu muhimu itakuwa na kazi ya kusaka ushindi mbele ya Simba katika Kariakoo Dabi.
HUYU HAPA SEMEJI

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa siku hazigandi na wanaamini watakutana na wapinzani wao Yanga kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi Oktoba 19 2024 Uwanja wa Mkapa.
Ikumbukwe kwamba kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii hatua ya nusu fainali Uwanja wa Mkapa baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 0-1 Yanga bao la ushindi likifungwa na Maxi Nzengeli ambaye amekuwa kwenye ubora wake ndani ya uwanja.
“Hatukuwa na matokeo mazuri dhidi yao kwenye mechi zetu ambazo zilipita hivyo hilo halitabadilika lakini kwenye mechi ambayo ipo mbele yetu sasa tunahitaji kupata ushindi muhimu na wachezaji wetu wote wapo kamili.”
“Kwenye mchezo wetu dhidi ya nyuma mwiko ambacho tunahitaji ni ushindi hiyo Oktoba 19 2024, wanasema siku zinakimbia hilo lipo wazi na siku hazigandi hivyo tutakutana uwanjani kwa ajili ya msako wa pointi tatu.
“Hayo mengine tunasema zilipendwa na hatuwezi kuzungumzia yaliyopita zaidi tunatazama yale yajayo kwa kuwa kila kitu kinawezekana na mchezo wetu utakuwa na ushindani mkubwa hilo linajulikana lakini kikubwa ni kuona kwamba tunapata matokeo chanya.
“Mashabiki wa Simba hii burudani inawahusu, nipende kuwatoa hofu kuhusu hili kwa kuwa maandalizi yameanza muda mrefu na wachezaji waliingia kambini mapema wakiwa na benchi la ufundi kwa ajili ya kuona namna gani wanakuwa na mbinu za kupata ushindi.”
HAWA HAPA HATIHATI KUIKOSA DABI

Kuna mastaa wa Simba ambao kuna uwezekano mkubwa kuikosa Kariakoo Dabi kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni Ayoub Lakred ambaye hayupo fiti kwa sasa baada ya kupata maumivu kwenye maandalizi ya msimu mpya 2024/25 nchini Misri.
Mbali na Lakred ambaye ni kipa mwamba Aishi Manula ambaye naye ni kipa pia hajawa fiti kwa ajili ya mchezo wa Dabi taarifa zinaeleza kuwa kutocheza kwake mechi kwa muda mrefu kunamuondoa uwepo wake kikosi cha kwanza.
Kwa mujibu wa Ally amesema kuwa beki Abdlazack Hamza ambaye alipata maumivu ya nyama za paja kwenye timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ameanza mazoezi hivyo ni jukumu la benchi la ufundi kumtumia ama la kulingana na ripoti ya madaktari.
Ellie Mpanzu ingizo jipya ndani ya Simba bado usajili wake kwa wachezaji wa ndani haujakamilika ni mpaka pale dirisha dogo litakapofunguliwa.

Yusuph Kagoma na Mzamiru Yassin hawa walikuwa nje kwa muda kutokana na kutokuwa fiti ila wameanza mazoezi na timu ni suala la benchi la ufundi kuamua ikiwa watapata nafasi kikosi cha kwanza kwenye Kariakoo Dabi.
MATOKEO YA SIMBA
Simba 3-0 Tabora United, Uwanja wa KMC, Agosti 18 2024 ni mchezo wa kwanza kwa Simba kwenye ligi na mtupiaji bao la kwanza ni Che Malone ilikuwa dakika ya 14 akitumia pasi ya Jean Ahoua.
Simba 4-0 Fountain Gate,Uwanja wa KMC, Mwenge ilikuwa Agosti 25 2024. Azam FC 0-2 Simba huu ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Simba kucheza ugenini ulichezwa Uwanja wa New Amaan Complex Septemba 26 2024.
Dodoma Jiji 0-1 Simba ilikuwa Septemba 29 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma walisepa na pointi tatu kwenye mchezo huu mchezo wa tano ilikuwa Simba 2-2 Coastal Union, Uwanja wa KMC, Mwenge walipogawana pointi mojamoja kwenye mchezo huo wakiwa nyumbani.
,

