OKTOBA 19 2024 mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya wababe wawili wenye maskani yao Kariakoo ambao ni Simba kutoka mtaa wa Msimbazi na Yanga kutoka mtaa wa Jangwani unasubiriwa kwa shauku kubwa kutokana na kila timu kupambania kupata pointi tatu muhimu.
Yanga inayodhaminiwa na SportPesa itakuwa kwenye kazi ya kuendeleza rekodi yake ya msimu wa 2023/24 kwa kukomba pointi sita mazima Kariakoo Dabi walipokutana ndani ya uwanja katika dakika 180. Tambo zimetawala kwa kila timu kuelekea Oktoba 19 2024 kwa kila mmoja kubainisha kuwa hesabu ni pointi tatu.

Simba ambayo kwa sasa inanolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids ilikwama kusepa na pointi tatu mbele ya Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi mchezo wa mzunguko wa kwanza ubao ulisoma Simba 1-5 Yanga na ule wa mzunguko wa pili ilikuwa Yanga 2-1 Simba. Ndani ya dakika 180 ni mabao 9 yalifungwa huku Yanga ikifunga mabao 7 na Simba ikifunga jumla ya mabao mawili.
Wafungaji pekee kwa Simba ni Kibu Dennis alitumia pasi ya Saido Ntibanzokiza mzunguko wa kwanza na Michael Fred alitumia pasi ya Clatous Chama ilikuwa ni mzunguko wa pili ambapo Simba ilipoteza kwa mara nyingine tena uwanjani.
SEMAJI TAMBO ZAKE HIZI HAPA

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amebainisha kuwa mchezo huo ni muhimu kupata pointi tatu kutokana na ushindani uliopo na maandalizi yameanza kuelekea kwenye mchezo huo.
“Tuna kazi Oktoba 19 ambapo tutakuwa Uwanja wa Mkapa kwenye Kariakoo Dabi, huu sio mchezo mwepesi kutokana na ushindani uliopo na hatukuwa na matokeo mazuri msimu uliopita hilo lipo wazi na sasa tunakwenda kupambana ili kupata matokeo mazuri.
“Maandalizi yanaendelea vizuri na tayari timu ipo kambini kwa ajili ya mchezo wetu ili kuona kwamba tunapata matokeo mazuri, muda uliopo kwa sasa ni wachezaji kuwa tayari kuelekea kwenye mchezo huo, mashabiki wajitokeze kwa wingi na tupo tayari.”
MWENDO WA SIMBA NDANI YA LIGI

Simba 3-0 Tabora United mchezo huu ulichezwa Uwanja wa KMC, Mwenge ilikuwa Agosti 18 2024 ni mchezo wa kwanza kwa Simba kwenye ligi na mtupiaji bao la kwanza ni Che Malone ilikuwa dakika ya 14.
Simba 4-0 Fountain Gate, huu ulikuwa ni mchezo wa pili kwa Simba ulichezwa Uwanja wa KMC, Mwenge ilikuwa Agosti 25 2024. Azam FC 0-2 Simba huu ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Simba kucheza ugenini ulichezwa Uwanja wa New Amaan Complex Septemba 26 2024.
Dodoma Jiji 0-1 Simba ilikuwa Septemba 29 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma walisepa na pointi tatu kwenye mchezo huu. Simba 2-2 Coastal Union kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC, Mwenge.
Safu ya ushambuliaji ya Simba imefunga mabao 12, Leonel Ateba, Jean Ahoua, Valentino Mashaka hawa wote wametupia mabao mawilimawili na ukuta umeruhusu mabao 2.
YANGA HAWAPOI
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amebainisha kuwa wanatambua umuhimu wa mchezo wao dhidi ya Simba na wapo tayari kwa ajili ya kupata pointi tatu muhimu katika uwanja kutokana na maandalizi ambayo yanafanyika.
“Tunakazi kubwa kuelekea kwenye mchezo wetu wa Kariakoo Dabi na malengo ni kupata pointi tatu muhimu kwenye mchezo wetu hilo lipo wazi na benchi la ufundi linafanyia kazi makosa yaliyopita kwenye mechi zetu ili kuwa bora.
“Mchezo wa Kariakoo Dabi unazidi kujitangaza nah ii ni muhimu na afya kwa soka letu, watu kutoka sehemu mbalimbali wanakuja kutazama mchezo huu hii inatokana na uimara wa ligi pamoja na uwekezaji hivyo tunakwenda kwenye mchezo huu kwa tahadhari kubwa na lengo ni kupata pointi tatu.”
MWENDO WA YANGA 2024/25

Kagera Sugar 0-2 Yanga mchezo huu ulichezwa Uwanja wa Kaitaba, Agosti 29 2024 na mtupiaji wa bao la kwanza ni Maxi Nzengeli ndani ya Yanga kwenye ligi. Ken Gold 0-1 Yanga huu ulikuwa mchezo wa pili kwa Yanga ugenini ilikuwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya mtupiaji alikuwa ni Ibrahim Bacca ambaye alitumia pasi ya Aziz Ki Septemba 25 2024.
Yanga 1-0 KMC, mchezo wa kwanza wakiwa Uwanja wa Azam Complex msimu wa 2024/25 ilikuwa Septemba 29 2024.
Yanga 4-0 Pamba Jiji ushindi mkubwa kwa Yanga ndani ya 2024/25 walikuwa Azam Complex ilikuwa Oktoba 3 2024. Kwenye mechi nne za Yanga haijaonja chungu ya kupoteza wala kuambulia sare ndani ya uwanja.

