Bacca VibeBacca Vibe

MABINGWA mara 30 ndani ya Ligi Kuu Bara, Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu Miguel Gamondi wametibua rekodi yao ndani ya dakika 180 kwenye mechi mbili mfululizo za ligi msimu wa 2024/25 kwa kukwama kuvunja rekodi yao ya msimu wa 2023/24.

Ikumbukwe kwamba msimu wa 2023/24 chini ya Gamondi ilisepa na pointi sita mazima kwenye mechi mbili za mwanzo huku safu ya ushambuliaji ikifunga jumla ya mabao 10 ikiandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza kwenye msimu kufunga mabao mengi uwanjani kwenye mechi za ligi.

Ipo wazi kwamba timu hiyo inayodhaminiwa na SportPesa imekuwa kwenye mwendo mzuri ndani ya uwanja ikipata ushindi na kuvunja rekodi mbalimbali imeanza msimu kwa mechi mbili za ligi zote ikiwa ugenini.

JIKUMBUSHE ILIVYOKUWA 2023/24

JOB
DICKSON Job mfungaji wa bao la kwanza Yanga 2023/24. Source: Yanga.

Rekodi za Yanga kwa mechi za mwanzo msimu wa 2023/24 ilikuwa namna hii:- Yanga 5-0 KMC mchezo huu ulichezwa Uwanja wa Azam Complex ulikuwa wa kwanza kwa Yanga ndani ya msimu ambapo mfungaji wa bao la kwanza alikuwa beki Dickson Job.

Kwenye mchezo huu Yanga ilifungua pazia la safari kuufuata ubingwa na iliendelea na mwendo huo kwa kuhitimisha msimu ikiwa na jumla ya pointi 80 kibindoni baada ya kucheza jumla ya mechi 30. Huu ulichezwa Agosti 23 2023.

Kete ya pili ilikuwa Yanga 5-0 JKT palepale Uwanja wa Azam Complex Yanga ilikomba pointi tatu mazima na kichapo cha 5G kiliendelea kwa wapinzani wao. Ndani ya dakika 180 safu ya ushambuliaji ya Yanga ilifunga mabao 10 na safu ya ulinzi haikuruhusu kufungwa kwenye mechi zake zote mbili ambazo ilianzia ikiwa nyumbani.

NGOMA IMEANZA KIVINGINE 2024/25

Nzengeli
Maxi Nzengeli mfungaji wa bao la kwanza Yanga 2024/25. Source: Yanga.

Ngoma imeanza kivingine kwa msimu wa 2024/25 ambapo mchezo wa kwanza Yanga ilianzia ugenini, Uwanja wa Kaitaba baada ya dakika 90 ubao ulisoma Kagera Sugar 0-2 Yanga.

Bao la kwanza la Yanga lilifungwa na kiungo mshambuliaji Maxi Nzengeli kwenye mchezo huo akitumia pasi ya Pacome ambaye naye ni kiungo wa kazi chaguo la kwanza la Gamondi.Mchezo wa pili kukamilisha dakika 180 ilikuwa dhidi ya Ken Gold.

Mchezo wa pili Yanga ilicheza Uwanja wa Sokoine Mbeya ambapo baada ya dakika 90 ubao ulisoma Ken Gold 0-1 Yanga bao likifungwa na Ibrahim Hamad Bacca akiwa ni beki wa kwanza ndani ya Yanga kufunga bao msimu wa 2024/25.

HAPA NDIPO TOFAUTI ILIPO

CHAMA
CLATOUS Chama kiungo wa Yanga dhidi ya Ken Gold msimu wa 2024/25. Source: Yanga.

Tofauti iliyopo ni kwenye matumizi ya nafasi ambazo Yanga inazitengeneza ndani ya uwanja kwa kuwa rekodi zinaonyesha kuwa kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa Uwanja wa Kaitaba ndani ya dakika 45 za mwanzo walitengeneza nafasi 7 zilizokuwa na hatari.

Pongezi kwa kipa wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda ambaye aliokoa hatari nyingi zilizokuwa zikienda langoni mwake licha ya kuruhusu kufungwa mabao mawili kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa mwanzo mwisho.

Kwa upande wa uwanja ni mmoja unaonekana ulikuwa na changamoto kwa Yanga ule wa Sokoine kwa kuwa Kaitaba ni uwanja wa nyasi bandia ambapo Gamondi aliweka wazi kuwa makosa yaliyotokea kwenye mechi zao yatafanyiwa kazi.

USHINDANI KUONGEZEKA

Msimu wa 2024/25 ushindani ni mkubwa kwa timu zote kupambania kombe ambapo kila timu imefanya usajili mzuri na inahitaji matokeo ndani ya uwanja kwenye mechi ambazo wanacheza uwanjani dakika 90 za kazikazi.

Kuhusu ushindani Gamondi aliweka wazi kuwa timu nyingi zimekuwa zikifanya maandalizi makubwa zinapocheza na Yanga ili kupata ushindi kwa kuwa hilo lipo wazi.

“Kila timu inapokutana na Yanga inajahidi kucheza vizuri na kupambana ili kufunga hilo lipo wazi na makocha wamekuwa wakifanya kazi kubwa kuwapa mbinu wachezaji wao na huwa ninawaambia wachezaji kuwa jambo la msingi kwenye mchezo ni kuwa makini na kutumia nafasi ambazo tunazipata.”

DAKIKA 180 MABAO MATATU

Gamondi
MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga 2024/25. Source: Yanga.

Yanga ndani ya dakika 180 safu ya ushambuliaji imefunga mabao matatu huku mchezo waliokusanya mabao mengi ikiwa ni ule dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa Kaitaba. Msimu wa 2023/24 ni mabao 10 walifunga pungufu ya mabao 7 kwenye mechi ambazo wamecheza na safu ya ulinzi bado uimara wake upo palepale kwa kuwa hawajafungwa. Kwenye mechi zote mbili ugenini imeshida na kukomba pointi sita mazima ndani ya uwanja.

 

 

Share this: