MNYAMA Simba kwenye anga la kimataifa amewaka kwa kutimiza malengo ya kutinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho 2024/25 baada ya kupata ushindi kwenye mchezo wao uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Septemba 22 2024.
Dakika 180 Simba imepata jumla ya ushindi wa mabao 3-1 ambapo katika mchezo waliokuwa ugenini walikwama kupata ushindi ubao ulisoma Al Ahli Tripoli 0-0 Simba hivyo walitoshana nguvu na mshindi wa jumla alipatikana kwenye mchezo wa pili uliochezwa katika ardhi ya Tanzania.
Kunakuwa sasa na timu mbili kutoka Tanzania ambazo zimetinga hatua ya makundi kwenye anga la kimataifa kila mmoja kwenye eneo lake analocheza. Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu Miguel Gamondi hawa wapo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga inayodhaminiwa na SportPesa imetinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 7-0 CBE SA ya Ethiopia huku Simba ikitinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho kwa kuwafungashia virago AL Ahli Tripoli ya Libya.

HUYU HAPA KOCHA FADLU WA SIMBA
Fadlu Davids, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa wachezaji walicheza kwa juhudi kubwa uwanjani kutokana na wapinzani wao kuwa na ubora ndani ya uwanja kwa kuwa waliwapa usumbufu uwanjani nje ndani.
“Tulikutana na wapinzani ambao walikuwa na kasi kubwa uwanjani na haikuwa timu ya kubeza kikubwa ni kuona tumefanikiwa kushinda na sasa kazi kwenye hatua inayofuata hatua ya makundi kuna kitu tutakwenda kufanya ili kuwa bora zaidi.
“Unaona tumekuwa na wachezaji wengi ambao bado ni vijana walifanya kazi kubwa kutafuta matokeo tulianza ugenini hatukufanikiwa lakini kuna vingi ambavyo tulijifunza ikiwa ni pamoja na uzoefu pamoja na namna ya kuwakabili wapinzani wetu tukiwa nyumbani jambo ambalo limetupa matokeo mazuri.

HAWA HAPA WATUPIAJI WA MNYAMA
Zilikuwa dakika 90 za kazi kwa wachezaji wa timu zote mbili ambapo mnyama alianza kutunguliwa mapema na Waarabu wa Libya ambao walimpa tabu kipa Mussa Camara huku safu ya ulinzi ikifanya kazi kubwa kutimiza majukumu yake.
Rekodi zinaonyesha kuwa ndani ya dakika 90 wapinzani Al Ahli Tripoli walifanya majaribio yenye hatari mawili, la kwanza ilikuwa dakika ya 16 na la pili ilikuwa dakika ya 88 yote walikuwa ndani ya 18 huku mpigaji ni yuleyule Cristovao Mabululu aliyefunga bao la kuongoza dakika ya 16.
Mabao ya Kibu Dennis dakika ya 36, Leonel Ateba dakika ya 45 na Edwin Balua dakika ya 88 hayo matatu yameipa tiketi Simba kutinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho mbele ya Al Ahli Tripoli ambayo ilianza kufunga bao dakika ya 16 kupitia kwa Cristovao Mabululu na kwenye mchezo huo alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 90.
KOSI LA USHINDI LA MNYAMA

Mussa Camara alianza langoni, Shomari Kapombe, Mohamed Hussen, Abdlazak Hamza, Che Malone,Yusuph Kagoma, Fernandes Mavambo, Leonel Ateba, Jean Ahoua, Joshua Mutale.
Kwa wachezaji wa akiba ni Ally Salim, Nouma, Chamou, Fabrince Ngoma, Okejapha, Awesu Awesu, Steve Muukwala, Edwin Balua.
HUYU HAPA MKANDAJI KIBU

Mkandaji Kibu Dennis ambaye alifunga bao la kuweka usawa kwenye mchezo huo Uwanja wa Mkapa akiwa ndani ya 18 amesema kuwa hesabu kubwa ilikuwa ni kupata ushindi katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.
“Ilikuwa ni muhimu kwetu kushinda yaani ubaya ubwela na kila mchezaji alikuwa anatambua hilo, tunawashukuru mashabiki kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo wetu muhimu na tumepata ushindi ikiwa ni furaha kwetu na mashabiki pia.”
HUYU HAPA SEMAJI
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa walikuwa wanapiga hesabu kubwa kutinga hatua ya makundi jambo ambalo limetimia pongezi kwa wachezaji na benchi la ufundi kufanya kazi kubwa ndani ya uwanja bila kuwasahau mashabiki.
“Mpango mkubwa ilikuwa kutinga hatua ya makundi huo umefanikiwa na imekuwa hivyo, pongezi kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani na wamefanya kazi kubwa kwelikweli mbele ya wapinzani wetu ambao walikuwa imara uwanjani.
“Wachezaji wametimiza majukumu yao kwa kucheza kwa ushirikiano mkubwa na hili ni muhimu kuwa na mwendelezo na sasa tunakwenda kwenye hesabu za kufanya vizuri kwenye hatua ya makundi ambapo benchi la ufundi litakuwa na mwendelezo wa kufanyia kazi makosa yaliyopita.”

