
Akicheza katika mchezo wake wa kwanza ndani ya jezi ya Simba, straika mpya wa timu hiyo, Lionel Ateba ameanza kwa mkwara mzito baada ya kufanikiwa kufunga bao lake la kwanza katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya kikosi cha Al Hilal ya Sudan.
Simba walicheza mchezo huo wa kirafiki Jumamosi, ambao ulipigwa kwenye dimba la KMC Complex, Dar es Salaam na kushuhudia timu hizo zikitoshana nguvu kwa matokeo ya sare ya bao 1-1.
MCHEZO ULIVYOKUWA
Timu zote ziliuanza mchezo huo kwa tahadhari, huku Simba wakionyesha dhamia ya kuibuka na ushindi mapema baada ya kuliandama lango la Al Hilal, huku wapinzani wao wakiwa imara kuzuia mashambulizi.
Mshambuliaji mpya wa Simba, Leonel Ateba aliyejiunga na timu hiyo kutoka ndani ya kikosi cha USM Alger ya Algeria aliipatia Simba bao la kwanza dakika ya 26 ya mchezo baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Ladaki Chasambi kutoka winga ya kulia.
Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika, Simba walikuwa mbele kwa bao 1-0 huku kila timu ikiwa imetengeneza nafasi kadhaa ambazo hazikutumiwa kama ilivyopasa. Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kucheza kwa tahadhari kubwa huku Al Hilal wakionekana kuwa na dhamira ya kusawazisha bao la utangulizi la Simba.
EZZALA AONYESHWA KADI NYEKUNDU
Dakika ya 53 ya mchezo nyota wa Al Hilal, Suliman Ezzala hakuweza kuendelea na mchezo baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kufuatia kumchezea madhambi Augustine Okajepha na kufanya wageni hao wamalize mchezo wakiwa pungufu.
Staa mpya wa Al Hilal, Sergie Pokou aliyesajiliwa kutokea ndani ya kikosi cha ASEC Mimosa alisawazishia Al Hilal bao hilo dakika ya 75 kwa shuti kali nje ya 18 baada ya kumzidi ujanja mlinzi, Kelvin Kijili.
SIMBA KIKOSI KILICHOCHEZA MCHEZO HUO

Kwenye mchezo huo kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davis alionekana kufanya mabadiliko kadhaa ya kikosi chake huku akiwapa nafasi kubwa wachezaji ambao walikuwa hawapati nafasi ya kuanza. Kikosi cha Simba kilikuwa kama ifuatavyo;
Manula (Abel 45′), Kapombe (Kijili 45′), Nouma (Omary 88′), Karaboue (Kazi 85′), Che Malone (Hamza 45′), Kagoma (Mzamiru 60′), Chasambi (Duchu 85′), Fernandex (Okejepha 45′), Ateba (Mashaka 60′), Awesu (Mutale 69′), Kibu (Karabaka 69′)
Walioonyeshwa kadi: Ateba 16′ Okajepha 68′
Ikumbukwe kuwa, Ateba ambaye alikosa michezo yote miwili ya awali ya Ligi Kuu huu unakuwa mchezo wake wa kwanza tangu alipotoka kwenye program maalum za kumuongezea utimamu wa mwili.
Mchezo dhidi ya Waarabu hao wa Sudan, ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya kwa Al Hilal ambapo timu hiyo inatarajiwa kushiriki Ligi Kuu ya Mauritania kutokana na hali ya machafuko ya kisiasa nchini Sudan.
Akizungumzia ubora ambao umeonyeshwa na Ateba, Meneja wa habari na mawasiliano wa Simba ambao wamewahi kulamba udhamini mnono wa Kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa, Ahmed Ally amesema kuwa nyota huyo alikuwa chini ya uangalizi maalum wa programu za utimamu wa mwili kutokana na kuchelewa kujiunga na wenzake na sasa yupo katika hali nzuri ya kupambania kiatu cha dhahabu.
“Wote mtakuwa mashahidi kuwa, Leonel Ateba amejiunga nasi siku chache zilizopita ambapo alifanyiwa vipimo vya afya na amefanya mazoezi kidogo na wenzake kwahiyo huu ni mchezo wa kwanza kwake lakini kaonyesha balaa kubwa. Goli moja ambalo amefunga litampa imani ya kufanya vizuri zaidi, naweza kusema sasa yupo tayari kupambania kiatu cha dhahabu.”
MUTALE MAMBO SAFI, AREJEA RASMI UWANJANI

Baada ya kukosekana kwenye mchezo uliopita dhidi ya Fountain Gate FC kufuatia kuwa na majeraha kiungo mshambuliaji wa Simba, Joshua Mutale amerejesha tabasamu Simba baada ya kurejea rasmi uwanjani kwenye mchezo huo dhidi ya Al Hilal ambapo aliingia uwanjani dakika ya 69 akichukua nafasi ya, Awesu Awesu.
Mutale alipata majeraha katika mchezo wa kwanza pale Simba walipoikaribisha Tabora United katika mchezo wa ufunguzi na kushuhudia mchezaji huyo akishindwa kuendelea na mchezo na kutolewa dakika ya 31 baada ya kupata maumivu ya mguu.

