
Mara baada ya kukosekana kwenye michezo miwili iliyopita ya Simba, straika mpya wa kikosi hicho Lionel Ateba hatimaye mambo yake yameakaa sawa na uongozi wa timu hiyo umetamba kuwa rasmi anatarajiwa kuanza balaa lake kwenye mchezo wao wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Al Hilal.
Waarabu hao wa Sudan tayari wako Tanzania kucheza mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki kama sehemu ya maandalizi ya msimu mpya ambapo timu hiyo inatarajiwa kushiriki Ligi Kuu ya Mauritania kutokana na hali ya machafuko ya kisiasa nchini Sudan.
Akizungumzia utayari wa staa huyo, Meneja wa habari na mawasiliano wa Simba ambao wamewahi kulamba udhamini mnono wa Kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa, Ahmed Ally amesema kuwa nyota huyo alikuwa chini ya uangalizi maalum wa programu za utimamu wa mwili kutokana na kuchelewa kujiunga na wenzake na sasa yupo katika hali nzuri ya kuuwasha moto na wenzake.
“Kama mnakumbuka, Leonel Ateba amejiunga nasi siku chache zilizopita ambapo alifanyiwa vipimo vya afya na amefanya mazoezi kidogo na wenzake kwahiyo tunaangalia maendeleo ya utimamu wake wa mwili juu ya kuanza kutumika rasmi. Na tunatarajia mchezo huu wa kirafiki tutamuona kwa mara ya kwanza akiwasha moto.
KOCHA SIMBA ATENGA SIKU MBILI
Sambamba na hilo Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kikosi kimepata nafasi ya kuingia kambini kwa siku mbili kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo wa kirafiki dhidi ya Al Hilal kutoka Sudan utakaopigwa Jumamosi Uwanja wa KMC Complex.
Ahmed apia amesema tayari wapinzani wao Al Hilal wameshatua nchini na msafara wa watu 34 kwa ajili ya mtanange huo.
MNYAMA BADO ANATAMBA KILELENI

Kikosi cha Simba wameendelea kutamba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Fountain Gate FC, mchezo ambao ulikuwa mchezo wa pili kwao kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Tabora United walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Wanasimba wamekuwa na mwanzo mzuri wa msimu huu wa 2024/25 wakicheza michezo yote miwili katika Uwanja wa KMC Complex unaopatikana Mwenge, Dar es Salaam ambapo mpaka sasa hawajafungwa bao lolote, wakiwa wameweka kambani mabao 7.
UBAYA UBWELA WANAUTAKA UBINGWA

Mara baada ya michezo hiyo miwili Wanamsimbazi wameweka wazi kuwa wameanza taratibu kujipata na malengo yao ni kuhakikisha wanashinda michezo iliyo mbele yao na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kushinda ubingwa msimu huu.
Akizungumzia kikosi chake kuelekea mchezo dhidi ya Al Hilal kocha mkuu wa Wekundu wa Msimbazi, Fadlu Davids amesema: “Ni jambo zuri kwetu kupata matokeo ya ushindi katika michezo yetu hii miwili ya kwanza. Taratibu baada ya kikosi chetu kupata wiki sita za mazoezi pamoja na kucheza mechi kadhaa za kirafiki, zile za Ngao ya Jamii na hizi za ligi, tunaendelea kuongezeka utayari wetu kwa michezo ya Ligi Kuu.
“Malengo yetu ilikuwa kuhakikisha tunaanza vizuri ligi kwa kupata matokeo ya ushindi na tunashukuru kufanikisha hilo. Kikosi chetu kipo kwenye umbo bora la kiushindani na mawasiliano ndani ya uwanjani yameendelea kuimarika, malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda kila mechi ili kujiweka sawa kwenye harakati za kupigania taji la ubingwa,” amesema Kocha Fadlu.
MUTALE KUREJEA UWANJANI MAPEMA

Baada ya kukosekana kwenye mchezo uliopita dhidi ya Fountain Gate FC kufuatia kuwa na majeraha kiungo mshambuliaji wa Simba, Joshua Mutale ameelezwa anaendelea vizuri na atarejea uwanjani mapema.
Mutale alipata majeraha katika mchezo wa kwanza pale Simba walipoikaribisha Tabora United katika mchezo wa ufunguzi na kushuhudia mchezaji huyo akishindwa kuendelea na mchezo na kutolewa dakika ya 31 baada ya kupata maumivu ya mguu.
Mutale ambaye baadaye alifanyiwa vipimo na anatarajiwa kukosekana kwa kipindi cha wiki mbili na mpaka sasa anaendelea na taratibu za matibabu ili kuwahi kurejea kujiunga na wenzake kwa ajili ya maandalizi ya michezo yao ijayo.

